31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Stars safi, Algeria pigo

KUBWANA ABDUCADO EMMANUEL, DAR ES SALAAM

WAKATI timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, ikiwa inaendelea vema na kambi yake nchini Afrika Kusini, wapinzani wao Algeria ‘The Desert Foxes’ wamepata pigo baada ya kuumia kwa staa wake, Sofiane Feghouli.

Algeria inawasili nchini kesho kucheza na Stars kwenye mchezo wa raundi ya pili wa kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2018 nchini Urusi, utakaofanyika Uwanja wa Taifa, Jumamosi hii, huku wa marudiano ukifanyika Jumanne ijayo jijini Algiers, Algeria.

Mtandao wa Chama cha Soka Algeria (FAF), umeripoti kuwa kiungo mshambuliaji huyo atakosekana kwenye mechi hiyo baada ya kupata majeraha ambayo bado hayajawekwa wazi.

Feghouli amekuwa chachu kubwa ya mafanikio ya Algeria tokea aanze kukichezea kikosi hicho mwaka 2011, akishirikiana na mastaa wengine Ryad Mahrez (Leicester City), Yacine Brahimi (FC Porto).

Moja ya rekodi alizowahi kuweka ni kuifungia timu hiyo bao la kwanza kwenye michuano ya Kombe la Dunia mwaka jana, baada ya miaka 28 kupita wakati Djamel Zidane, alipofunga kwa mara ya mwisho mwaka 1986.

Mbali na pigo hilo, Algeria wananyemelewa na pigo jingine la Kocha Mkuu wao, Christian Gourcuff raia wa Ufaransa, kutangaza uamuzi wa kujiuzulu mara baada ya mechi mbili za Stars kumalizika, kutokana na shinikizo analopata kutoka kwa vyombo vya habari vya nchini humo.

Stars inayoshika nafasi ya 135 duniani, huku Algeria ikikamata ya 26, ipo kamili kuelekea mchezo huo na jana jioni ilitarajiwa kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya timu ya Taifa ya vijana ya Afrika Kusini chini ya miaka 23.

Akizungumzia kambi ya nchini Afrika Kusini, Kocha Mkuu wa Stars, Charles Mkwasa, amesema kuwa mpaka sasa wachezaji wake wote wapo katika hali nzuri na hakuna majeruhi na kila mmoja yupo tayari kwa mchezo huo.

“Wachezaji wapo vizuri kiafya, kifikra na morali ni ya hali ya juu, wamekuwa wakifanya mazoezi kwa nguvu na kuonyesha umakini mkubwa,” alisema.

Mkwasa amewaomba Watanzania na wadau wote wa soka nchini, kujitokeza kwa wingi kuwapa sapoti ya kuwashangilia vijana katika mchezo huo kwani kutawafanya wachezaji kujisikia wapo nyumbani na kucheza kwa nguvu zaidi.

Mshindi wa jumla wa mchezo huo atafuzu kwa raundi ya mwisho ya michuano hiyo ya hatua ya makundi, itakayoshirikisha timu 20 bora katika makundi matano na bingwa wa kila kundi atafuzu kwa fainali hizo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles