25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Sitta alisaidia kujenga upinzani bungeni

sitta-1NA MWANDISHI MAALUMU,

MIONGONI mwa mambo ambayo hutia ukakasi ni kwa namna ambavyo wasomi wengi wa Tanzania mbali na kuvaa majoho yao baada ya kuhitimu vyuo, lakini wamekuwa wakishindwa kutoa uelekeo chanya kwa kutumia jicho pevu ili kuweka uwiano sawa kati ya watawala na watawaliwa kwa ajili ya mustakabali wa taifa letu.

Mfumo huu wa wanataaluma wetu kuwa makasuku na wakati mwingine bendera fuata upepo ulianza mapema katika awamu ya kwanza katika utawala wa mwalimu Julius Nyerere.

Haijulikani sababu iliyopelekea wasomi wengi kuanzia utawala wa Mwalimu kuwa watu wa kusifia badala ya kukosoa, kushauri na kutazamisha,  kama ni mfumo wa uongozi uliokuwepo kwamba ulikuwa unaogopa kukosolewa chini ya mwavuli wa kuijenga nchi  au ni woga wa wahusika wenyewe.

Nasema mfumo wa uongozi uliokuwepo kwa maana inasemekana kumkosoa Mwalimu Nyerere ambaye tayari alikuwa ameishajizungushia wigo wa kuaminiwa na wananchi kwamba yeye ni mkombozi, kulihitaji kujitoa muhanga kama mtu anayehitaji kuonja nyongo ya mamba.

Wengi wa waliothubutu kumkosoa Mwalimu kwa lengo la kutaka mabadiliko ya uongozi,  kiuchumi au kujiimarisha kisiasa kama si kupotea katika anga za kisiasa basi waliikimbia  nchi.

Hata hivyo pamoja na mazingira tata katika kumkosoa Mwalimu bado wapo baadhi ya wasomi waliojaribu kukunjua makucha kwa yale mambo ambayo yalikuwa yakiwakera japo bado kibano kilikuwa palepale.

Haya Samuel John Sitta tunayemlilia hivi leo anaweza kuingizwa kwenye vitabu vya historia kwamba yeye ni miongoni mwa wasomi wachache tena bado wakingali wanafunzi wa vyuo vikuu waliweza kumtikisa Mwalimu Nyerere.

Sitta alisoma shahada yake ya kwanza katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwa muda wa miaka saba maana mwaka 1966   aliwashawishi wanafunzi wenzie wapatao 399 kufanya mgomo na kuandamana kupinga kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na kukatwa pesa.

Mbali na mgomo huo wanafunzi hao walitoa maneno ya kumkasirisha mwalimu wakati huo akiwa Rais mpaka akawafukuza chuo pale waliposema: ‘‘Heri wakati wa ukoloni kuliko utawala wa Mwalimu Nyerere.’’

Hata hivyo wanafunzi wapatao 392 walikuja kupata msamaha kutoka kwa Mwalimu mwenyewe baada ya hasira kali kupungua huku  wanafunzi wengine wapatao saba vinara wa mgomo huo akiwamo Sitta wakikataliwa msamaha.

Baada ya ushawishi wa viongozi wa chuo wakati huo, Mwalimu alikubali na kuandika barua zenye kumb. Na C3/Sa.13 ya 2/3/1967 na C3/Ss.13 ya 9/7/1967 ambapo alikubali vijana hao warejee chuoni kwa sharti la watukutu wawili Sitta na Mwabulambo watandikwe viboko.

Wahenga walisema: ‘‘Usione vyaelea vimeundwa’’Utundu, utukutu, ujasiri na kujiamini ambavyo tumekuwa tukivishuhudia kwa Sitta katika enzi za uhai wake katika nyanja mbalimbali za uongozi wake kisiasa,  havikuanza leo bali vina historia yake.

Uwezo wa uongozi wa Sitta ulikuja kudhihirika waziwazi mwaka 2005 wakati alipochaguliwa kuliongoza Bunge la Tisa.

Wakati mwanasiasa huyu akianza kuliongoza Bunge hilo alianza kwa kasi huku akisema atalifanya Bunge kuwa la ‘‘Standard and Speed.’’ Hata hivyo pamoja na mbwembwe zake hizo bado wananchi na wanasiasa wengi walisema kwamba hizo ni guvu za soda maana hawezi kubadilisha chochote ndani ya mfumo wa CCM.

Kumbe kuishi kwa mazoea wakati mwingine unaweza ukaikosea nafsi yako kwani hisia ambazo zilikuwa zimetanda ndani ya mioyo ya wananchi zilikuwa kinyume dhidi ya mwanasiasa huyu kwani baada ya hapo aliweza kuonyesha kwa vitendo kile alichokisema kwa maneno.

Ni katika Bunge la Tisa chini ya mfumo wa vyama vingi tulishuhudia mijadala ikiendeshwa bila upendeleo wa kusema aliyetoa mchango ni wa kutoka chama tawala au upinzani. Yote haya ni mafanikio na ubunifu wa Sitta.

Ni dhahiri Sitta alikuwa Spika wa wabunge wote aliyekuwa na moyo wa kifua kuvumilia mawazo tofauti ya wabunge ili kuhakikisha mijadala inapitishwa kwa amani huku kila mmoja akiwa ameridhika.

Si tu Sitta alikuwa na uwezo wa kuwaunganisha wabunge wa pande zote mbili kwa maana ya kutoka chama tawala na upinzani bali pia aliweza kukabiliana na changamoto nyingi zikiwemo za ufisadi na rushwa.

Ni ukweli usiopingika katika Uspika wa Sitta kutokana na kuwepo uwazi na demokrasia pana ndani ya Bunge ndipo paliibuka kashfa zenye kutikisa ikiwamo ya Richmond ambayo  inasemekana kuna fedha nyingi za wananchi zilipotea  kwa uzembe au kwa utashi wa wahusika.

Kutokana na Sitta kuwa shupavu na mwenye kujiamini aliweza kuwaongoza wabunge wote wakajadili suala la kashfa hiyo kwa ajili ya masilahi ya Taifa na kupelekea Waziri Mkuu wakati huo, Edward Lowassa na wengine kujiuzulu.

Ni Spika pekee aliyesaidia kuwafanya wananchi hasa vijana kulipenda Bunge lao hivyo na wao kuwa na ndoto za kutaka siku moja kuwa wabunge kutokana na jinsi walivyokuwa wakijenga hoja zenye mashiko mbali na utofauti wao wa itikadi za vyama.

Kwa haraka haraka unaweza kusema Sitta ni miongoni mwa wanasiasa waliochangia kuujenga upinzani na hivyo kuendelea kupata wabunge wengi baada ya michango yao ya kupinga ufisadi kuwa wazi ndani ya Bunge katika miaka mitano ya uongozi wake.

Spika huyu ambaye ametangulia mbele ya haki akiwa na umri wa miaka 74 baada ya kupatwa na umauti katika Hospitali ya Technical University of Munich nchini Ujerumani, historia yake ya kuongoza Bunge la Tisa katika viwango na kwa kasi ndiyo iliyopelekea apigiwe upatu na hatimaye kufanikiwa kuliongoza Bunge Maalumu la Katiba mwaka 2014.

Akiwa ameliongoza Jimbo la Urambo kabla halijagawanywa tangu mwaka 1975 hadi 1995 aliposhindwa katika uchaguzi mkuu wa vyama vingi na kufanikiwa kurejea tena kuliongoza jimbo hilo likiwa tayari limegawanywa yeye akichukua upande wa Mashariki tangu mwaka 2005 hadi 2015 ni ishara tosha kwamba  hakuwa mwanasiasa mwenye  wepesi wa kukata tamaa.

Kama wanasiasa wengine walivyo na kiu na tamaa ya kushika nyadhifa za juu zaidi kiuongozi ili kukuza na kuyapaisha majina yao,  ndivyo ilivyokuwa kwa marehemu Sitta kwani mbali na kuwa Mbunge wa Urambo miaka 35  kwa nyakati tofauti bado alithubutu kuwania kuteuliwa kugombea kiti cha Urais kupitia  tiketi ya CCM mwaka 2015 japo alibwagwa chini.

Pamoja na  mwanasiasa huyu aliyeongoza Bunge la Tisa kwa kasi na viwango kulaumiwa kuwa aliboronga wakati wa kuliongoza Bunge Maalumu la Katiba kwa kuibeba CCM, bado atakumbukwa kama msomi aliyeitendea haki taaluma yake ya sheria kuliko wasomi wengi wa siku hizi ambao wamekuwa makasuku huku wakibaki  wakisifia watawala ili nao siku moja wakumbukwe katika ufalme.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles