29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

TAMASHA LA KUPIGANA NA NYANYA LAHARIBU TANI 160

JOSEPH HIZA NA MASHIRIKA YA HABARI

NYANYA ni kiungo cha chakula, si tu hutoa ladha nzuri katika mchuzi, kachumbari au mboga bali pia zina faida kubwa katika mwili wa binadamu.

Miongoni mwa faida hizo ni uwapo wa vitamin C, A na K pamoja na madini mengine kama vile potassium, manganese, ufumwele na kadhalika.

Virutubisho hivyo pamoja na mambo mengine hupunguza uwezekano wa uoni hafifu, kuzuia saratani ya kibofu, utumbo, mapafu, koo, mdomo na kizazi.

Pia husaidia kusafisha ngozi na kupunguza kiwango cha sukari katika damu na ulaji mwingi kusaidia upatikanaji wa usingizi mzuri, uimara wa mifupa, nywele na kupunguza maumivu kwa kutaja chache.

Mbali ya hilo, kilimo cha zao hilo kina faida za kiuchumi, kutokana na ukweli kuwa ni tunda linalonunulika kutokana na kuwa sehemu ya mlo wa kila siku.

Wakati ikiwa hivyo, nchini Hispania kiungo hicho pia hutumika kwa matumizi mengine ya kujifurahisha, ambayo kamwe katikia mataifa yetu yanayoendelea yangehesabiwa uharibifu wa chakula.

Ni kutokana na kutumika katika tamasha maarufu la kupigana na chakula liitwalo La Tomatina, ambalo hufanyika Jumatano ya mwisho ya mwezi Agosti.

Hivyo, mwaka huu lilifanyika Agosti 30 katika mji wa Bunoi karibu na Valencia chini ya ulinzi mkali kutokana na uwapo wa hofu ya mashambulizi kutoka kwa wanamgambo wenye itikadi kali za kidini.

Katika tamasha hilo, watu mbalimbali wageni na wenyeji wazee, wakubwa kwa watoto hukusanyika sehemu moja na hupigana kwa kurushiana nyanya limekuwa likifanyika tangu miaka ya 1940.

Katika tamasha hilo mwaka huu, nyanya tani 160 zilitumika katika mapigano hayo ya kurushiana tunda hilo yaliyodumu takribani saa moja, huku kila mmoja akigeuka mwekundu.

Aidha, limekuwa likifanyika katika nchi nyingine duniani kama vile Chile, Amerika ya Kusini, ambako lilitangazwa kuwa rasmi mwaka 2013 katika baadhi ya manispaa za mji ikiwamo mji mkuu wa Santiago baada ya watu fulani kipindi hicho kuanza kurushiana nyanya kwa lengo la kujifurahisha.

Maelfu kwa maelfu ya watu kutoka sehemu mbalimbali duniani hujazana  kushiriki mapambano haya makubwa ya vyakula ambapo zaidi ya tani 100 za nyanya zilizoiva hutumika kama silaha ya mapigano mitaani.

Sherehe hii inayodumu kwa muda usiopungua wiki moja, hujumuisha muziki, magwaride, uchezaji muziki na maonesho ya kucheza na moto ya aina mbalimbali ikiwa ni pamoja na ya kulipua baruti zenye kutoa mwanga wa rangi mbalimbali za kuvutia.

Kila mwaka, watu wanaokadiriwa kuwa kati ya 40,000 hadi 50,000 hushiriki, na hivyo kuifanya idadi ya watu ya mji wa Bunol kuongeza marudufu kwa vile una wakazi 9,000 tu.

Idadi ya washiriki wa mapambano haya imekuwa ikiongezeka kila mwaka na kutokana na hilo, ukumbi wa Halmashauri ya Mji wa Bunol, mwaka 2013 uliamua kuanzisha mtindo wa watu kuingia kwa kulipa tiketi, jambo ambalo miaka ya nyuma halikuwapo.

Kutokana sherehe hiyo kubwa ya kitalii nchini Hispania, watu wanaokwenda kwa lengo la kuhudhuria huwa kubwa kuliko uwezo wa mji huo kuhudumia malazi ya watu.

Hivyo, baadhi ya watu hufika mji wa jirani wa Valencia uliopo kilomita 38 kutoka Bunol ambapo huenda na kurudi baada ya sherehe hizo kwa mabasi ya abiria.

Ni sherehe inayouacha mji huo ukiwa na kila aina ya uchafu ndani ya muda mfupi sana unaotokana na mabaki ya nyanya zinazotumika kwenye mapambano.

Katika kujitayarisha kwa mrundikano huo mkubwa wa uchafu, wenye maduka hujitayarisha kwa kuziba maeneo ya mbele ya maduka yao na hata ya maofisi kwa makaratasi maalumu ili kuhakikisha sherehe hizi haziwakwazi watu wanaokwenda kwenye maduka yao kibiashara.

Kwa kawaida tamasha huanza saa tano asubuhi, wakati malori mengi makubwa yanapowasili kwenye eneo la katikati ya mji na kuanza kushusha mizigo mikubwa na mingi ya nyanya zilizowiva.

Eneo linalofahamika sana kwa shughuli hii ni la Plaza del Pueblo. Nyanya hizi hununuliwa kutoka mji mwingine, ambako zao hili hulimwa kwa wingi na hivyo kufanya bei yake kuwa ya chini.

Ishara maalum ya kuanza kwa pambano hutolewa; ambayo ni kufyatuliwa kwa bunduki ya maji na hapo kelele hutawala ghafla na hapo kila mtu kumshambulia mwingine.

Washiriki hushauriwa kuvaa miwani ya kulinda macho yao dhidi ya majimaji ya nyanya hizo, pamoja na mipira ya mikononi.

Sheria nyingine ni kwamba washiriki wote hawaruhusiwi kuja na kitu chochote kinachoweza kumletea madhara mwingine, kama vile chupa, bilauri au kikombe cha udongo.

Ingawa kuna sheria ya kuzuia mtu kuchana nguo ya mtu mwingine wakati wa mapambano haya, lakini mara nyingi washiriki hushindwa kuheshimu hili na imekuwa ni kawaida kuona watu wakichaniana nguo.

Baada ya saa moja, mapambano hufika mwisho wakati bunduki za maji zinapofyatuliwa tena kuonesha ishara ya kumaliza mapambano. Inapotolewa ishara hiyo, hakuna nyanya zaidi zinazoruhusiwa kurushwa.

Mtu anapoona hali ya mji huo muda mfupi kabla ya mapambano hayo ya nyanya kuanza na akaona muda mfupi baada ya kipenga cha kusitisha mapambano hayo, anaweza akashangaa kwa namna mji huo unavyobadilika kwa muda mfupi. Baada ya kumalizika kwa mpambano shughuli za kusafisha mji huanza.

 Tamasha hili lilianzaje?

Kumbukumbu zinaonesha huenda sherehe hizi zilianza mwaka 1944 au 1945, lakini zikapigwa marufuku wakati wa utawala wa Jenerali Fransisco Franco.

Inaaminika zilianza wakati wa magwaride ya vijana ambapo watu waliotaka kushiriki walitakiwa kwanza kupambana kwenye eneo la Plaza del Pueblo.

Kulikuwa na vibanda vya kuuza mbogamboga katika eneo jirani, makundi ya watu waliokuwa wakifanya mchezo huu wa kushambuliana, wakajikuta wakivamia mabanda na kuchukua nyanya na kuanza kurushiana.

Polisi walilazimika kuingilia kati na kuwalazimisha wale waliohusika na uharibifu huu, kulipa fidia.

Kumbukumbu zinaonyesha hii ni moja ya vile vinavyoweza kuonekana kama vyanzo ama chimbuko za kuanza kwa sherehe hizi za Tomatina.

Inasemekana mwaka uliofuatia, mapambano hayo yalirudia siku ileile ya Jumatano ya  Agosti lakini safari hii walikuja na vikapu vyao vya nyanya kutoka majumbani kwao.

Sherehe hizi zikapigwa marufuku na kuruhusiwa mara kwa mara baada ya shinikizo la wakazi waliozizoea.

Baadaye manispaa za miji zilizikubali katika miaka ya 1980 na kuchukua rasmi matayarisho ya sherehe hii hadi leo hii ambayo imegeuka sehemu ya utalii wenye kuingiza fedha nyingi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles