30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Siri tano za wasichana walioongoza kitaifa kidato cha sita

Kaimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Tabora, Mathias Lubatula
Kaimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Tabora, Mathias Lubatula

NA NORA DAMIAN, DAR ES SALAAM

MATOKEO ya Kidato cha Sita 2016, yaliyotangazwa mwanzoni mwa wiki hii yanaonyesha ufaulu wa jumla katika mtihani huo umeshuka kwa asilimia 0.93 ikilinganishwa na mwaka 2015, ambapo ufaulu ulikuwa asilimia 98.87.

Katika matokeo hayo ufaulu wa mwaka huu ni asilimia 97.94, huku idadi ya watahiniwa waliofaulu vizuri katika daraja la kwanza, pili na tatu, ikiongezeka kwa asilimia 3.72 kutoka asilimia 89.41 mwaka 2015 mpaka asilimia 93.13 mwaka 2016.

Licha ya matokeo ya mtihani wa Taifa wa Kidato cha Sita kuonyesha wavulana kuongoza katika 10 bora, lakini pia wako wasichana walioweza kufanya vizuri katika mtihani.

Katika matokeo hayo wasichana bora katika masomo ya biashara ni Juliana (WeruWeu), Halima Kulava (Al-Muntazir), Albertina (Kazima), Lucy Sanga (Alpha), Husna Mori (Loyola), Rahmat Mandara (St Mary Goreti), Sauda Kitalima (Weruweru), Happiness Kira (St Mary Goreti), Itika Mwakisambwe (Weruweru) na Radegunda Dionis (Kazima).

Wasichana bora katika masomo ya lugha na sanaa ni Edith (St Mary’s Mazinde Juu), Zuhura Sakaya (Feza Girls), Editha (Bigwa Sisters Seminary), Vivian Magesa (Lake), Vaileth James (Chief Ihunyo), Christina Mtangi na Asnath Masanza (St Mary’s Mazinde Juu), Neema Paul (Tabora Girls), Lohi Ako (Weruweru) na Edna Leonard (Loyola).

Wasichana bora katika masomo ya sayansi ni Magreth (Marian Girls), Bertha Nguyamu, Mary Kilapilo na Regina Lugola (St Mary’s Mazinde Juu), Nola Matolo (Feza Girls), Selina Pius (Pandahili), Queenlisajoan Olan’g (Marian Girls), Nasma Nyindo (Kilakala), Sheikha Rashid (Feza Girls) na Lilian Hema (Tabora Girls).

Gazeti hili lilizungumza na wakuu wa shule na baadhi ya wanafunzi walioongoza kitaifai katika masomo ya sayans, lugha na sanaa ili kujua siri ya mafanikio yao.

WANAFUNZI

Bertha Nguyamu (18) kutoka Shule ya Sekondari ya St Mary’s Mazinde Juu iliyoko mkoani Tanga, ambaye ameshika nafasi ya pili kitaifa kwa wasichana wanaosoma masomo ya sayansi, anasema alikuwa akishirikiana na wenzake ambao karibu wote wamepata daraja la kwanza katika matokeo hayo.

“Shule yetu ina mazingira mazuri ya kujifunza na walimu wanajituma sana. Masomo yalikuwa mengi na kuna wakati nililazimika kupunguza muda wa kulala nikawa nalala kwa saa mbili au tatu ili kupata muda zaidi wa kujisomea,” anasema Bertha ambaye alikuwa akichukua mchepuo wa Fizikia, Kemia na Hisabati.

Mwanafunzi huyo ambaye pia ameshika nafasi ya tisa kitaifa, anasema walikuwa wanaamka alfajiri na kuanza kujisomea kisha kuanzia saa 12 hadi saa 1 huingia katika misa na baada ya hapo hupata chai kisha kuingia darasani.

Bertha pia alikuwa kiongozi katika klabu ya wanafunzi wa sayansi shuleni kwao, anasema matarajio yake ni kuwa mtaalamu wa mafuta na gesi na kwmaba amevutiwa kusoma taaluma hiyo ili kuendeleza rasilimali zilizopo nchini.

“Mafanikio yapo kwa kila mtu lakini lazima mtu afanye bidii kwa sababu hakuna kitu kinachoshindikana, nawashauri wasichana wasijishushe kwamba hawawezi masomo ya sayansi bali wajitume kwa kusoma vitabu kwa wingi,” anasema.

Mwanafunzi huyo anaishauri serikali kutoa mikopo kwa wanafunzi wote na kuacha kuwabagua wale waliosoma katika shule za watu binafsi.

Baba mzazi wa Bertha, Peter Nguyamu ambaye ni daktari katika Hospitali ya Mtakatifu Benedict iliyopo Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara, anasema mwanawe alikuwa na juhudi kubwa za kusoma tangu alipokuwa shule ya msingi.

“Alikuwa anapenda sana shule na tulikuwa tunamtia moyo asome kwa bidii. Wazazi wana sehemu kubwa katika maendeleo ya watoto hivyo ni vizuri wafuatilie kwa makini na kama kuna sehemu za kusahihisha wafanye hivyo mapema.

“Wazazi wawasikilize watoto wanahitaji nini, wasiwaburuze bali wawape uhuru watoto kuchagua wanachojitaji,” anasema Dk. Nguyamu.

Naye Regina Luoga kutoka katika shule hiyo ambaye alishika nafasi ya nne katika masomo ya sayansi anasema; “Mungu ndiye amewezesha yote na matarajio yangu ni kuwa mtaalamu wa mafuta na gesi kwa sababu taaluma hiyo ndiyo iko katika soko la ajira kwa sasa.

Neema Paul kutoka Shule ya Sekondari ya Wasichana Tabora aliyeshika nafasi ya nane katika masomo ya lugha na sanaa anasema; “Kikubwa unatakiwa kutambua na kuheshimu kwamba wewe ni mwanafunzi na ukishatambua hilo kinachofuata ni kutumikia uanafunzi wako.

“Pia unatakiwa uwe na mpangilio mzuri wa muda, kujali mchango wa mwalimu na mlezi hasa unapokuwa shuleni na zaidi ya yote kusoma kwa bidii ndio msingi wa mafanikio,”.

Anasema matarajio yake ni kusoma sheria lakini atawashirikisha wazazi na ndugu zake wa karibu katika suala hilo.

Mwanafunzi mwingine Lilian Hema kutoka katika shule hiyo ambaye alishika nafasi ya 10 katika masomo ya sayansi, anasema kitu kikubwa ambacho kimemsaidia ni kujituma na kupata msaada kutoka kwa walimu na wazazi.

Lilian ambaye ni mtoto wa sita kati ya watoto wanane, anasema ndoto yake ni kuwa daktari.

Kwa upande wake Zuhura Sakaya kutoka Shule ya Wasichana ya Fezza aliyeshika nafasi ya pili kitaifa katika masomo ya sanaa na lugha, anasema kujiamini na kumwamini Mungu ndiyo siri ya mafanikio yake.

“Nawaasa wasichana wenzangu wakikutana na changamoto tofauti wapambane nazo na kuziepuka,” anasema Sakaya.

WALIMU

Kaimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Tabora, Mathias Lubatula, anasema wameweka utaratibu wa kufanya mitihani mara tatu kwa kila wiki ambayo inasaidia kuwapima wanafunzi vizuri.

“Hii mitihani huwa tunaiita Fitnes Test na huwa inafanyika Jumatatu, Jumatano na Ijumaa, pia huwa tunafanya mitihani na kushindanishwa na shule zingine za vipaji maalumu kama Tabora Boys, Msalato, Kilakala na za binafsi ambazo ziko vizuri kitaaluma.

“Kuna ongezeko kubwa la wanafunzi hivyo usiku inabidi mwalimu arudi kuja kufundisha kwa sababu ukifundisha wanafunzi wachache uelewa unakuwa mkubwa,” anasema Mwalimu Lubatula.

Kwa mujibu wa Mwalimu huyo, hivi sasa shule hiyo ina wanafunzi 841 lakini ina walimu tisa tu wa sayansi hali inayowalazimu kuwachanganya wanafunzi wa sayansi wa michepuo tofauti katika darasa moja.

“Walimu wa Fizikia wako watatu hivyo wanafunzi wa mchepuo wa Fizikia, Kemia na Hisabati na wale wa mchepuo wa Fizikia, Kemia na Baiolojia huwa wanaingia pamoja ili kupunguza mzigo wa ufundishaji,” anasema.

Anasema matarajio yao ni kuongeza ufaulu zaidi ili waweze kuingia katika kumi bora kwa sababu shule hiyo ni ya vipaji maalum.

Kuhusu wanafunzi Neema Paul na Lilian Hema waliofanya vizuri katika masomo ya sayansi pamoja na sanaa na lugha, anasema; “Neema alikuwa anatambua nini anapaswa kufanya na pia alikuwa ni kiongozi wa bwalo, Lilian alikuwa mtulivu, mpole na ana kipaji cha pekee,”.

Naye Mwalimu wa Taaluma kutoka Shule ya Wasichana ya Feza, Zakia Irembe, anasema wana utawala mzuri pamoja na ushirikiano kutoka kwa wanafunzi, wazazi na walimu ambao umewafanya kuishi kama familia moja.

“Wanafunzi wetu wote wanajua wajibu wao ni nini, tuna vitendea kazi vya kutosha, maktaba na maabara ya kisasa,” anasema Mwalimu Irembe.

Kuhusu shule zenye jinsia tofauti kufanya vizuri tofauti na mchanganyiko, anasema “Kabla ya kuja hapa nilishawahi kufundisha shule zenye jinsia zote na ni kweli zina changamoto nyingi kuliko zile zenye jinsia moja…lakini hiki si kigezo suala la msingi ni kuwaelimisha wanafunzi ili wajitambue zaidi pale walipo,” anasema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles