23.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

‘TAALUMA, NIDHAMU HAVINA BUDI KWENDA SAMBAMBA’

Na CHRISTINA GAULUHANGA-DAR ES SALAAM


MMOMONYOKO wa maadili unaendelea kuikumba jamii kwa kasi ya ajabu na kuzorotesha ustawi wa maendeleo ya taifa.

Hii inatokana na ukweli kwamba maendeleo ya sayansi na teknolojia kwa kiasi kikubwa yanachangia vijana wengi kuiga mambo mengi kutoka kwenye mitandao ya kijamii kiasi cha kuchanganyikiwa katika maisha.

Watoto ni kundi linalohitaji kuangaliwa kwa namna ya pekee, vinginevyo matumaini yao katika siku za usoni yanaweza kusambaratika na hatimaye kuwa katika hatari kubwa.

Kutokana na hali hiyo shule zinategemewa kuwajenga watoto kimaadili hasa katika kudhibiti nidhamu mbaya na kuhakikisha watoto wanatii sheria, kanuni na taratibu nyingine.

Hivi ndivyo inavyofanya Shule ya Awali na Msingi ya Heritage iliyoko Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam ambayo inahakikisha kuwa maadili na taaluma vinaenda sambamba.

Shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 2004, imeshuhudia ukuaji wenye tija na upanuzi wa wigo wa utoaji wa huduma ya elimu bora.

Akizungumza wakati wa mahafali ya 10 ya shule hiyo yaliyofanyika wiki iliyopita shuleni hapo, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Magige Magabe, anasema shule hiyo ilianza ikiwa na wanafunzi 20 lakini sasa ina wanafunzi 880.

Anasema elimu wanayotoa inalenga kuwasaidia wanafunzi kutambua na kuendeleza vipaji na vipawa walivyonavyo katika viwango vya kimataifa.

Mwalimu huyo anasema wamekuwa wakiwaandaa vyema wanafunzi na kuwapatia uwezo mzuri wa kuendelea na elimu ya sekondari.

“Shule yetu imefanikiwa kutayarisha wanafunzi wawajibikaji na wenye nidhamu ya hali ya juu kwa ajili ya elimu ya sekondari na hatimaye elimu ya juu kwa ajili ya utumishi na huduma bora kwa taifa,” anasema Mwalimu Magabe.

Anasema tangu kuanzishwa kwa shule hiyo wanafunzi wote wa darasa la nne na la saba wamekuwa wakifaulu kwa asilimia 100 katika mtihani wa taifa.

Kwa mujibu wa mwalimu huyo kati ya mwaka 2008 na 2016, wahitimu 453 wa darasa la saba wote walifaulu kwa asilimia 100.

Anasema kwa upande wa Manispaa ya Ilala, nafasi ya shule kati ya mwaka 2008 na 2016 imekuwa ni kati ya tatu na ya saba.

“Matokeo haya ni ishara kuwa Heritage ni taasisi imara inayokua na yenye mustakabali mzuri. Tunajivunia sifa njema ya kuwa kitovu cha maadili na makuzi sahihi,” anasema.

Mwalimu huyo anasema pia wameanza mchakato wa kufundisha kwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Teknohama) ili kuwaandaa vyema wanafunzi na kuwajengea uwezo wa kuendelea na elimu ya sekondari.

Mmoja wa wahitimu, Bhuyegi Nyaimaga, anaishauri serikali kuangalia upya suala la vitabu vya kiada kwa sababu kuwapo kwa machapisho mengi kunachangia ugumu katika kujifunza.

“Kuwapo kwa machapisho mengi ya vitabu vya kiada vyenye dhana kinzani katika baadhi ya mada kunasababisha kuwe na ugumu katika kujifunza, tunaomba suala hili liangaliwe kwa makini,” anasema Nyaimaga.

Mwanafunzi huyo anasema wamejengewa ujasiri wa kutosha na kuondolewa hofu ya kujibu mitihani ya ndani na nje ya shule.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mahafali hayo, anasema shule zinatakiwa kuwa na mipango mikakati ya maendeleo na kutoa elimu inayowajenga watoto badala ya kutumia ujanja ujanja katika mitihani ya kitaifa.

“Shule zinatakiwa ziwafundishe wanafunzi kujitegemea. Zitoe elimu itakayojenga motto kimaadili ili kukabiliana na changamoto ya kuporomoka kwa maadili katika jamii ya Watanzania,” anasema Mjema.

Katika mahafali hayo wanafunzi 82 walihitimu darasa lasaba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles