27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

SOKO LA KARIAKOO LADAI SHERIA MPYA ISIYOWABANA KUJIONGEZA

NA TUNU NASSOR-DAR ES SALAAM


SOKO la Kariakoo ni soko kuu lililopo katikati ya Jiji la Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla na lipo kati ya mitaa ya Nyamwezi, Mkunguni, Sikukuu na Tandamti.

Soko hili lipo chini ya Shirika la Masoko ya Kariakoo (SMK), limekuwa likitegemewa na wakazi wa Dar es Salaam hasa katika kujipatia mahitaji yao ya  kila siku.

Pia limekuwa ni soko tegemeo la wakulima wa mikoa mbalimbali ambao hulitumia kuuza mazao yao ya chakula na bidhaa zao.

Hata hivyo, soko limekuwa likikumbwa na changamoto mbalimbali ambazo zinahitaji kupata ufumbuzi wake mapema.

Kaimu Meneja wa Soko hilo, Donald Sokoni, anasema mgongano wa kimasilahi kati ya soko hilo na manispaa zilizopo jijini Dar es Salaam unasababisha kukimbiwa  na wakulima wanaoleta bidhaa katika soko hilo.

Anasema kitendo cha Manispaa ya Ilala kuzuia magari ya mizigo kuingia mjini mchana, kunasababisha wakulima kupeleka mazao katika masoko mengine.

“Manispaa ya Ilala ina masoko yake ambayo yanashindana na Kariakoo, hivyo agizo la kuzuia magari ya mizigo kwa madai ya  kupunguza msongamano mjini ni sababu za ushindani wa kibiashara na masoko yao,” anasema Sokoni.

Anasema changamoto hii inasababisha SMK kufikiria namna ya kuitatua kwa kuanzisha masoko mengine pembezoni ili wakulima waweze kufikishia mizigo yao huko wakati wa mchana.

 

“Kariakoo tunataka kuifanya kuwa kama ‘Super makert’, bidhaa zote zitafikishiwa katika masoko ya pembezoni na yakishafungashwa katika vifungashio bora ndipo yaletwe,” anasema Sokoni.

 

“Hii itasaidia  kuondoa msongamano wa magari na kupunguza uzalishaji wa taka katika soko hilo,” anasema Sokoni.

 

Anaongeza kuwa kwa sasa wako katika mazungumzo na halmashauri za wilaya mpya za Ubungo na Kigamboni ili waweze kupata maeneo ya kujenga masoko hayo.

 

Anasema pia changamoto nyingine ni soko hilo kuzidiwa kwa wafanyabiashara na kusababisha baadhi yao kukosa maeneo ya kufanyia shughuli zao.

 

“Tuna wafanyabiashara wengi kwa sasa lakini eneo tulilonalo halitoshelezi kukidhi mahitaji halisi ya wafanayabiashara hao, hivyo kuanzisha masoko pembezoni itasaidia kukidhi mahitaji haya,” anasema Sokoni.

Anasema changamoto nyingine ni uvamizi wa eneo la soko unaofanywa na wamachinga ambao huuza bidhaa ambazo zinapatikana sokoni, hivyo kusababisha wafanyabiashara wa ndani ya soko kukosa wateja.

“Tumevamiwa na wamachinga pande zote za soko na bidhaa wanazouza ni zilezile  zilizopo sokoni,  jambo ambalo linapunguza idadi ya wateja wanaoingia ndani,” anasema.

Anasema hata hivyo SMK inatamani kujitanua kibiashara katika mikoa mingine, lakini kwa mujibu wa sheria iliyoanzisha soko hilo inaonesha kuwa soko hilo litatoa huduma zake jijini Dar es Saalam tu.

“Tupo kwenye mchakato wa kuomba kubadilishwa kwa vipengele vilivyopo katika sheria ili iruhusu kwetu kwenda katika mikoa mbalimbali,” anasema Sokoni.

Anaongeza katika sheria namba 36 ya mwaka 1974 iliyoanzisha soko hilo, kuna baadhi ya vipengele vimepitwa na wakati kwa kuwa wakati linaanzishwa lilikuwa ni kwa ajili ya kutoa huduma.

“Sheria hii inalitaka shirika linapotaka kupandisha kodi kwa wapangaji wake ni lazima likae nao wajadili ndipo kodi zipande, wakati huo tulikuwa tunatoa huduma lakini kwa sasa tumeingizwa katika biashara huku bado sheria iko vilevile,” anasema.

Aidha, anasema pamoja na changamoto hizo, yapo mafanikio yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwa soko hilo.

Anasema hali ya usafi imekuwa ikiimarika siku hadi siku katika soko hilo kutokana na mipango wanayojiwekea.

“Hakuna soko kwa hapa Dar es Salaam linaloweza kutufikia kwa usafi hivyo soko letu ni safi zaidi,” anasema.

Anaongeza kuwa mafanikio hayo hayakuishia hapo tu, vilevile soko hilo limekuwa na ulinzi mkubwa, hali ambayo imepunguza kabisa wizi sokoni hapo.

“Hakuna wizi kwa sasa sokoni hapa kwani tuna askari wanaoshirikiana na kampuni ya ulinzi huku kamera za CCTV nazo zikisaidia,” anasema Sokoni.

Kaimu Meneja huyo anaongeza kuwa wameanza kuimarisha kipato cha shirika  hilo kwa kujenga maduka madogo madogo pembezoni.

“Tunaendelea kubuni miradi itakayowezesha kuwa na vyanzo vingine  zaidi vya mapato,” anasema.

Sokoni anatoa wito kwa wawekezaji kujitokeza na kujenga masoko madogo katika maeneo yao makubwa yaliyopo Tabata Bima na Mbezi Makonde.

Wadau wanena

Wadadisi wa mambo wadai kuwa tatizo kubwa la soko hilo ni  kuwa na uongozi ambao umekosa ubunifu wa ufanyaji shughuli kwa tija na kuweza kuisaidia nchi kujiongeza kiuchumi na maendeleo.

Wanasema kama wangejipanga soko hilo lingeweza kupeleka nje bidhaa za Tanzania zikiwamo matunda, viazi vitamu, magimbi, mbogamboga, maharage mabichi  na samaki kutoka soko la feri, kwani wanao uwezo wa fedha kufanya hayo, lakini wakabaki kufukuzana na machinga.

Wazo la Supermarket si la kwao kwani ni Kamishna Charles Kaenja amabaye wakati wa Kamisheni ya Jiji alipanga ili kupambana na kukithiri uchafu ni kuwa mazao mengi ya wakulima yana vifungashio duni na hivyo iliamuriwa mizigo yao ishushwe Mbezi Mwisho na kutolewa taka hizo na bidhaa kupelekwa Kariakoo zikiwa safi.

Wadau wengine wanalilaumu soko kuwa mlezi wa vibaka wa jiji.

 

mwisho

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles