33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Taifa Stars mbele kwa mbele

Na MOHAMED KASSARA

KIKOSI cha timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, leo kitashuka dimbani ugenini kutafuta ushindi dhidi ya Cape Verde katika mchezo wa kusaka tiketi ya kushiriki fainali za mataifa Afrika (Afcon) utakaochezwa Uwanja wa Taifa jijini Praia.

Taifa Stars itaingia katika mchezo huo, ikihitaji ushindi ili kufufua matumaini ya kufuzu fainali hizo ambazo kwa mara ya mwisho ilishiriki mwaka 1980, michuano iliyofanyika nchini Nigeria.

Mchezo huo utakuwa wa pili kwa kocha raia wa Nigeria, Emmanuel Amunike, aliyekabidhiwa jukumu la kukinoa kikosi hicho kwa mkataba wa miaka miwili, akichukua nafasi ya mzawa, Salumu Mayanga.

Amunike atakuwa akikiongoza kikosi hicho kwa mara ya pili, baada ya kuiongoza Taifa Stars kuvuna pointi moja ugenini dhidi ya Uganda.

Timu hizo zimekutana katika michezo mitatu ya mashindano yote, ambapo Taifa Stars ilishinda mmoja, imepoteza mmoja na kutoka sare mmoja.

Mara ya mwisho timu hizo zilipokutana, Taifa Stars ilikubali kipigo cha bao 1-0, ukiwa ni mchezo wa kutafuta kufuzu fainali za Kombe la Dunia uliochezwa Juni 7 mwaka 2008.

Katika mchezo huo, Taifa Stars itawakosa beki, Andrew Vincent ‘Dante’ na viungo Jonas Mkude na Frank Domayo, kutokana na majeraha, wakati  kiungo Salum Kihimbwa na mshambuliaji, Kelvin Sabato, watakosekana kutokana na sababu za kiufundi.

Baada ya kutema nyota hao, kocha huyo amewaongeza makipa wawili, Aaron Kalambo wa Tanzania Prisons na Benedicto Tinocco wa Mtibwa Sugar.

Msafara wa kikosi cha wachezaji 23, wakiwemo wachezaji tisa wanaocheza soka nje ya nchi ulitua juzi nchini humo ukiongozwa na nyota wa zamani wa Taifa Stars, Peter Tino.

Tino aliiongoza Taifa Stars kufuzu Afcon ya mwaka 1980.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Meneja wa Taifa Stars, Dany Msangi, alisema kikosi kitakachoivaa Cape Verde kipo timamu kimwili na kiakili.

“Tunashukuru tumefika salama, tulipata fursa ya kufanya mazoezi katika uwanja tutakaochezea, baadaye tutakuwa na kikao kidogo cha wachezaji na benchi la ufundi kuangalia mbinu za wapinzani wetu.

“Wachezaji wote wapo katika morali ya hali ya juu, kila mmoja anaonyesha utayari wa kuipigania nchi yake, pia tunatambua umuhimu wa mchezo huu, hivyo tumejiandaa vizuri kuhakikisha tunashinda ugenini kabla ya kwenda kumaliza kazi Dar es Salaam,” alisema Msangi.

Mchezo wa marudiano kati ya Taifa Stars na Cape Verde utafanyika Oktoba 16, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika michuano hiyo, Tanzania imepangwa Kundi L pamoja na timu za Uganda, Lesotho na Cape Verde.

Taifa Stars katika msimamo wa kundi hilo inashika nafasi ya tatu, nyuma ya vinara, Uganda wenye pointi nne, ikifuatiwa na Lesotho yenye pointi mbili sawa na Tanzania, huku Cape Verde ikiwa mkiani na pointi moja.

Stars ilizindua kampeni zake kwa kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Lesotho mchezo uliochezwa Juni 10 mwaka jana  Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kabla ya kulazimisha suluhu na Uganda katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Nelson Mandela, Kampala.

Cape Verde ilizindua harakati zake kwa kupoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Uganda katika mchezo wa kwanza uliochezwa jijini Praia, kabla ya kutoka sare ya bao 1-1 na Lesotho jijini Praia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles