30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

TALAKA YA ‘EU’ INAPOILAZIMISHA UINGEREZA KUJIPANGA UPYA

WAINGEREZA walipopiga kura ya kujiondoa kutoka Jumuiya ya Ulaya (EU), wengi walidhania kuwa lingekuwa jambo rahisi tofauti na uhalisia wa mchakato wa kujiondoa ulivyo mgumu pengine kuliko hata kujiunga. Walifanya uamuzi huo chini ya aliyekuwa Waziri Mkuu David Cameroon ambaye muda mfupi baadaye alijiuzulu, mchakato ukafanyika kwa mujibu wa Katiba akapatikana Waziri Mkuu wa sasa Theresa May aliyenyakuwa nafasi hiyo baada ya mpinzani wake wa karibu Boris Johson, mhafidhina aliyepinga kwa nguvu zote kubaki kwa UK kwenye Jumuiya hiyo kujiondoa kwenye kinyang’anyiro, lakini baadaye alikabidhiwa rungu la kusimamia mambo ya nje katika Serikali mpya. 

May akashika rasmi hatamu na kutamka kwamba hatoitisha uchaguzi wa mapema kabla ya muhula kumalizika mwaka 2020, lakini mgawanyiko wa msimamo kuhusu mchakato wa kujiondoa EU umemlazimisha Waziri Mkuu huyo kutangaza uchaguzi wa mapema mwezi mmoja na ushei kutoka sasa itakapotimu Alhamisi ya Juni 8.

Kwa mujibu wa utaratibu Waziri Mkuu akiitisha uchaguzi wa mapema kabla ya wakati kutokana na sababu atakazotoa, anatakiwa kupata idhini ya theluthi mbili ya wabunge wote ingawa hatua yake inaonekana kama kamari hatari kwa upande wake lakini alitamka kuwa mazungumzo ya kujitoa EU yanapozidi kushika kasi Uingereza inahitaji kuwa na msimamo mmoja usiokinzana na kukanganya mchakato huo. Nia hiyo ya Theresa May imeungwa mkono na wabunge kwa idadi ya kura 522 dhidi ya 13 na pia alimtaarifu rasmi Malkia kuhusiana na uamuzi huo, akibainisha kuwa Waingereza wanaelekea kuelewa hitaji la mchakato wa kujiondoa EU lakini figisu ziko bungeni na serikalini hivyo ni muhimu kuweka mambo sawa, akiamini kwamba chama chake kitashinda na kumpa nguvu zaidi ya kusimamia mchakato huo bila upinzani. 

Lakini upande wa pili wapinzani wake wanapanga kutumia fursa hiyo kupiku kuburuzwa kama wanavyodai kwamba nafasi hii tamu si ya kuikosa, ili kusimika Serikali itakayozingatia maslahi ya Taifa katika kujiondoa EU tofauti na ilivyo sasa huku chama hasimu cha Labour chini ya kiongozi wake Jeremy Corbyn kimeshapanga mikakati ya siri kwenye kikao chake cha Kamati Kuu. Kuna mkanganyiko katika suala zima la uchaguzi ingawa May anatarajiwa kushinda lakini ikumbukwe kuwa aliupata Uwaziri Mkuu kwa nasibu baada ya Boris kujiondoa na kumdondoshea ngekewa.

Ndiyo maana wapinzani wake wanadai kuwa hajiamini hususani kutokana na kukataa kushiriki midahalo kwenye luninga kuelekea uchaguzi huo kama ilivyo ada, huku wakienda mbali zaidi kwa kutaka midahalo iendeshwe na May awekewe kiti chake na asipohudhuria atajidhihirisha kuwa amekacha kutokana na kutojimudu. Utaratibu unaotakiwa kuzingatiwa ili kupiga kura ni pamoja na kuandikishwa waliotimiza umri wa miaka 18, raia halali wa Uingereza na kama anaishi nje ya nchi lazima awe alijiandikisha kupiga kura ndani ya miaka 15 iliyopita, kujiandikisha kusizidi siku ya mwisho ya Mei na wanaoishi katika maeneo mawili, mathalani wanachuo, wanaweza kujiandikisha kote lakini siku ya kupiga kura wanatakiwa kutumia sehemu moja tu.

Kimchakato kutoka tarehe ya leo siku nne zijazo wagombea wote wanapaswa kuwasilisha nyaraka za kuteuliwa na vyama vyao, pamoja na kuchapishwa wasifu wao na ugawaji wa vifaa vya kupigia kura na ifikapo Juni 8 kura zitapigwa kuanzia saa moja asubuhi hadi saa nne usiku, Juni 13 Bunge jipya la 57 litakutana kwa mara ya kwanza na siku sita baadaye litazinduliwa rasmi. Mchuano mkubwa ni kati ya Theresa May wa chama cha Conservative na Jeremy Cornby wa chama cha Labour ambapo vyama hivyo vilipishana kwa asilimia 6.4 tu katika uchaguzi wa mwisho ulionyakuliwa na Conservative chini ya David Cameroon.  Kihistoria vyote ni vyama vikuu tangu mwaka 1922 na kuanzia mwaka 1935 ndivyo vilivyotoa mawaziri wakuu wa Uingereza hadi sasa. 

Lakini pia usimsahau Waziri Mwandamizi wa Scotland, Nicola Strugeon wa Scottish National Party aliyedhamiria kuanzisha mchakato wa kujitenga na Falme ya Uingereza jaribio lililozimwa awali na linalopingwa na Waziri Mkuu May. Wagombea wengine ni pamoja na wa Ireland ya Kaskazini wakiwamo Arlene Foster wa Democratic Unionist Party na Gerry Adams wa chama cha Sinn Féin wanaotarajiwa kutikisa uchaguzi huo.

Ukiutazama uchaguzi huu uliosababishwa na mchakato wa kujiondoa EU kuanza rasmi kwa mujibu wa utaratibu, kwa Taifa hilo kuanzisha mchakato wa miaka miwili ambao ukikamilika kwa wakati ifikapo Machi mwaka 2019 Uingereza haitakuwa mwanachama, ingawa si rahisi kama inavyodhaniwa kwani ikishajitoa UK inapaswa kusimamia maslahi yake katika uwiano wake na nchi zilizosalia ndani ya umoja huo, hususani kwa makubaliano ya kibiashara na sekta nyingine kwa kuwa sasa itakuwa ikiafikiana na nchi moja moja na si umoja mzima, suala litakalogeuka kipaumbele cha kampeni wakati wapinzani wa ‘Brexit’ wakisubiri kwa hamu kutumia nafasi hiyo kukwamisha kujiondoa. 

Lakini May akishinda atapeta kwani hatahitajika kuitisha uchaguzi mwingine hadi mwaka 2022, ni subira ya kukaba pumzi hadi siku uchaguzi utakapofanyika mwezi mmoja ujao!

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles