24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

TAKWIMU WAELEZA SARAFU YA TANZANIA ILIVYOSHUKA

PATRICIA KIMELEMETA NA LEONARD MANG’OHA


OFISI ya Taifa ya Takwimu (NBS) imesema thamani ya sarafu ya Tanzania imeshuka ambako kwa sasa uwezo wa Sh 100   katika kununua bidhaa umeshuka hadi   Sh 92.18.

Imesema pia kuwa mfumuko wa bei umepanda na kuathiri zaidi bidhaa za chakula ukiwamo mchele, matunda na mtama.

Kwa sababu hiyo  baadhi ya wasomi waliozungumza na gazeti hili wamesema hali hiyo inaweza kusababisha   maisha kuwa magumu hivyo ni muhimu   serikali ichukue hatua  kukabiliana na hali hiyo.

Taarifa ya NBS

Akizungumza na waandishi wa habari   Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Takwimu za Jamii na Sensa ya Watu kutoka NBS, Ephraim Kwesigabo, alisema bidhaa ambayo mtu alikuwa anainunua   kwa Sh 100  kipindi kilichopita, hivi sasa  hataweza kuinunua kwa sababu uwezo wa shilingi umeshuka.

“Kitu ambacho ulikuwa na uwezo wa kukinunua kwa Sh 100 wakati uliopita, hivi sasa   huwezi kukinunua kwa fedha hiyo, kwa sasa utahitaji kuongeza Sh 8.82  ndiyo ununue   kitu hicho,” alisema.

Akizungumzia mfumuko wa bei na huduma nyinginezo, alisema umeongezeka hadi kufikia asilimia 5.3 kwa  Septemba kutoka asilimia tano kwa Agosti.

Alisema mfumuko huo ulitokana na ongezeko la bei  za vyakula na bidhaa zisizo za vyakula.

“Bidhaa zilizochangia ongezeko hilo ni pamoja na dagaa ambazo  zilizoongezeka kwa asilimia 7.6, matunda makavu kama nazi asilimia 3.1, viazi vitamu 3.0, mchele 1.5.

“Nyingine ni    ndizi za kupika asilimia 1.5, bidhaa zisizo za vyakula zilizochangia ongezeko hilo kwa fahirisi ni mkaa asilimia 4.0, dizeli 2.4 na petrol 0.6,”alisema Kwesigabo.

Alisema mfumuko wa bei ya   vyakula nyumbani na migahawani kwa Agosti ulikua asilimia 9.1 na   Septemba uliongezeka hadi kufikia asilimia 9.8 huku bidhaa zisizo za vyakula ukibakia kuwa asilimia 3.1.

“Mfumuko wa bei kwa taifa kwa kipimo cha mwaka unapima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma nyinginezo zinazotumiwa na kaya binafsi,” alisema.

Alisema fahirisi za bei zimeongezeka hadi 108.48 kwa   Septemba 2017 kutoka 103.03 kwa   Septemba 2016, hivyo  mfumuko wa bei za bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa   septemba 2017 umeongezeka hadi kufikia 9.3 kutoka asilimia 8.6 ilivyokuwa  Agosti 2017.

Alisema mfumuko wa bei ya bidhaa ambao haujajumuisha vyakula na nishati kwa   Septemba 2017 ulipungua kidogo hadi kufikia asilimia 1.7 kutoka asilimia 1.8 kwa Agosti 2017.

WASOMI

Wakizungumza na MTANZANIA jana, baadhi ya wachumi kutoka vyuo mbalimbali nchini walisema kitendo cha kushuka thamani ya sh 100 kinaongeza umaskini.

“Katika masuala ya ununuzi, nguvu ya shilingi imeshuka, hali ambayo inaweza kuongeza umaskini hasa kwa wananchi wenye kipato kidogo ambao wanaishi chini ya dola moja,”alisema Mhadhiri Dk. Prosper Ngowi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe   Morogoro.

Alisema kutokana na hali hiyo, mkakati wa serikali wa kupunguza umaskini unaweza kushindikana   kutokana na wananchi wake kushindwa kufanya ununuzi kwa gharama nafuu.

Dk. Ngowi alisema   serikali inapaswa kuliangalia suala hilo kwa  makini kwa sababu linaweza kuchangia kuongezeka  umaskini kutokana na wananchi  kushindwa kufanya ununuzi kwa Sh 100.

Profesa Damian Gabagambi kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine Morogoro (SUA), alisema kutokana na takwimu hizo hali ya maisha ya wananchi itaporomoka na wataishi katika mazingira magumu.

Alisema kulingana na kipato cha watanzania, wananchi watapata bidhaa chache tofauti na   awali ambako walikuwa wanapata bidhaa nyingi zinazokidhi mahitaji.

Alisema   hali ya maisha ya watanzania itarudi nyuma na kuwa duni hali ambayo inaweza kuchangia umaskini kuongezeka.

“Ongezeko la mshahara la kila mwaka ni muhimu kwa sababu linasaidia wafanyakazi kupata mahitaji hata kama kuna hali ngumu ya maisha.

“Thamani ya shilingi ya mwaka huu haiwezi kulingana na thamani ya kiasi cha fedha kwa kila mwaka,” alisema Gabagambi.

Alisema  shilingi moja ya mwaka jana ina nguvu kuliko ya mwaka huu na ya mwaka huu itakuwa na nguvu kuliko ya mwakani.

Ndiyo maana wananchi hawali fedha, badala yake wananunua bidhaa kwa kutumia fedha, hivyo basi hata ukiwa tajiri utakufa nazo, hapo ndipo inapoonekana umuhimu wa fedha kwa ajili ya kupata mahitaji muhimu, alisema.

Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Hajji Semboja alisema   wananchi watahitaji nguvu kubwa kwa ajili ya kununua bidhaa ambazo awali  zilikua zinapatikana kwa Sh 100 lakini sasa haiwezekani.

Alisema kupanda na kushuka   thamani ya shilingi ni suala la mpito na siyo la kudumu kwa sababu serikali katika kipindi hiki inaelekeza fedha nyingi kwenye miradi mikubwa ya maendeleo ambayo inahitaji kutoa kwa kupunguza matumizi ya kawaida.

Alisema katika uchumi hiyo ni hali ya kawaida lakini wananchi watajiuliza ikiwa itakwenda   mfululizo wa miezi mitatu ambako athari yake inaweza ikawa kubwa.

Profesa Semboja alisema uchumi wa Tanzania unategemea zaidi sekta ya kilimo, lakini pia bidhaa zinazozalishwa zina thamani ndogo kuliko mahitaji halisi.

Vilevile  baadhi ya bidhaa zikiwamo za vyakula  zinazalishwa viwandani hivyo   wananchi wanalazimika kununua bidhaa kutoka nje ambazo zina gharama kubwa kuliko zile zinazozalishwa nchini.

Alisema kwa hali hiyo  wananchi wengi hasa wenye kipato cha chini wataumia na hata wafanyakazi ambao wana kipato cha kawaida.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles