24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

TAASISI IMARA ZA UDHIBITI USHINDANI ZINAHITAJIKA

Na JUSTIN DAMIAN


KWA wale wenye kumbukumbu nzuri wakati simu za kiganjani zinaingia miaka ya 1990, wanaweza kuwa na historia nzuri ya kusimulia wakilinganisha na hali ilivyo kwa sasa.

Miaka hiyo ilikuwapo kampuni moja iliyokuwa inajulikana kama Mobitel. Hata simu watu walizokuwa wanatumia waliziita Mobitel, halafu zikawa ‘kimobitel’.

Kipindi hicho haikuwa rahisi kuweza kumiliki simu ya kiganjani kama ilivyo leo, ambapo mtu yeyote yule anaweza kumiliki simu. Kampuni ya Mobitel ilikuwa kampuni hodhi na peke yake na ndiyo ilikuwa ikiuza simu pamoja na kutoa huduma za mawasiliano. Kwa sababu hiyo, simu zilikuwa ghali, kwani iliamua kuuza bei inayotaka kwa soko lililokuwa linachipukia kwa kasi. Kununua simu ilikuwa ni gharama kubwa na waliokuwa nazo walihesabika kuwa wana ukwasi.

Hata baada ya kuinunua ulihitaji kuwa na fedha za kutosha kuendelea kuitumia. Lilikuwa ni jambo la kawaida kwamba unapopiga simu unatozwa na hata anayepokea anatozwa pia kwa kupokea simu. Muda wa maongezi uliuzwa kwa thamani ya Dola ya Kimarekani na kiwango cha chini ilikuwa ni Dola tano, sawa na Sh 2500, leo zipo vocha hata za Sh 200.

Wengi watakubaliana na mimi kuwa katika mazingira kama hayo isingekuwa rahisi kwa watu wengi kuweza kumiliki simu za mkononi kama ilivyo leo. Hata hivyo, wahenga wanasema siku hazigandi na mambo yamebadilika.

Sababu moja kubwa ambayo imeweza kufanya upatikanaji wa huduma za simu na nyingine nyingi kuwa rahisi ni kutokana  na ushindani. Hali ya ushindani umeleta makampuni mengine na kushusha bei za bidhaa na huduma zao ili kupata wateja ambao hufuata bei nafuu.

Pamoja na kuwa ushindani ni mzuri, usipodhibitiwa unaweza kuwa na madhara. Wiki iliyopita, Tume ya Ushindani (FCC) kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti ya REPOA walikuwa wenyeji wa Mkutano wa Tatu wa Mwaka unaohusiana na masuala ya ushindani  kwa nchi za SADC, uliofanyika jijini kwa wiki moja.

Mkutano huo uliweza kuzileta pamoja taasisi za udhibiti kutoka Zambia, Botswana, Afrika Kusini, Namibia, Tanzania, Kenya na Uganda. Washiriki walibadilishana mawazo na uzoefu juu ya namna  ya kuboresha ushindani na mazingira ya ushindani ili usiumize  wadau wa soko.

Akizungumza na gazeti hili, Dk. Donald Mmari, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa REPOA, anasema ushindani katika biashara na masoko ni muhimu sana. Anaeleza kuwa unapokuwapo  ushindani ambao ni mzuri unasaidia katika kuongeza ufanisi kwenye uzalishaji wa bidhaa, lakini pia unasaidia kulinda walaji kwa kuwafanya wapate huduma nzuri na kwa bei nafuu kwa kuwapo kwa ushindani.

“Ushindani unaimarisha ubunifu, ambapo makampuni hujaribu kubuni bidhaa na huduma nzuri ambazo pia zinakuwa za bei nafuu ili kuwavutia wateja,” anaeleza.

Dk. Mmari anasema, kwa ujumla wake, ushindani ni muhimu kwa sababu husaidia uchumi kukua kwa haraka.

“Hata hivyo, ushindani  unahitaji udhibiti na ndiyo maana tunasema taasisi hizi za udhibiti kama Tume ya Ushindani Tanzania (FCC) ni lazima ziwe na nguvu, uzoefu, watendaji wa kutosha pamoja na rasilimali fedha kwa ajili ya kufanya utafiti wa kuelewa vizuri sheria mbalimbali zinazohusiana na masuala ya ushindani,” anasema.

Anasema mkutano huo ni muhimu, kwa kuwa huwaleta wataalamu ambao hutoa uzoefu wao juu ya nchi nyingine na hasa mataifa makubwa, kwa kuwa mataifa hayo yana makampuni makubwa yenye uelewa mkubwa wa sheria za masuala ya ushindani.

“Sisi kama taasisi ya utafiti, tuliona ni jambo jema kushirikiana na taasisi nyingine za utafiti kutoka ndani ya Afrika pamoja na mamlaka hizi za udhibiti ili kuwapo na uelewa mpana zaidi. Kwa hiyo kumekuwa na watafiti waliofanya utafiti na kuwasilisha mada zao pamoja na matokeo ya tafiti zao,” alieleza.

Kwa upande wake, Profesa Eleanor Fox kutoka nchini Marekani, ambaye ni mtaalamu nguli duniani wa masula ya Sera na Sheria za Ushindani,  alisema pamoja na umuhimu wa ushindani kwa maendeleo ya nchi zinazoendelea kama Tanzania, bado taasisi za udhibiti wa ushindani zinakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo zinazifanya kushindwa kutimiza wajibu wake ipasavyo.

“Rasilimali fedha pamoja na rasilimali watu ni kati ya changamoto zinazozikabili taasisi za udhibiti kwa nchi zinazoendelea. Kama serikali zitaweza kutambua umuhimu wa hizi sera za ushindani, pengine wataweza kutenga rasilimali zaidi. Uwekezaji kwenye eneo hili ni muhimu sana na wenye faida kubwa kwa vile utasaidia wananchi  kuweza kupata  huduma bora na kwa gharama nafuu,” anabainisha.

Anasema rasilimali kwa ajili ya kufanya utafiti zinahitajika. “Utafiti ni muhimu kwa kuwa utawezesha namna moja ya kutengeneza ushindani wa haki, hasa katika nchi zinazoendelea na kuwawezesha wajasiriamali wapya kuingia sokoni. Ili kufanikisha hili utafiti kwenye eneo la Sheria za ushindani pamoja na sera unahitajika, ili kuweza kudhibiti nguvu za makampuni makubwa na kuwawezesha watu wapya pamoja na wajasiriamali waweze kuingia sokoni na kuweza kushindal.”

Alielezea changamoto nyingine kuwa ipo kwenye mfumo wa soko huria. “Sera hii inapotumiwa na mataifa makubwa bila kuangalia hali halisi katika mataifa madogo, inaweza kuumiza mataifa haya madogo. Kinachotakiwa kufanyika ni mataifa madogo kushirikiana na kuhakikisha kuwa wanapaza sauti na kusema namna ambavyo mfumo wa soko unapaswa kuwa ili usiwaumize watu wake,” alifafanua.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles