27.5 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

TAJIRI WA TAKUKURU ASOMEWA MASHTAKA 45

TUHUMA: Mhasibu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU),Godfrey Gugai (kulia) na George Makaranga (kushoto),wanaotuhumiwa kwa kukutwa na mali zisizoendana na kipato chao wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam jana. Picha na John Dande

Na KULWA MZEE-DAR ES SALAAM


ALIYEKUWA Mhasibu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Godfrey Gugai na wenzake watatu wamefikishwa mahakamani wakikabiliwa na mashtaka 43 yakiwamo ya kumiliki mali zisizo na maelezo, kughushi na kutakatisha fedha.

Washtakiwa hao walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana na kusomewa mashtaka   na Wakili wa Serikali Wankyo Simon mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Wankyo aliwataja washtakiwa kuwa ni Gugai, George Makaranga, Leonard Aloys na Yasini Katera.

Alidai katika shtaka la kwanza, mshtakiwa Gugai anadaiwa kati ya Januari 2005 na Desemba 2015 akiwa ofisa wa umma aliyeajiriwa na Takukuru, alikutwa akiwa anamiliki mali yenye thamani ya Sh bilioni 3.634 ambayo haiendani na kipato chake cha sasa na cha nyuma ambacho ni Sh milioni 852.183.

Alidai shtaka la pili mpaka la sita, Gugai anadaiwa kughushi mikataba ya mauziano ya nyumba akionyesha aliuza kwa watu mbalimbali wakiwamo washtakiwa wenzake hivyo walionunua ndiyo wamiliki halali wakati si kweli.

Anadaiwa kuonyesha kuwa Agosti, 2007 alimuuzia Zenna Mgallah ploti namba 225 block 6, iliyopo Mbweni JKT, Julai 2011 alionyesha ameuza nyumba namba 621,622 na 623 zilizopo block A Gomba Arumeru kwa Salehe Saa wakati si kweli.

Gugai anadaiwa Oktoba 20,2013 kwa kughushi alionyesha kuwa alimuuzia Arif Premji nyumba namba 64 iliyopo Ununio,  Desemba 20, 2014 alionyesha alimuuzia nyumba namba 737 block C Edith Mbatia iliyopo Mwarongo Tanga na shtaka la sita anadaiwa alidanganya kuonyesha alimuuzia Mbatia nyumba namba 1,2,3 block J iliyopo Mwarongo.

Wankyo alidai shtaka la saba linamkabili mshtakiwa wa kwanza na wa pili Makaranga ambako inadaiwa Novemba 20,2011 walighushi mkataba kuonyesha Gugai alimuuzia Makaranga nyumba namba 150 block 8 iliyopo Bunju akionyesha ndiye mmiliki wa nyumba hiyo.

Shtaka la 8 mpaka la 11 la kughushi pia linamkabili mshtakiwa wa kwanza na wa tatu Aloys ambako inadaiwa Novemba 19, 2009 Gugai alionyesha kamuuzia Aloys nyumba namba 275, 277, 296 na 297 zilizopo block 2  Nyamhongolo Mwanza.

Shtaka la tisa Gugai anadaiwa kughushi akionyesha kamuuzia Aloys nyumba namba 90 block 5 Bugarika Mwanza,  shtaka la 10 ni kumuuzia Aloys nyumba namba 713 block B Kiseke Mwanza na Oktoba 20, 2015 alionyesha kamuuzia nyumba nyingine namba 230 block B Nyegezi Mwanza.

“Mheshimiwa hakimu shtaka la 12 mpaka 20 linamkabili mshtakiwa wa kwanza Gugai akidaiwa kughushi akionyesha kamuuzia nyumba Manwal Masalakulangwa, Bunju, Bagamoyo na Buyuni Temeke.

“Mshtakiwa anadaiwa kughushi mkataba wa mauzo akionyesha kamuuzia nyumba Rose Abdallah nyumba mbili Dodoma, Mwongozo Temeke, Chidachi North na Itege Dodoma.

“Gugai anadaiwa kughushi akionyesha kamuuzia nyumba Patrick Magesa nyumba mbili zilizopo mkoani Tanga huku akionyesha mnunuzi huyo ndiye mmiliki, “alidai Wankyo.

Katika shtaka la 21 na 22 Gugai anadaiwa kughushi akionyesha kamuuzia nyumba mbili mshtakiwa Yasini Katera zilizopo Nyegezi Mwanza na kuonyesha ndiye mmiliki.

Kuanzia shtaka la 23 mpaka 43 washtakiwa wanashtakiwa  kutakatisha fedha ambako shtaka la 23 mpaka 27 Gugai anadaiwa kuficha umiliki wa mali huku akijua ni mazalia ya mali zisizo na maelezo ambalo ni kosa tangulizi la kutakatisha fedha.

Nyumba hizo ni zile alizodai kuuza kwa Zena, Salehe, Arif na Edith.

Shtaka la 28 linamkabili Gugai na Makaranga wakidaiwa kutakatisha fedha kwa kuficha umiliki wa nyumba aliyouza Gugai kwa Makaranga na shtaka la 29 mpaka 32 linawakabili Gugai na Aloys.

Gugai anadaiwa kutakatisha fedha kwa kuuza nyumba nne kwa Aloys huku akijua ni zao la mali zisizokuwa na maelezo ambalo ni kosa tangulizi la utakatishaji fedha.

Wakili wa Serikali, Max Ally akisaidia kusoma mashtaka, alidai shtaka la 33 mpaka la 41 linamkabili Gugai akidaiwa kutakatisha fedha kwa kumuuzia nyumba tatu Masalakulangwa, nyumba nne za Rose na nyumba mbili Patrick huku akijua ni zao la rushwa ambalo ni kosa tangulizi la kutakatisha fedha.

Mac alidai shtaka la 42 na 43 linamkabili mshtakiwa Gugai na Yasini ambako Gugai anadaiwa kumuuzia nyumba mbili Yasini huku akijua mazalia ya rushwa ambalo ni kosa tangulizi la kutakatisha fedha.

Baada ya kumaliza kusoma mashtaka, Wakili Wankyo alidai upelelezi haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa ambako ataieleza mahakama hatua ambayo upelelezi umefikia.

Kabla ya Hakimu Simba kuahirisha kesi, Wakili wa Utetezi, Alex Mgongolwa, aliwasilisha hoja akidai mashtaka ya kutakatisha fedha kuanzia namba 23 mpaka 43 ni batili yafutwe.

Mgolwa alidai mashtaka hayo hayakidhi vigezo vya kuwa mashtaka ya kutakatisha fedha kwa sababu maelezo ya mashtaka hayaelezi kosa hivyo yanakosa hadhi ya kuwapo mahakamani hapo.

Hoja hizo zilipingwa vikali na upande wa Jamhuri ambao walionyesha kwamba mashtaka ni sahihi yanapaswa kuendelea kuwapo mahakamani hivyo wakaomba hoja za utetezi zisikubaliwe kwa vile hazina msingi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles