31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Spika: Tutafanya kazi na ofisi ya CAG, si Assad

Na RAMADHAN HASSAN

-DODOMA

MNYUKANO wa Spika wa Bunge, Job Ndugai na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad umeendelea baada ya kiongozi huyo wa bunge kusema chombo hicho hakijakataa kufanya kazi na  ofisi ya CAG bali kimekataa kufanya kazi na Profesa Assad.

Kauli hiyo ya Ndugai imekuja ikiwa ni siku moja tangu Profesa Assad kusema suala hilo inabidi liangaliwe kwa busara zaidi kwani linaweza kuwa na athari kubwa kuliko linavyotazamwa.

Katika kauli yake, Profesa Assad alisema; “Mimi nafikiri tukae chini tutazame halafu tuone athari ni zipi ili kuepuka tatizo ambalo linaweza kutokea. 

“Ninaamini kuna watu wana busara na ‘probably’ wanatoa busara zao, wasiwasi wangu ni kwamba linaweza kuwa tatizo kubwa kuliko lilivyo sasa hivi. 

 “‘Technically’ inaweza kuibua ‘constitutional crisis’ (mgogoro wa kikatiba) kwa sababu ripoti (Ripoti za Ukaguzi wa Hesabu za Serikali za mwaka 2017/18) imeshawasilishwa kwa Rais na mimi siwakilishi ripoti bungeni. 

“Kwa hiyo Rais atasababisha ripoti zile ziende bungeni katika siku sita zijazo na kama Bunge litakataa kuzipokea, hiyo itakuwa tatizo kubwa zaidi. Kwa hiyo wasiwasi wangu ni huo. Na zikishawasilishwa bungeni zinakuwa ‘public document’, mimi ninapata fursa ya kuzungumza.

 “Tafsiri ya kwamba hatutafanya kazi na CAG ni tafsiri pana sana, inatakiwa tuijue vizuri na kama nilivyokwambia mimi bado sijapata hizo habari kwa uhakika (za Bunge kukataa kufanya naye kazi), ninazitafuta leo (jana) na nitaongea na watu wangu, kisha tutafanya tathmini ni nini cha kufanya.”

Alipoulizwa endapo anaweza kuchukua ‘uamuzi mgumu’ , Profesa Assad alisema: “Sina maamuzi yoyote ya kuchukua bwana, ninachofanya mimi hapa ni kufanya dua tu basi, watu waongoze vizuri, wafanye maamuzi ambayo yana faida na nchi hii basi, lakini mimi sina cha kufanya, nina ‘constitution duties’ (majukumu ya kikatiba) zangu nitaendelea nazo na nitaendelea kuzitekeleza.”

NDUGAI AJA NA MPYA

Jana baada ya kipindi cha maswali na majibu, Ndugai alisema; “vyombo vya habari vimekuwa vikiripoti tofauti kuhusiana na lile azimio la Bunge na kwamba tumekataa kufanya kazi na Ofisi ya CAG.

“Hakuna sehemu yoyote ambayo Bunge limekataa kufanya kazi na Ofisi ya CAG. Bunge hili limekataa kufanya kazi na mtu ambaye ni Profesa Assad basi, tusiripoti tofauti tukauchonganisha umma kwa kuuchanganya.”

Jana jioni Ndugai alifanya mkutano na waandishi wa habari na alipoulizwa kama ataipokea ripoti ya CAG ikiwa na saini ya Profesa Assad, alisema; “hili habari ya saini hilo halinihusu, sisi hatufanyi kazi na Assad.”

Alisema yeye ameaminiwa na watu wa Kongwa na wabunge wengine pia wameaminiwa na wananchi sio mbuzi. 

“Huyu aliyetudharau sisi, mimi kule Kongwa ndio wameniamini, tena hii mara ya nne, mimi sio mjinga, ndivyo walivyoingia wote, mtu kaaminiwa na watu sio mbuzi na hatujamchokoza yeye anakwenda huko anasema.

“Hii vipi na mnajua kwanini tunakasirika, baadhi yetu huwa mnaingia kwenye Kamati ya PAC, mmewahi kukuta kikao ambacho hakina maofisa wa CAG? Ni lazima wawepo wale.

“Ukifikia polisi ndio kwa IGP, wao ndio wanapitia hayo mapungufu halafu wanakuja hapo wanawapokea, sisi Bunge tupo pembeni, asubuhi wanakuja pamoja wakifika walioitwa wanaachwa nje.

“Wanakaa pale wale maofisa wa CAG wanaingia ndani ndio wanaeleza kwamba hawa wana mapungufu gani, walivyoridhika huko mnajuaje? Kwamba huko hawakupewa kitu chochote, wanasema tatizo ni mambo mawili na wao ndio wanapendekeza.

“Yaani tofauti na afisa yeyote Ofisi ya CAG ni ‘part’ ya kila kitu. Hivi mtu ambaye umeshirikishwa kiasi hicho unawezaje kukaa pembeni na kusema dhaifu, yule sio mimi wakati wewe ni ‘part’ (sehemu) na hii ni tabia fulani ambayo siyo ya kiungwana, lile jambo lilitukera,” alisema Spika Ndugai.

Alisema alipoulizwa alisema kwamba anajibu kihasibu akaambiwa tupe kamusi ya kihasibu.

“Hatuendi hivyo duniani, kama mtu analalamika neno lako linanikwaza unaomba msamaha mambo yanaendelea kama kawaida,” alisema.

LEMA

Alipoulizwa juu ya kutaja deni la Lema juzi, alisema huenda akawa sio peke yake anayedaiwa, lakini akasisitiza kwamba jambo hilo limemchanganya. 

“Wewe unaweza kusema huogopi risasi, mimi naogopa,” alisema Ndugai.

BUNGE KUTODHAMINI TENA MIKOPO YA WABUNGE

Katika hatua nyingine, Spika Ndugai alisema kwamba wanaangalia utaratibu Bunge lisiwe wadhamini wa mikopo ya wabunge.

“Next time (wakati mwingine) niwepo nisiwepo tusiruhusu kudhamini wabunge kuingia katika madeni kiasi hiki.

“Ni uhuru wa kujadili lakini hayo ni maoni yangu, next time atakayekopa benki atakopa yeye mwenyewe wala hatutajua hizo takwimu.

“Wakati mwingine huenda kodi zenu zikatumika kulipa hayo madeni, kwanini iwe hivyo?” alisema.

Alipotakiwa kutolea ufafanuzi kuhusu wabunge wa Chama cha CUF waliotimuliwa kuhusiana na hatma ya mikopo yao, Spika Ndugai alisema jambo hilo limekuwa likiwapa wakati mgumu. 

“Katika mitihani ambayo tunayo ni ile ya wale wabunge sijui kumi sijui nane, wanadaiwa zaidi ya bilioni moja na hawana uwezo wa kulipa na mikataba ile ipo hovyo hovyo, kama watakazia inawezekana kuna fedha zenu zikatumika kulipa,” alisema Spika Ndugai.

ILIVYOKUWA SAKATA LA CAG NA BUNGE

Januari 20 mwaka huu, Profesa Assad alifika mbele ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge huku kamati hiyo ikitumia zaidi ya saa tatu kumhoji.

Kuhojiwa huko kulikuja kufuatia wito wa Spika Ndugai alioutoa Januari 7, mwaka huu kumtaka kufika kwenye kamati hiyo kutokana na kauli yake ya kuliita Bunge ni dhaifu vinginevyo atapelekwa akiwa amefungwa pingu.

Profesa Assad alipokuwa akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa aliulizwa juu ya ripoti zake za kila mwaka ambazo baadhi ya watu wanaona kama hazifanyiwi kazi.

CAG akijibu swali hilo alisema; “hilo ni jambo ambalo kimsingi ni kazi ya Bunge. Kama tunatoa ripoti zinazoonyesha kuna ubadhirifu halafu hatua hazichukuliwi, huo kwangu ni udhaifu wa Bunge. Bunge linatakiwa kusimamia na kuhakikisha pale panapoonekana kuna matatizo basi hatua zinachukuliwa.

“Sisi kazi yetu ni kutoa ripoti. Na huu udhaifu nafikiri ni jambo lenye kusikitisha. Lakini ni jambo ambalo muda si mrefu huenda litarekebishika. Ni tatizo kubwa ambalo tunahisi Bunge linashindwa kufanya kazi yake kama inavyotakiwa.

“Sitaki kuwa labda nasema hili kwa sababu linahusisha watu fulani, lakini ninachotaka kusema ni kuwa Bunge likifanya kazi yake vizuri, hata huu udhaifu unaoonekana utapungua.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles