SUMU KATIKA DAMU HUUA WAGONJWA-DK. MPOKI

0
562


VERONICA ROMWALD Na

FRANK KAGUMISA (SAUT)-DAR ES SALAAM

Watu  milioni 30 kila mwaka huugua ugonjwa wa sepsisi duniani, ambao hutokana na uwepo wa bakteria hatari kwenye mwili ambao husababisha uzalishaji wa kemikali hatari.

Kemikali hizo ndizo ambazo husababisha mtu kuumwa mno na wakati mwingine kufikia kupata ‘mshituko’ na hatimaye kifo.

Hayo yalielezwa Dar es Salaam jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii. Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Mpoki Ulisubisya alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Sepsisi Duniani yanayofanyika Septemba 13, kila mwaka.

“Kwa kipindi kirefu taasisi zetu zimekuwa zikitibu magonjwa mbalimbali kulingana na jinsi ulivyo, waligundua kuna nyanja moja isipoangaliwa kwa umakini matokeo ya tiba hayatakuwa mazuri.

“Wataalamu walieleza, kwa sababu ya kutokuangalia kwa makini sumu inayopatikana katika damu baada ya maambukizi mbalimbali wagonjwa wengi wanapoteza maisha kwa sababu ya yale madhara ya sumu hizo,” alisema

Alisema tafiti zilizofanyika nchini zinaonesha takriban asilimia 31 ya watoto wachanga wanaozaliwa huwa na ugonjwa huo.

“Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaeleza kati ya watu milioni 30 wanaougua kila mwaka, milioni sita hufariki dunia.

“Hapa nchini asilimia 32 ya watoto wachanga hufariki kwa ugonjwa huu na asilimia nane ya wajawazito na wanawake waliojifungua hufariki dunia kwa ugonjwa huu pia,” alisema.

Alisema hata hivyo jamii haina uwelewa wa kutosha juu ya ugonjwa huo ambao huweza kusababishwa na maambukizi kwenye mapafu, tumbo, figo na damu,” alibainisha.

Alisema wagonjwa wanaotibiwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) na wanaotumia dawa za saratani nao huwa kwenye uwezekano wa kupata ugonjwa huu.

Alisema dalili mojawapo za ugonjwa huo ni mtu kuhisi joto kali la mwili, mapigo ya moyo kwenda kasi au taratibu na kuhema haraka haraka.

Alisema kutokana na athari yake huweza kusababisha figo kushindwa kufanya kazi na ikiwa hatua hazitachukuliwa mgonjwa hupoteza fahamu na baadae moyo kushindwa kufanya kazi sawa sawa.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here