30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Staili mpya mawaziri kukwepa kutumbuliwa

Na MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

ULE msemo maarufu kwamba; sumu haionjwi kwa ulimi ndio ambao pengine unaonekana kuakisi kasi ya utendaji wa mawaziri wa Rais Dk. John Magufuli ambao sasa wanaonekana kubuni staili ya mpya ya kutatua kero mbalimbali wakiwa wamekusanyana kundi.

Katika kile ambacho kinaweza kujenga taswira kwamba mawaziri wa Rais Magufuli hawataki kukutwa na yale yaliyowakuta wenzao ambao waliondolewa mara moja baada ya utendaji wao kunyooshewa vidole, hivi sasa wamekuwa wakizunguka huko na huko  wakati mwingine wakiwa kundi  la mawaziri kati ya wawili hadi 13 katika mkutano mmoja kuhakikisha wanatatua kero mbalimbali zinazowakabili wananchi, wawekezaji na nyinginezo.

Rais Magufuli ambaye tangu aingie madarakani 2015 amejipambanua kama mtu asiye na mzaha kwa mawaziri wake na watendaji wanaokwenda kinyume.

Tangu alipounda baraza lake la kwanza la Mawaziri Desemba 2015 likiwa na mawaziri 19 katika wizara 18 wakati huo, tayari ameowaondoa wengi, na kuwahamisha baadhi  kutokana na sababu mbalimbali huku sita tu akiwa hajawagusa.

Mawaziri hao ambao hajawagusa ni  William Lukuvi (Ardhi na Maendeleo ya Makazi), Dk

Hussein Mwinyi (Ulinzi), Ummy Mwalimu (Afya), Profesa Joyce

Ndalichako (Elimu), Dk Philip Mpango (Fedha na Mipango), na Jenista Mhagama (Sera, Uratibu na Bunge).

Tukio la karibuni na ambalo baadhi wanaona linaakisi kasi na pengine staili ya sasa ya mawaziri hao kutembea na kutokea kwenye mikutano ya kutatua kero wakiwa kundi ni uamuzi wa Rais Magufuli kumwondoa aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara Joseph Kakunda na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Charles Kichere kwa kushindwa kutatua kero za wafanyabiashara.

Kakunda na Kichere  waliondolewa baada ya wafanyabiashara kumshitaki kwa Rais Magufuli  kwa kushindwa kutatua kero zao katika mkutano uliofanyika Ikulu Dar es salaam Juni, mwaka huu.

Nafasi ya Kakunda ilichukuliwa na aliyekuwa naibu Waziri wa Kilimo, Innocent Bashungwa na ile ya Kichere TRA ilichukuliwa na Edwin Mhede. 

Wafanyabishara hao waliinyooshea kidole TRA na Wizara ya Viwanda wakidai haiwatendei haki, na miongoni mwa kero zilizotajwa na wafanyabiashara hao ni utitiri wa kodi, vibali vya kuingiza bidhaa kutoka nje ya nchi, urasimu katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na madai ya watendaji wa wizara ya Viwanda na Biashara kujisifu kuvifunga viwanda kutokana na dosari mbalimbali na madai ya kodi na ushuru.

Pengine kutokana kumbukumbu hiyo, katika mikutano miwili tofauti iliyofanyika Dar, es Salaam Morogoro na Kibaha mkoani Pwani ndani ya wiki hii ya mashauriano kati ya Serikali, wafanyabiashara na wawekezaji, mawaziri kati ya tisa na 13 walikusanyana kusikiliza kero na kuangalia namna ya kuzitatua.

Watu wenye kumbukumbu zao wanasema idadi hiyo ya mawaziri kuonekana katika mkutano mmoja kwa ajili ya kutatua kero, haijawahi kutokea katika kipindi kirefu.

Katika mkutano uliofanyika Dar es Salam uliwakutanisha mawaziri 13 na wafanyabiashara walioelekeza kero zile zile zilizowahi kulalamikiwa Ikulu.

Wafanyabiashara hao walinyooshea utaratibu mbovu wa kuingiza na kuchukua mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam, tozo nyingi zinazofanywa na Shrika la Wakala wa Meli (Tasac).

Kero nyingine ni mwenendo mbovu wa biashara ya ndani na wateja wan chi jirani hasa katika Soko la Kariakoo, tozo nyingi, ucheleweshaji wa vibali, ukosefu wa mfumo bora wa kulinda viwanda vya ndani na nyingine. 

Timu kama hiyo ya mawaziri ilikutana na wafanyabiashara Desemba 4, mkoani Morogoro kwa ajili ya kusikiliza na kutatua kero kama hizo.

Katikati ya wiki hii mawaziri watatu na  manaibu mawaziri tisa walikutana katika mkutano wa mashauriano wa siku moja uliofanyika Kibaha mkoani Pwani ambao ulihudhuriwa na mawaziri karibu wote ni wa wizara zile zile zinazoonekana kuzunguka pamoja.

Mawaziri hao ni  Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angellah Kairuki, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William  Lukuvi , Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mussa Sima, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,Constantine Kanyasu ,Naibu  Waziri wa Mambo wa Ndani ya Nchi,Hamad Masauni.

Wengine ni Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Ashatu Kijaji, Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Antony Mavunde  (Kazi, Vijana na Ajira), Naibu Waziri Ofisi ya Rais  Tamisemi, Josephat Kandege.

Katika mkutano huo wawekezaji na wafanyabiashara walipata nafasi kufikisha malalamiko yao ambayo ni kikwazo katika shughuli zao.

Pamoja na mambo mengine ulizungumzia changamoto za ardhi ambapo Lukuvi alitoa wito kwa wakuu wa mikoa kuhakikisha  wanawalinda wamiliki wa ardhi ambao wapo kisheria.

Mkutano huo uliofanyika mjini Kibaha, uliongozwa na Waziri  Kairuki.

Waziri Lukuvi alibainisha kuwa  Mkoa wa Pwani unaongoza kwa uvamizi ambapo Wilaya ya Bagamoyo inatajwa kuwa kinara.

Lukuvi alisema, wakuu hao wa mikoa wana askari wanaoweza kuwaondoa waliojimilikisha  ardhi kinyume cha sheria.

“Tumieni mabaraza ya ardhi yaliyoundwa kisheria kuondoa wavamizi kwenye maeneo ambayo yanamilikiwa kisheria” alisema.

Naye Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga aliwahimiza wawekezaji kuwekeza kwenye kilimo cha alizeti na michikichi kwa ajili ya mafuta ya kupikia.

Hasunga alisema, kuna uhitaji wa mafuta ya kula tani 650 ambazo kiasi cha shilingi bilioni 675 zimekuwa zikitumika kuagiza mafuta kutoka nje ya nchi.

Alisema, upande wa mafuta wawekezaji ni wachache, hivyo wakipatikana wengi wataokoa fedha ambazo zinaenda nje.

Aidha kuhusiana na mikopo kwa wakulima alisema, kwa anayetaka kulima awasiliane na mfuko wa pembejeo pamoja na benki ya kilimo kupata taratibu.

Akihitimisha mkutano huo Waziri Kairuki aliwahahakikishia kuwa majibu yote ambayo hayajapatikana papo hapo wizara inaandaa bango kitita ambalo malalamiko na changamoto zote zitajumuishwa na kupelekwa kwa ajili ya kufanyia kazi ngazi zote ikiwamo kwa Rais na Waziri Mkuu.

Aliwapongeza wawekezaji wazawa ambao wameweza kusajili miradi zaidi ya 70 kwa mwaka huu pekee huku akizitaka taasisi za kibenki kuondoa urasimu katika kutoa mikopo kwa wawekezaji wazawa badala yake waweke mazingira rafiki.

Mkutano wa Kibaha ulihudhuriwa na Taasisi wezeshi, mwenyekiti wa wafanyabiashara Mkoa wa Pwani, mwenyekiti wa wafanyabiashara ndogondogo machinga, wawekezaji pamoja na viongozi wengine kutoka Halmashauri na Mkoa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles