23 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 17, 2024

Contact us: [email protected]

Siri ya Mbowe Kuzuiwa

mboweNa Waandishi Wetu, Dar na Dodoma
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, jana Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, alizuiwa kumaliza kusoma hotuba yake ambayo ndani yake ilikuwa ikiwalipua vigogo waliohusika na uchotwaji wa fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow huku akieleza kilichojificha ndani ya kashfa ya mtambo wa kufua umeme wa Dowans na Richmond.
Amesema suala hilo la Dowans na Richmond, lilichochewa na makundi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) , na sasa linaliligharimu taifa kwa kudaiwa Sh bilioni 120.
Wakati Mbowe akitakiwa kuketi kwa madai kuwa muda wake ulikuwa dakika 30 na zilikuwa zimeisha, mwanzo wa hotuba yake alikuwa amezungumzia masuala ya kura ya maoni, uandikishaji wapiga kura na Uchaguzi Mkuu.
Pamoja na juhudi za baadhi ya wabunge wa upinzani akiwamo Mbowe, kumweleza Spika wa Bunge, Anne Makinda kwamba kambi hiyo walikuwa wamekubaliana kiongozi wao atumie dakika 50 na wengine watumie 20 kila mmoja, kiongozi huyo wa Bunge aligomea hatua hiyo na kusema kanuni hairuhusu.
Mwiba wa Mbowe
Kati ya vipengele vilivyokuwa kwenye hotuba ya Mbowe ambavyo havikusomwa ni pamoja na kile kilichokuwa na kichwa cha habari ,‘Serikali Kupuuza na kulidanganya Bunge’.
Sehemu ya eneo hilo ilikuwa inasema: “ Taifa hili limekuwa mhanga wa mara kwa mara wa uzembe au kudanganywa na hata kupuuzwa kwa maazimio ya Bunge, ambalo kikatiba, ndilo lenye wajibu wa kuisimamia Serikali.
“Kupuuzwa huku kwa Bunge kunadhalilisha uwepo wa taasisi hii nyeti ya Taifa, kunaondoa uwajibikaji wa viongozi na watumishi wa Serikali na hatimaye kunalisababishia taifa hasara kubwa siyo tu kiuchumi katika maeneo yanayohusu musuala ya kiuchumi, bali pia katika upatikanaji haki katika taifa,” inasema hotuba hiyo.
Dowans/ Richmond
Katika sehemu ya hotuba ya Mbowe, ilisema: ‘Mlolongo huu wa kushindwa kusimamia nchi, kuendekeza makundi na vita vya siasa ndani ya CCM na Serikali yake kwa gharama ya taifa.
“Taifa hili sasa linadaiwa Sh bilioni 120 baada ya kushindwa kwenye kesi ya Dowans/Richmond katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi (ICC) huko Paris,” ilisema hotuba hiyo.
Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema, alisema Serikali haijataka kuliweka jambo hilo wazi na ni dhahiri kuna siri kubwa inayosababisha jambo hilo kuwa la usiri mkubwa.
“Huko mbele ya safari jambo hili litaligharimu taifa mabilioni haya ya fedha ambayo yangeweza kuepukika kama ukweli, uwazi na haki vingetawala mchakato mzima wa kashfa ya Richmond.
“Serikali isimame sasa na ilieleze taifa ni nani anasema kweli, ni nani alilidanganya Bunge na ni nani analindwa na serikali katika kashfa hii?” ilihoji.
Iliendelea kusema: “Mapambano ya mitandao ndani ya serikali ya CCM na minyukano ya kupigania maslahi na ulaji ndani ya mikataba mbalimbali ya miradi ya umma ikiongozwa na walio karibu na watawala na familia zao imeota mizizi katika serikali hii.
“Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ingependa kujua kwamba serikali hii ya CCM ambayo imefikia mwisho wake ni kwa nini inawaachia Watanzania madeni makubwa hivi?
“Je, kashfa hizo zote za serikali kushindwa kuwajibika, kutafuta visingizio vya kufunika madhambi yake, ndiyo maisha bora kwa kila Mtanzania ambayo wananchi waliahidiwa miaka 10 iliyopita?” alisema na kuhoji.
Alihoji na kutaka kujua kauli ya serikali juu ya tabia ya kuwabebesha wananchi mizigo ya madeni huku Serikali ikijitahidi kwa nguvu zake zote kuwasafisha viongozi walioitumbukiza nchi kwenye madhila hayo.
Escrow
Kuhusu kashfa ya Escrow, hotuba ya Mbowe ilieleza tangu kampuni hiyo ilivyoingia nchini mwaka 1994 na mawaziri waliokuwa kwenye wizara mbalimbali zinazodaiwa kuisaidia kuwekeza nchini mpaka kuchotwa kwa zaidi ya Sh bilioni 300 Benki Kuu (BoT).
“Watanzania wanajua na dunia inajua kwamba kama kuna wizi wa mchana kweupe umefanyiwa nchi hii ni kashfa ya Tegeta Escrow, watumishi wa umma wamehongwa mamilioni ya fedha, majina yametajwa.
“Pamoja na maazimio ya Bunge kuwataja kwa ushahidi jinsi walivyoshindwa kutekeleza majukumu yao, serikali imekuwa hailali eti ikitafuta njia ya kuwasafisha.
“Hii ni serikali pekee duniani inayokasirika Bunge likifanya kazi yake sawa sawa ya kuisimamia ndiyo maana mara nyingi imegeuka na kutafuta njia ya kufunika madudu ambayo siyo tu yameiaibisha sana, bali yamegharimu kodi nyingi za wananchi,” ilieleza hotuba hiyo.
Alisema Serikali inajua kwamba utekelezaji wa bajeti ya Serikali inayomalizika ya mwaka 2014/15 umekwamishwa na kashfa ya Tegeta Escrow baada ya nchi wafadhili kuzuia kutoa fedha za kuchangia fungu la maendeleo kutokana na tabia ya Serikali kufunika kombe mwanaharamu apite kwenye kashfa hiyo.
“Tunataka serikali iseme inapolinda na kubeba wahusika wa kashfa hizi inataka kuwasaidia wananchi au viongozi wameamua kujiunga dhidi ya wananchi wao?”
Mnyukano ndani ya Bunge
Mvurugano huo ulianza baada ya Spika Makinda kumtaka Mbowe akae kwa madai muda wake wa dakika 30 wa kusoma hotuba umemalizika.
Baada ya kauli hiyo, Mbowe alimweleza Spika Makinda kwamba kambi imekuabaliana kumwachia dakika za kusoma hotuba hiyo na kuimaliza, Makinda akamweleza kuwa huo siyo utaratibu.
“Mbowe kengele ya pili hiyo imelia lakini naona bado unaendelea kuwasilisha, naomba ukae chini anayefuata ataendelea kusoma.
Kanuni za Bunge zinawataka kutumia muda wa dakika 90 kuwasilisha hotuba tatu za kambi rasmi ya upizani ambazo ni hotuba ya Msemaji Mkuu wa kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Hotuba Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani anayeshughulikia Uwekezaji na Uwezeshaji na Hotuba ya Msemaji wa Tamisemi,” alisema Makinda.
Alisema kutokana na hali hiyo, muda wake umekwisha, hivyo basi anapaswa kukaa chini na msemaji mwingine aweze kuinuka na kuendelea.
Wakati Makinda akisema hayo, baadhi ya wabunge wa upinzani akiwamo, Tundu Lissu, David Silinde na Paulina Gekulu, walikuwa wamesima na kuwasha vipaza sauti kutaka kumtetea Mbowe.
Kutokana na hali hiyo, Makinda alisema: “ Tunapoteza muda jamani, kaa chini, mpishe msemaji mwingine awasilishe hotuba yake, mna tabia mbaya…msifanye ujanja ujanja hapa… naomba mkae chini tuelewane kidogo, nafuata kanuni hizi hapa,” alisema Makinda.

Kampeni bungeni
Baada ya kuwasilishwa hotuba hiyo wabunge wa upande wa Chadema na CCM walikuwa wakirushiana vijembe ndani ya Bunge huku kila mmoja akitamba kuibuka mshindi katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Aliyekuwa wa kwanza kuchangia hotuba hiyo alikuwa Mbunge wa Viti Maalumu, Mariam Msabaha (Chadema), ambaye alisema pamoja na kuzuiwa kwa kiongozi wao kutomaliza kuisoma hotuba hiyo, CCM ikae ikijua itaitoa nchi kwa Ukawa Oktoba mwaka huu.
“Pamoja na kushindwa kwa kila hila ninawaomba makada wote nendeni katika twitter, facebook, televisheni pamoja na magazeti mtaipata hotuba yote ya kiongozi na muisome.
“Sasa tunasema Ukawa ndiyo mpango mzima na CCM mnaitoa nchi mtake mistake, tendeni haki kwa Watanzania,” alisema
Baada ya kumaliza mbunge huyo alijikuta akipigwa vijembe kutoka kwa wabunge wa CCM waliochangia hotuba hiyo ya bajeti ya Waziri Mkuu, ambao ni Tauhda Cassin Nyimbo (Viti Maalumu), Ismail Rage (Tabora) na Ali Keissy (Nkasi Kaskazini).
Pinda na bajeti ya Sh trilioni 5
Awali Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliwasilisha bungeni makadirio ya Sh trilioni 5.763, kwa ajili ya matumizi ya ofisi yake kwa mwaka wa fedha wa 2015/2016.

Akiwasilisha makadirio hayo bungeni jana mjini hapa, Pinda aliliomba Bunge kuidhinisha kiasi hicho cha fedha, ambako kati ya hizo Sh bilioni 177.337 ni kwa ajili ya Mfuko wa Bunge, ikiwa ni matumizi ya kawaida na fedha za maendeleo.

Katika hotuba hiyo, Sh trilioni 4.766 zimetengwa kwa ajili ya halmashauri zote nchini na kati ya hizo Sh trilioni 4.023 ni za matumizi ya kawaida na Sh bilioni 743 ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Sh bilioni 311.763 zimeombwa kwa ajili ya ofisi ya waziri mkuu na taasisi zake na kati ya hizo Sh bilioni 264 ni za matumizi ya kawaida na Sh bilioni 47.283 ni za miradi ya maendeleo, huku ofisi za wakuu wa mikoa zikiombewa Sh bilioni 280.

TAMISEMI
Ofisi ya Waziri Mkuu -Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na taasisi zake imeombewa Sh bilioni 405.101, kati ya hizo Sh bilioni 50 ni za matumizi ya kawaida na Sh bilioni 354 ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

BUNGE
Ofisi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeombewa Sh bilioni 177.337 kwa ajili ya Mfuko wa Bunge.

Kati ya fedha hizo Sh bilioni 169 ni za matumizi ya kawaida na Sh bilioni nane ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Katika hotuba hiyo waziri mkuu pia alizungumzia masuala mtambuko na changamoto mbalimbali zinazoikabili Serikali likiwamo suala la rushwa, uharibifu wa mazingira na ongezeko la ajali za barabarani.

RUSHWA

Pinda alisema Serikali inaendelea na mapambano dhidi ya rushwa kwa kutekeleza Mpango Mkakati wa tatu wa taifa wa Kudhibiti Rushwa (NACSAP).

Habari hii imeandaliwa na Fredy Azzah, Patricia Kimelemeta na Koku David (Dar) na Khamis Mkotya (Dodoma)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles