24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

SUMUKUVU TISHIO BIASHARA NAFAKA AFRIKA MASHARIKI

Na JUSTIN DAMIAN

MAZAO ya nafaka kutoka  nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), yanaendelea kushindwa kushindana katika masoko ya kimataida kutokana na sumu hatari inayojulikana kitaalamu kama Sumukuvu (Aflatoxin)

Sumukuvu, ni aina ya sumu inayozalishwa na fangasi au kuvu aina ya Aspergillus Flavus. Fangasi hawa hukaa kwenye udongo na masalia yaliyooza shambani. Mazao mengi huathirika na sumukuvu wakati bado yakiwa shambani.

Baadhi ya mazao ambayo hushambuliwa na sumu hii ni pamoja na mahindi, karanga, kunde na mengineyo. Sumu kuvu haiwezi kuonekana kwa macho, haina harufu, haina kionjo na wala haina rangi.

Kwa mujibu wa Fahari Marwa ambaye ni Mchumi anayeshughulikia masuala ya kilimo kutoka Jumuia Afrika Mashariki, sumukuvu ina madhara makubwa kwa afya ya binadamu  na wanyama jambo ambalo limepelekea udhibiti mkali wa mazao yanayoingia haswa nchi zinazoendelea.

Anasema nchi wanachama wa EAC zimekuwa zikishindwa kutumia vizuri masoko ya nje na haswa nchi zilizoendelea kutokana na mazao yake kuwa na kiasi kikubwa cha sumukuvu.

“Kwa mfano, kwenye nchi wanachama wa Jumuiya ya Ulaya (EU), kuna viwango maalum ambavyo vimewekwa na ambavyo hufuatwa  kwa ukamilifu ili kupunguza matumizi ya nafaka zenye sumu hii hatari. Kuweza kufikia viwango hivyo, bado ni changamoto kubwa kwa nchi za Kiafrika ikiwamo nchi wanachama wa EAC,” anasema Marwa

Mchumi huyo anasema, mazao ambayo yameathiriwa na sumukuvu hupata bei ndogo yawapo sokoni au wakati mwingine kuharibiwa kabisa kutegemeana na kiwango cha sumu kilichoonekana.

Marwa anafafanua kuwa, athari za sumukuvu zimekuwa na changamoto kubwa kwenye kilimo, afya pamoja na biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki.

“Suala la sumukuvu ni moja kati ya changamoto kubwa ambayo imechangia kurudisha nyuma ari ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi,” anaongeza

Kutokana na ukubwa wa tatizo la sumukuvu, Secretariati ya EAC imekuwa ikifanya jitihada mbali mbali za kukabiliana nalo. Muongozo wa nchi wanachama kushirikiana kwenye tatizo hili unatolewa kwenye kifungu cha 105 cha Kuanzishwa kwa Jumuiya hiyo.

Wiki iliyopita, wafanya maamuzi kutoka nchi wanachama walikutana jijini Dar es Salaam ambapo walipewa semina ya wiki moja na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo katika Eneo la Kitropiki (IITA) ili kuelewa ukubwa wa tatizo na madhara yake.

Dk George Mahuku kutoka IITA aliwaambia waandishi wa habari kuwa, karibu asilimia 25 ya vyakula ulimwenguni vina maambukizi ya sumu kuvu na kuongeza kuwa takribani watu bilioni 2.5 wako katika hatari ya kudhurika

Anasema ukiachana na madhara ya kiuchumi, sumukuvu inamadhara makubwa ya kiaafya ikiwamo Saratani, hasa ya ini, kushusha kinga ya mwili, kudumaa hasa kwa watoto, sumu kwenye figo na vifo kwa binadamu na wanyama ikiwa viwango vya sumu kuvu ni vikubwa.

“Baadhi ya sumu kuvu hutoka kwa mama kwenda kwa mtoto akiwa bado tumboni. Kutokana na madhara ya afya yanayosababishwa na sumu kuvu kwa binadamu na wanyama sumu kuvu haziruhusiwi kuwepo katika mazao yaliyokusudiwa kwa biashara na kama zikigunduliwa katika mazao ya kilimo hayatauzika na badala yake yatateketezwa. Kwa kiwango kikubwa sumu kuvu huathiri biashara, faida na afya za wazalishaji,” anaeleza

Anasema taasisi ya IITA imefanikiwa kutengeneza dawa inayojulikana kama Aflasafe ambayo ni fangasi wasio na madhara ambao huwekwa mashambani kwa ajili ya kupambana na sumukuvu.

“Mradi wa kuzuia sumu kuvu kwenye mazao ni mradi wa njia ya kibailojia yaani tunatumia bakteria wasio na madhara kumzuia bakteria mwingine mwenye madhara,” anaelezea Dk Mahuku

Anasema kwa kawaida kwenye udongo ndiyo mahali wanapoishi fangasi na humo wapo wanaotengeneza sumu na wasiotengeneza sumu lakini kwa uwiano fangasi wanaotengeneza sumu ni wengi kuliko wasiotengeneza sumu.

“Fangasi hao wakiwa kwenye udongo wanakuwa na hali  ya vumbi vumbi hivyo wanakuwa wepesi wanaoweza kupeperushwa kwenye hewa na upepo, wadudu, wanyama au ndege.

“Wakipeperushwa wanaweza kufika kwenye maua, kwa hiyo wakati maua na poleni inaingia kwenye matunda ili yafungwe inaweza kuingia na hao fangasi,” anasema.

Zaidi anafafanua kuwa,  mazao yanaendelea kukua vizuri hadi yanakauka tayari kwa kuvunwa lakini kumbe ndani yake kuna fangasi wanazaliana na yak- ipimwa yanapovunwa yanakutwa na sumu kuvu.

Mtaalamu huyo wa mimea anasema, dawa hiyo tayari imeshafanyiwa majaribio ya kina na kwamba imeonyesha mafanikio makubwa.

“Baada ya kufanyiwa majaribio, Aflasafe imeonekana kuwa na ufanisi mkubwa ambao unafikia zaidi ya asilimia 85. Kwa sasa tupo katika hatua za kuisajili ili iweze kuzalishwa kwa wingi na kisha kuwafikia wakulima wengi,” anaeleza

Anasema, kuwa baada ya dawa hiyo kusajiliwa na kisha kuaanza kusambazwa kwa wingi, wakulima wataweza kuzalisha nafaka ambazo ni salama kwa afya pamoja na kuweza kuuza katika nchi ambazo walishindwa kuuza mwanzoni kutokana na mazao yao kuwa na kiwango kikubwa cha sumu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles