27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Takukuru Ilala kupambana na rushwa uchaguzi Serikali za Mitaa

Christina Gauluhanga, Dar es Salaam

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mkoa wa Ilala, imejipanga kuhakikisha rushwa haipenyi katika uchaguzi katika ngazi ya Serikali za Mtaa unaotajwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu na uchaguzi mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika mwakani.

Imesema katika kuzingatia umuhimu wa uchaguzi, Takukuru imejizatiti kufuatilia kwa makini hatua kwa hatua uchaguzi huo na watakaojihusisha nayo, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo Aprili 11, Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Ilala, Christopher Myava, amesema uchaguzi unapaswa kuendeshwa na kusimamiwa kwa uadilifu na umakini mkubwa.

Myava ambaye alikuwa akitoa ripoti ya utendaji kazi kwa kipindi cha robo mwaka, amesema Takukuru imedhamiria kuhakikisha vitendo vya rushwa katika uchaguzi huo vinakomeshwa ili kuzingatia sheria, kanuni na taratibu ili haki, usawa, uhuru na demokrasia viweze kustawi, kuendelezwa na kudumishwa.

“Rushwa katika uchaguzi ni hatari na inaweza kuleta madhara kwa taifa kwani viongozi wala rushwa au watoa rushwa hawataweza kusimamia nchi kwa misingi ya haki, usawa, uwazi, uwajibikaji na uzalendo,” amesema Myava.

Aidha, Kamanda huyo wa Takukuru amesema rushwa ikiota mizizi bila kuchukuliwa hatua za sheria, wahusika hata wananchi wapokea rushwa hawawezi kuhoji masuala mbalimbali kwa viongozi wao.

Myava amesema hadi sasa Takukuru katika kipindi hiki, wamefanikiwa kuwafikisha mahakamani vigogo 29 wakiwamo viongozi sita wa vyama vya siasa pamoja na watumishi wa sekta binafsi na za umma kwa tuhuma za rushwa.

Watuhumiwa hao walikamatwa katika kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu na miongoni mwao ni wanasiasa, mtumishi mmoja wa mahakama, taasisi ya kifedha, vyombo vya ulinzi, watumishi wa sekta ya elimu, watumishi wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), watumishi wa afya, wa sekta binafsi na wa mashirika ya umma.

“Watuhumiwa hawa walifikishwa mahakamani kujibu tuhuma zao za rushwa na kesi hizo zinaendelea,” amesema Myava.

Mbali na hayo, Myava amesema Takukuru inaendelea kufanya uchunguzi wa tuhuma mbalimbali kwa kufungua majalada 14 yanayohusu uhujumu uchumi, ukwepaji kodi, hongo, ubadhirifu wa mali za umma, rushwa ya ngono na uchunguzi wa miradi iliyotekelezwa chini ya viwango.

Amesema katika ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo, wanaangalia thamani halisi ya fedha za umma na kubaini uvujaji wa fedha hizo, ambapo wamebaini miradi sita kati ya nane iliyotekelezwa ina viashiria vya rushwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles