26.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

TAMFI: Sheria inahitajika kukuza sekta ndogo za fedha

WINNIE TerryNA CHRISTINA GAULUHANGA, DAR ES SALAAM

KUTOKUWAPO kwa sheria ya kuongoza sekta ndogo za fedha kumesababisha kuwapo kwa migogoro mingi huku mingine ikisababisha taasisi kadhaa za fedha kushindwa kujiendesha.

Wadau wa fedha hapa nchini wanaona ipo haja ya kuundwa chombo maalumu cha kusimamia shughuli hizo ikiwamo sheria ambazo zitawaongoza kiutendaji.

Shirikisho la Taasisi na Asasi za Fedha Nchini (TAMFI), watapata matumaini mapya endapo muswada wa sheria ya asasi na taasisi zinazotoa huduma za kifedha kwa watu wanaofanya shughuli ndogo na kati utawasilishwa bungeni na kupitishwa kuwa sheria.

Mtendaji Mkuu wa TAMFI, Winnie Terry, anasema kwa miaka mitano sasa taasisi yake imekuwa ikifanya kampeni kubwa kuhakikisha sheria hiyo inakuwapo ili kuziweka imara huduma za sekta ndogo ya fedha inayotegemewa sana na watu wa hali ya chini na kati hasa vijijini.

Winnie anasema taasisi na asasi hizo za fedha kwa wahitaji wadogo zimekuwa zikitoa huduma hiyo muhimu ya ukopeshaji kwa mamilioni ya wahitaji bila kuwapo na sheria wala kanuni za uendeshaji.

Anasema taasisi yake ina matumaini makubwa kwamba kama serikali itapitisha muswada huo ambao wao wamechangia mapendekezo yake, uendeshaji wa huduma hiyo utafuata kanuni na hivyo kuleta tija kwa wananchi na taifa.

Anasema baada ya utafiti wa kina ambao ulionesha udhaifu wa uendeshaji kutokana na kukosekana kwa sheria na kanuni zinazogusa sekta ndogo ya fedha kwa watu wa chini  na kati.

Anasema TAMFI walitengeneza mapendekezo ya muswada wa namna shughuli za ukopeshaji zinavyostahili kuwa na kuuwasilisha serikalini ili kuingizwa katika mchakato wa bunge kutengenezwa sheria.

Anasema walifurahishwa na hatua ya serikali ya kuchukua mapendekezo yao na kutengeneza muswada wa sheria wa asasi na taasisi zinazotoa huduma za kifedha kwa watu wenye kufanya shughuli ndogo na kati wa mwaka 2015.

Winnie anasema TAMFI kwa kushirikiana na taasisi iliyo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu inayotetea mazingira bora ya biashara (BEST-AC) imekuwa ikishawishi kuboreshwa kwa huduma ya sekta ndogo ya fedha kwa kuundwa sheria na kanuni zinazoambatana nazo ili kuiboresha.

“Haja ya kuwapo kwa sheria hii kunatokana na kuwapo kwa sera ya fedha ya sekta ndogo iliyotengenezwa miaka 14 iliyopita ambayo haina sheria inayoendana na ukuaji wa sekta hiyo inayobeba uchumi wa vijijini na kiasi kidogo cha watu wa mjini,”anasema Winnie.

Anasema ili sekta hiyo ikue kwa namna inavyotakiwa ipo haja ya kuwa na sheria zitakazobeba sekta hiyo katika hatua nyingine ya ukuaji wake.

“Tumekuwa tukipigania sheria na kanuni zake zitungwe ili sekta iweze kukua kwa uwazi na kulinda walaji wake. Kutokuwapo kwa sheria kunafanya shughuli za uwekezaji katika sekta hii kuwa za shaka na hivyo kuwazuia wakopeshaji na wawekezaji kuwa huru,” anasema.

Pia anasema uanzishwaji wa benki za kuhudumia watu wa chini na wa kati kwenye sekta hiyo umekuwa changamoto kubwa na hii inaweza kueleweka kwa mfumo tata wa ukopaji na mitaji.

Winnie anasema ili kuharakisha ukuaji wa sekta hiyo ipo haja ya kuwa na sheria na kanuni za kuendesha ili kuwapo na uwazi katika huduma hiyo katika soko.

Anasema asilimia 70 ya Watanzania hawana huduma za kibenki, taasisi za fedha kwa ajili ya watu wa kati na chini (MFIs) ndizo zinazosaidia na ndiyo maana ipo haja ya kuwapo kwa mfumo wa sheria unaozunguka uendeshaji wa sekta ya fedha kwa ajili ya watu wa kati na chini.

Anasema mbali ya Vicoba kuwa ndiyo njia ya kuwekeza na kukopeshana inayotumika sana vijijini na baadhi ya maeneo ya mijini, vinashamiri bila kuwapo na taasisi wala sheria ya  kuangalia mwenendo wake.

“Ni dhahiri kukosekana kwa sheria kumechangia kwa kiasi kikubwa kuwepo na ugoigoi katika uendeshaji wake, kutokuwepo kwa mfumo wa uendeshaji wa kitaasisi, uwezo mdogo wa kuendelea, kuwapo na ushindani usiokuwa na sababu na kutokuwa na  nguvu ya kupata fedha kutoka katika vyanzo  mbalimbali,”anasema Winnie.

Anataja changamoto nyingine inayosababishwa na kutokuwapo kwa sheria na kanuni ni kuzuka wadau wanaokuwa na madeni makubwa kunakochangiwa na ushindani wa soko miongoni mwa asasi.

Pia anasema baadhi ya asasi zinatumia vibaya maridhiano ya mikopo kama dhamana ya wadau wakati wakikopa kwa kutokuwa wastaarabu katika ukusanyaji wa marejesho.

Pamoja na changamoto hizo Winnie anasema TAMFI ina matumaini kwamba Serikali ya Awamu ya Tano itawezesha kupatikana kwa sheria kutokana na kasi yake na hasa katika masuala yanayogusa fedha.

“Ni matumaini yangu kwamba serikali mpya itasaidika katika kuweka mazingira bora ya uendeshaji wa sekta hii ndogo na hivyo kupunguza hofu kwa watoaji mikopo na wakopaji,”anasema Winnie.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles