24.5 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Sugu ataka viongozi wapimwe akili

      FREDY AZZAH-DODOMA

MBUNGE wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi  (Chadema), maarufu kwa jina la Sugu, ametaka viongozi wote nchini kuanzia ngazi ya kijiji, wapimwe akili.

Pia, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche (Chadema), amesema mawaziri wanaosema umasikini ni uzalendo, wanaishi kwenye nyumba nzuri na kutembelea mashangingi ya Serikali.

Sugu na Heche, walisema hayo   Dodoma jana wakati wakichangia mapendekezo ya mpango wa maendeleo wa taifa na mwongozo wa maandalizi ya mpango na bajeti ya mwaka 2019/20.

Jana, baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu, mchangiaji wa kwanza alikuwa ni Sugu ambaye mchango wake ulimfanya Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama, kusimama mara kadhaa kutaka Sugu afute baadhi ya kauli zake.

Hoja ya kwanza ya Sugu baada ya kusimama, alisema katika Bunge la 10, Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde (CCM), alikuwa akizungumzia suala la wabunge kupimwa afya ya akili.

“Wakati ule nilikuwa simwelewi, lakini sasa hivi nakubaliana naye kabisa, nataka viongozi wote kuanzia ngazi ya chini mpaka ya juu tupimwe akili kwa sababu siku hizi baadhi ya wakuu wa wilaya na mikoa wanaongea mambo yasiyoeleweka,” alisema Sugu.

Kauli hiyo ilimfanya Mhagama asimame na kuomba kuhusu utaratibu.

Alisema Bunge la 10 lilikufa na mambo yake yote na kwamba kitendo cha Sugu kulitolea mfano siyo sahihi kwa kuwa kanuni za Bunge zinazuia mbunge kutoa kauli za kuudhi bungeni.

Alipoendelea kuchangia, Sugu pia alikemea tabia ya polisi kufanya mauaji kwa raia na uchunguzi wa masuala hayo kupuuzwa.

Kwa mujibu wa Sugu, jimboni kwake zaidi ya watu watatu wameuawa na polisi na mmoja ndugu zake wameacha mwili wa marehemu hadi leo hawajauzika wakitaka uchunguzi huru.

Kauli hiyo ilimfanya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, asimame na kusema Sugu anatoa tuhuma nzito kwa polisi ambazo hawezi kuzithibitisha na kumtaka aache kutoa tuhuma hizo.

“Watu wanaanza kushangaa, wanatukana polisi wakati polisi wangu wako huku ndani, naomba mchangiaji badala ya kujikita kusema polisi wanaua, nikimwambia alete taarifa sijui atafanyaje. Naomba asichafue polisi, asitumie vibaya uhuru wa kutoa maoni,” alisema Kangi.

Akijibu hoja hiyo, Sugu alisema: “Wewe mwenyewe Kangi ni mmoja wa waliopata sintofahamu ya awamu ya tano, ulipigwa kesi ya rushwa sijui iliishia wapi!”

Kwa upande wake, Heche alisema licha ya Serikali kusema inakusanya mapato mengi ikilinganishwa na awamu zilizopita, tangu 2015 hakuna ajira zilizotolewa.

“Mpango wewe unayependa uzalendo, mnatuaminisha uzalendo ni umasikini, mbona unatumia magari ya VX ya umma, mnakaa kwenye nyumba nzuri. Acheni kujinasibu kwa walalahoi.

“Tuambieni tangu muingie madarakani mlikuta walalahoi wangapi na mmepunguza wangapi.

“Mnatenga Sh trilioni 11.8 za maendeleo, halafu mnakuja kutoa Sh trilioni sita, hii maana yake asilimia 45 ya fedha za maendeleo hazijaenda, asilimia 45 ya miradi ya maendeleo haijatekelezwa, lakini Serikali tukufu inayokusanya kuliko zote ipo tu.

“Kabla ya mwaka 2015, gunia la mahindi liliuzwa kwa Sh 100,000, lakini sasa hivi gunia moja linauzwa kwa bei ambayo mkulima hapati fedha ya kununulia mbolea.

“Jana wanunuzi wa korosho wamesema hawanunui tena korosho, sasa naomba Mpango ukija hapa, useme Serikali itanunua korosho zote zilizo kwenye maghala kwa Sh 3,000 bila kupungua.

“Kwa sasa haki za binadamu zinatetereka, mnakuja hapa mnasema polisi gani wanauwa watu, mimi mdogo wangu aliuawa kituo cha polisi.

“ Zitto (Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe), juzi kasema polisi wameua halafu anaitwa kutishwa,” alisema Heche.

Mbunge wa Chambani, Yusuph Salum Hussein (CUF), alisema kwa hali ilivyo sasa, wa kulaumiwa ni Bunge ambalo limeshindwa kutimiza wajibu wake wa kuisimamia Serikali.

“Katiba inasema tukishapitisha bajeti, tusimamie itekelezwe, Serikali inafanya itakavyo kwa sababu sisi wasimamiaji wa Serikali hatufanyi kazi yetu,” alisema.

Mbunge wa Viti Maalumu, Munde Tambwe (CCM), alisema wabunge wa upinzani wanazungumzia watu kutekwa huku wakisahau kuwa suala la uhalifu ni janga la dunia.

“Suala la usalama ni la dunia, kwa siku moja Marekani wanatekwa zaidi ya watu 200, tusiseme tu ni hapa kwetu, hili ni janga la dunia, naomba tu Serikali iongeze fedha kwenye vyombo vya usalama ili kudhibiti janga hili la dunia.

“Wapinzani wanasema tume ya uchaguzi ibadilike, najiuliza, wao hapa wapo zaidi ya 100, hivi waliingiaje bungeni?”

Kuhusu suala la Katiba, alisema hakuna wananchi wanaotaka Katiba bali wanaoitaka wanataka rais ashindwe kutekeleza majukumu yake ili badaye waanze kumlaumu.

Mbunge wa Makambako, Deo Sanga (CCM), alipendekeza baada ya Bunge kumalizika, Spika wa Bunge, Job Ndugai aandaye sherehe ndogo ya kuipongeza Serikali kwa kazi nzuri inayoifanya.

Alisema jimboni kwake wananchi wana shida ya maji, barabara, pembejeo na kwamba hawahitaji Katiba mpya.

Pamoja na hayo, alitaka Rais Dk. John Magufuli, awe rais wa maisha kutokana na kazi nzuri anayoifanya.

Mbunge wa Sumve, Richard Ndasa (CCM), alipongeza juhudi za kufufua Shirika la Ndege Tanzania  (ATCL) huku akishauri Serikali isomeshe marubani wengi zaidi kwa kuwa hadi sasa kuna marubani 33 kati ya marubani 70 wanaohitajika.

Pia alishauri Serikali kujenga kiwanda cha nguo kanda ya ziwa   kuongeza thamani ya pamba inayolimwa na wakulima.

Mbunge wa Momba, David Silinde (Chadema), alisema kwenye hotuba ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Phillip Mpango, amesema kutofikiwa kwa malengo ya ajira kulisababisha bajeti ya 2017 kutofikiwa.

Kutokana na hali hiyo, alisema alitarajia kuona mpango wa sasa ukiainisha namna ya kutoka katika hali hiyo.

“Rwanda kabla ya waziri kuteuliwa, anasema atafanya kitu gani na kwa muda gani na akishindwa huondoka mwenyewe.

“Tukipima mawaziri leo hapa, tutajua nani anapiga porojo nani wa mwisho kwenye kazi kwa sababu hapa wanalinda ajira kwa kusifia tu,” alisema.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles