24.4 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

SIRI YAFICHUKA KURA ZA CCM BUYUNGU

Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam


SIKU moja baada ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, kukiri kwamba Uchaguzi Mdogo Jimbo la Buyungu ulikuwa mgumu, mengine mapya yameibuka.

CCM ilishinda uchaguzi huo uliofanyika Jumapili, huku pia ikishinda uchaguzi mdogo wa madiwani katika kata 36, zilizofanya uchaguzi siku hiyo na 41 ambazo madiwani wake walipita bila kupingwa baada ya wapinzani kuenguliwa katika hatua za awali.

Taarifa kutoka Buyungu ambazo gazeti hili limezipata, zinadai kuwa moja ya mbinu walizotumia CCM kuibuka na ushindi ni kuweka ngumu katika kata nne ambazo wapigakura wengi hawakushiriki kupiga kura mwaka 2015 kwa sababu ya umbali wa makazi yao na vituo vya kura.

Baadhi ya kata hizo ni pamoja na Mtukuza na Nyambibuye zenye wapigakura zaidi ya 8,000.

CCM wanadaiwa waliweka pia nguvu kwenye Kata ya Kiziguzigu, anayotoka aliyekuwa mgombea wao, Christopher Chiza, ambayo kwenye uchaguzi wa mwaka 2015, walishindwa.

Kwa upande wao, Chadema, waliweka nguvu nyingi katika kata za Gwarama, nyumbani kwa aliyekuwa mgombea wao, Elia Michael, Kasuga ambako ni nyumbani kwa marehemu mwalimu Mwalimu Kasuku Bilago aliyekuwa mbunge, Kasanda na Kakoko mjini.

“Mwaka 2015 walipata kura nyingi kwenye maeneo haya, na mwaka huu waliweka tena nguvu nyingi wakijua kuna kura zao za kutosha, lakini wakasahau kwenye uchaguzi mdogo mwamko wa wapigakura huwa si mkubwa,” kilisema chanzo chetu.

CHADEMA WAJA NA MADAI MAPYA

Jana, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema, ambaye alikuwa Buyungu kuendesha kampeni hizo, alisema pamoja na rafu za CCM, wao wanaendelea kukusanya fomu za matokeo kutoka kwa mawakala wao ambapo hadi sasa  kata tisa walizonazo zikionyesha walipata kura zaidi ya 18,000, wakati zilizotangazwa ni 16,000.

Mrema alisema katika kampeni hizo, baadhi ya viongozi wakubwa waliokuwa nao ni pamoja na Mbunge wa Kigoma Mjini na Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, aliyekaa siku mbili na kufanya mikutano kwenye kata tatu.

Alisema Mbunge wa Kibamba na Naibu Katibu Mkuu bara wa chama hicho, John Mnyika, alikaa siku tatu na kufanya mikutano kwenye kata tisa, huku Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe, akikaa siku nne na kufanya mikutano katika kata 10.

 Kwa habari zaidi jipatie nakala yako ya gazeti la MTANZANIA.
- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles