30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

“Soka la walemavu wa viungo linaweza kuibeba Tanzania”

NA WINFRIDA MTOI

MCHEZO wa soka kwa watu wenye ulemavu unaojulikana pia kwa jina la ‘Amputee football’, umeanza kuchezwa hapa nchini.

Tayari ligi ya soka ya walemavu imeanzishwa.

Awali mchezo huo, ulikuwa ukichezwa kwa kujifurahisha lakini, baada ya kuanzishwa kwa Shirikisho la Soka la Watu Wenye Ulemavu (TAFF), umeanza kuchezwa rasmi katika mashindano.

 Mara nyingi, mchezo huo unahusisha  walemavu  wenye mguu mmoja na ndiyo sababu kuna wakati  mashindano yake yanafahamika ‘Single Leg Amputee Sports’, licha ya kwamba, uhusisha pia walemavu wa viungo vingine.

Kwa Afrika, Angola ndio nchi inayoongoza kufanya vizuri katika mchezo huo, ambao mwaka jana ilifanikiwa kutwaa Kombe la Dunia, katika michuano iliyofanyika nchini Mexico.

Angola iliibuka mabingwa, baada ya kuifunga Uturuki mikwaju ya penalti 5- 4.

Tanzania pia inaonekana kuja juu katika mchezo huo, kwani TAFF licha ya kutokuwa na muda mrefu tangu kuanzishwa kwake, lakini tayari imeendesha ligi na kupata timu ya Taifa iliyoshiriki michuana ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa).

Michuano ya Cecafa ilifanyikaTanzania  mwezi uliopita, ikiwa ni mara yake ya kwanza .

Katika michuano hiyo, Tanzania ilishika nafasi ya tatu, Rwanda ilitwaa ubingwa, huku Kenya  ikimaliza nafasi ya pili.

Licha ya timu ya Tanzania maarufu Tembo Worries kushiriki kwa mara ya kwanza na  kushika nafasi ya tatu katika michuano hiyo, imefanikiwa kuipaisha nchi katika  viwango vya mchezo huo, ikishika namba moja kwa ubora katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Kutokana na hatua hiyo, Tembo Worries, inatarajia kuiwakilisha Tanzania katika michuano ya Kombe la Mataifa Afrika kwa watu wenye ulemavu, itakayoanza  Septemba 30 hadi Oktoba 14, mwaka huu nchini Angola.

Kwa sasa kikosi hicho, kipo katika maandalizi ya michuano hiyo na kutokana  ubora iliouonyesha timu ya Nigeria ambayo nayo itashiriki  mashindano ya Afrika, imeomba mchezo wa kirafiki na Tanzania.

Mechi hiyo ilitarajiwa kuchezwa Jumapili hii,  lakini  umesogezwa mbele hadi mwezi ujao kutokana Nigeria kutaka kukamilisha bajeti zao kabla ya kuondoka nchini kwao.

Kuelekea michuano hiyo ya Afrika, MTANZANIA limezungumza na Katibu Mkuu wa TAFF, Moses Mabula ili kufahamu kinachoendelea hasa katika kuhakikisha mchezo huo unakua.

Mabula anasema hatua waliyofikia kwa kufanikiwa kuingia katika timu bora za Afrika na kushiriki michuano mikubwa, inawapa moyo wakuendelea kupambana.

 Anasema kwa sasa wameanzia Mkoa wa Dar es Salaam, walianza na ligi iliyokuwa na timu nne na kuchagua wachezaji wa timu ya taifa iliyoshiriki Cecafa.

Anaeleza kuwa, baada ya kufanya vizuri Dar es Salaam, wanafikiria kuingia katika mikoa ya karibu kama Pwani, kuanza kuhamasisha mchezo huo kabla ya kwenda mikoa mingine.

“Bado shirikisho letu ni changa, limeanzishwa mwaka Julai mwaka jana na tumefanya ligi mara moja na kuchagua timu ya taifa, mambo yakikaa sawa tunatarajia kuingia katika mikoa ya karibu kwanza kabla ya kuueneza katika mikoa mingine Tanzania nzima,” anasema Mabula.

Kuhusu maandalizi kuelekea mashindano ya Afrika, anasema Tembo Worriers imeanza mazoezi na kama Nigeria watashindwa kutokea watacheza mechi za kirafiki na timu nyingine za Ukanda wa Afrika Mashariki.

“Programu ya mazoezi tumeanza muda mrefu kawa sababu tulikuwa tunarajia kucheza mechi ya kirafiki, hata kama haitakuwepo kwa wakati huu,  hatutasitisha mazoezi,” anaeleza.

Anaendelea kueleza kuwa, katika kuhakikisha wanafanya vizuri katika michuano ya Afrika nchini Angola, wamempa majukumu kocha Salvatory Edward, kukinoa kikosi hicho.

Mabula anasema, Edward amejitolea  kuisaidia timu hiyo katika  mambo ya kiufundi  na watakuwa naye hadi  katika michuano hiyo.

“Tunajianda vizuri tunataka kwenda kuonyesha ushindani, licha ya kuwa ni mara ya kwanza kushiriki kama tulivyofanya Cecafa, kitu kizuri kwa sasa tuna kocha Salvatory Edward anayetusaidia mambo ya kiufundi,” anafafanua.

Waomba wadau kuwasaidia

Anasema katika michuano hiyo, timu inajigharamia yenyewe usafiri wa kwenda na kurudi, lakini mambo mengine yanagharamiwa na waandaaji kama vile chakula na malazi.

Anafafanua kuwa, kiasi cha fedha kinachohitajika kukamilisha safari ni sh 170 milioni na wameandaa harambee inayotarajia kufanyika mwezi ujao, Dar es Salaam.

“Kiasi kidogo cha fedha tulichonacho kwa sasa, tunakitumia kuwatengenezea hati za kusafiria wachezaji, kwa sababu wote hawana na matumizi  mengine ya maandalizi.

“Rai yangu kwa Watanzania wapende michezo yote na wajitokeze katika  harambee hiyo katika siku tutakayoitangaza hivi karibu.

“Kama tumefanya vibaya katika Afcon ya soka la kawaida, kwa jitihada zinazoonyeshwa na wachezaji wa Amputee, timu yetu inaweza ikawafuta machozi ya miaka mingi,” anasema.

Changamoto

Mabula anasema, changamoto kubwa waliyonayo ni wachezaji wengi kujilea wenyewe kupitia mitaji yao midogo ya bajaji, lakini kwa wale wasiokuwa nazo inakuwa ni vigumu kupata nauli ya kuhudhulia mazoezi.

Anasema pia kuna uelewa mdogo wa watu kuhusu mchezo huo, imekuwa ni tatizo kwa sababu wameendesha michuano mikubwa kama Cecafa, lakini mahudhurio yamekuwa  hayaridhishi.

“Fikiria hata watu wenyewe wenye ulemavu,  wamekuwa hawajitokezi katika mashindano, lakini tumepanga kutoa elimu kwa njia mbalimbali ikiwamo semina,” anaeleza.

Amputee Football ni maarufu katika nchi mbalimbali duniani, tofauti na Angola kuwa nchi ya kwanza Afrika kuchukua Kombe la Dunia, nchi nyingine zilizowahi kutwaa ubingwa huo ni Urusi ikichukua mara nne mwaka 1998, 2002, 2003 na 2014.

Nyingine ni Brazil ilichukua mwaka 2000, 2001 na 2005,  Jamhuri ya Uzbekistan, ilitwaa kombe hilo  mara tatu mfululizo mwaka 2007,2010 na 2012.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles