33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Taifa letu, fahari yetu

Kikwete na SheinNa Waandishi wetu

RAIS Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein jana wamepokea Katiba inayopendekezwa mjini Dodoma.

Akizungumza katika sherehe  zilizofanyika Uwanja wa Jamhuri,Rais Kikwete aliwataka watu ambao hawakuridhika na mchakato wavute subira.

Sherehe hizo zimefanyika huku wajumbe wa kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wakiwa wamesusia vikao vya Bunge hilo tangu Aprili 16, mwaka huu.

Rais Kikwete aliyeanza kuhutubia saa moja jioni, alisema licha ya uzuri wa Katiba inayopendekezwa kuna mambo ambayo hayakupata nafasi hivyo akashauri wajumbe wasioridhika kuvuta subira.

“Kutokubalika kwa baadhi ya mambo haina maana kuwa hayakuwa ya msingi… mawazo yako mazuri, lakini siyo sasa. Wakati ukifika jambo hilo hilo ulilokuwa ukilidai utalipata. Kuna watu wanaotaka Serikali tatu, hao hao utaona wamebadilika,” alisema Rais Kikwete huku akishangiliwa na umati wa watu waliofurika katika uwanja huo.

Huku akikumbushia historia ya maisha yake, Rais Kikwete alisema aliwahi kufanya kazi Zanzibar na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Afro Shirazi (ASP), Thabit Kombo ambaye alimhusia kuhusu wakati.

“Mimi nilifanya kazi Zanzibar wakati ule wa kuunganisha TANU na ASP… mwaka 1977 nilikuwa bado kijana mbichi (kicheko)….sivyo mnavyofikiria.

“Kuna wakati tulikwenda Ikulu ya Chakechake kule Tibirizi. Kuna jambo tulikuwa tukizungumza na Thabit Kombo akasema, kuna jambo ninalotaka kukwambia kijana kuhusu wakati. Kama wakati haujafika, unalotaka liwe haliwi…kuna watu walitaka mambo yao yawe lakini wakati bado,” alisisitiza Rais Kikwete.

Alisema vita vya maneno na malumbano sasa viishe kwani Bunge Maalumu la Katiba na Tume ya Mabadiliko ya Katiba wamemaliza kazi yao.

Rais Kikwete alisema hatua iliyobaki ni kuwaachia wananchi ambao ndio wenye uamuzi wa mwisho kwa kuipigia kura Katiba inayopendekezwa.

“Kupatikana kwa Katiba inayopendekezwa nzuri ni wazi sasa uamuzi umebaki kwa wananchi, maana tunajua wasemaji wapo wengi. Tumieni busara za mbayuwayu kwani akili za kuambiwa changanya na zako.

“Yaliyopita si ndwele tugange yajayo, vita ya maneno na malumbano sasa yaishe, kama ingekuwa vita ningesema sasa tusitishe mapigano,” alisema Rais Kikwete.

Katiba ni halali

Rais Kikwete alisisitiza Katiba inayopendekezwa ni halali kwa sababu ilipitishwa kwa theluthi mbili pande zote za Muungano.

“Wajumbe wa Bara walikuwa 411 na wajumbe wa Zanzibar walikuwa 219, ili upate theluthi mbili ya Zanzibar ilikuwa ni kura 146. Hofu ilikuwa Zanzibar, lakini bahati nzuri mambo yakawa mazuri, kati ya kura 146 zikapatikana 148, Bara nako ndiyo usiseme. Kwahiyo Katiba hii ni halali kabisa,” alisema Rais Kikwete.

Hofu ya kura ya maoni

Akizungumza kukamilika kwa Katiba hiyo inayopendekezwa, alisema pamoja na matukio kadhaa, baadhi ya watu walikuwa wakishauri kazi hiyo ifanyike ili kupitisha Uchaguzi Mkuu ujao.

Alisema kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2013, kifungu cha 10, inatakiwa kura ya maoni kufanyika ndani ya siku 84 baada ya kukabidhiwa kwa Katiba inayopendekezwa.

Rais Kikwete alisema kumekuwa na maoni mbalimbali kutoka kwa wadau huku wengine wakitaka kuahirishwa kwa mchakato wa kura ya maoni ili kupitisha uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura.

Alisema  ili jambo hilo liweze kufanyika ni lazima Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ifanyiwe marekebisho katika Bunge la Jamhuri ya Muungano.

“Suala hili tumemuachia Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kuona kama kuna uwezekano katika Bunge lijalo sheria hii inaweza kubadilika, maana wengine wanasema tubadili baadhi ya mambo hayajakaa sawa.

“Tume ya Uchaguzi sasa iko katika mchakato wa uboreshaji wa daftari la kudumu nao….ndio wamepewa kazi ya kusimamia,sasa tusubiri tuone kama kuna mabadiliko wananchi watafahamishwa,” alisema.

Awali Rais Kikwete alieleza mlolongo wa matukio tangu alipotangaza dhamira ya kuandikwa Katiba mpya Desemba 31, 2011 huku akifichua jinsi makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) walivyopokea habari hiyo kwa shingo upande.

“Wapo waliopinga na wengine walionihoji jambo hilo umelitoa wapi wakati haikuwa ajenda ya Chama Cha Mapinduzi. Mimi niliwaambia ni maoni ya wananchi na ndiye mwakilishi wao mkuu, lakini nilipata wakati mgumu kuwaeleza wajumbe hao.

“Baadhi ya waliokuwa wakipinga niliwateua kwenye Bunge Maalumu la Katiba na wamekuwa msaada mkubwa,” alisema Rais Kikwete.

Alifafanua jinsi alivyovutana na vyama vya upinzani hasa vya CUF, Chadema na NCCR Mageuzi huku akifichua kwamba baadhi ya makada wa CCM hawakutaka akutane na vyama hivyo.

Alisema alipotangaza mchakato wa Katiba, ulipokewa kwa mtazamo tofauti.

Rais Kikwete alisema changamoto zilianza mapema tangu ilipotangazwa hatua ya ukusanyaji maoni Novemba 18, 2011  ambapo kuna kundi liligoma na kufikia hatua ya kususia Bunge.

“Baada ya kususia niliwakusanya na kuanza mazungumzo ya kutafuta suluhu na vyama vya CCM, CUF, NCCR-Mageuzi, Chadema na taasisi zisizokuwa za kiserikali na tukakubaliana Novemba na Januari kwa kuvitaka vyama kuleta mapendekezo ili kuchuja yanayofaa ili yawasilishwe bungeni,” alisema.

Rais Kikwete alisema Februari 2012 yalifanyika marekebisho ya Katiba na kuwezesha Aprili 6, 2012 kuteuliwa kwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba.

“Desemba 30, 2013 Tume iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Joseph Warioba ilikamilisha kazi yake na kukabidhi Rasimu ya pili kwangu na kwa Rais wa Zanzibar, Dk. Mohammed Shein pale Karimjee,” alisema.

Alisema  kuna marekebisho mbalimbali yalitakiwa kufanywa ambapo alitakiwa kuongeza wajumbe katika kundi maalumu kutoka 166 hadi 201 kazi aliyoimaliza Januari 2014.

Rais Kikwete alisema  pamoja na kufanya mambo yote kwa ajili ya kuhakikisha makundi yote ya wajumbe yanashiriki kuhakikisha Katiba mpya inapatikana, lakini alishangaa kusikia tena Aprili 16, mwaka huu Ukawa wametoka tena bungeni.

“Pamoja na wajumbe waliobaki kunitaka kuwaacha waliotoka,lakini nilifanya jitihada mbalimbali ikiwamo na taasisi mbalimbali kushiriki kuwasihi warudi bungeni bado walisusia, waliokuwa wamebaki wakanihakikishia lazima wataipata Katiba hata bila hao Ukawa,” alisema.

Alisema  Samuel Sitta alimuomba kumuongezea siku 45, lakini alitambua muda huo usingetosha akaamua kuwaongezea siku 60.

Chenge

Awali Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi ya Bunge Maalumu la Katiba, Andrew Chenge  alisema Katiba inayopendekezwa imezingatia Rasimu ya pili ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa asilimia 81.8, huku akisema mambo mapya yaliyoingizwa ni asilimia 18.2.

Habari hii imeandaliwa na Elias Msuya, Shabani Matutu na Agatha Charles (Dar) na Maregesi Paul (Dodoma).

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles