23.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Siri kifo cha Mtikila yafichuka

ChristopherMtikilaNA GUSTAPHU HAULE, PWANI NA TUNU NASSOR, DAR ES SALAAM

SIRI ya kifo cha aliyekuwa mwanasiasa nguli na  Mwenyekiti wa Chama cha Democratic (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, imeanza kufichuka.

Uchunguzi wa kitabibu umebaini kuwa, Mchungaji Mtikila alifariki dunia baada ya kuvunjika mbavu nane, huku damu nyingi ikivujia katika mfumo wa hewa, kitendo kilichosababisha ashindwe kupumua.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Jaffari Ibrahim alisema  taarifa za kuumia  kwa mwanasiasa huyo zimetokana na uchunguzi uliofanywa na jopo la madaktari katika Hospitali ya Rufaa ya Tumbi.

Kamnda Ibrahimu, alisema timu maalumu iliyoongozwa na  mkuu wa utawala wa askari wa Kikosi cha Usalama  Barabarani Makao Makuu, Johansen Kahatano, Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Pwani  na wataalamu wa sayansi ya makosa ya jinai kutoka makao makuu ya polisi akiwemo daktari wa maabara ya kisayansi inayohusu uchunguzi wa makosa ya jinai ACP Kashindye, walibaini mambo manne yaliyosababisha kutokea ajali hiyo.

 

Alisema kabla ya ajali hiyo kutokea Oktoba 2, mwaka huu, jioni Mchungaji Mtikila na wenzake waliondoka  Dr es Salaam kwenda mkoani Njombe ambapo walifika Oktoba 3 alfajiri kwa ajili ya kampeni ya chama chao.

Alisema Mchungaji Mtikila na wenzake wakiwa Njombe, wanadaiwa walipata ajali kwa kugonga magari mawili yaliyopata na kusababisha uharibifu wa gari lao.

Baada ya tatizo hilo, walishauriwa kulifanyia matengenezo  gari lao kabla ya kuendelea kulitumia.

Hata hivyo, baada ya kumaliza shughuli zao za kichama, Mchungaji  Mtikila na wenzake Oktoba 3, saa 3 usiku waliondoka Njombe kurudi D ar es Salaam.

Alisema walipofika Kijiji cha Msolwa saa 11:45 alfajiri walipata ajali  ambayo  inadaiwa chanzo chake ni mwendokasi.

Alisema baada ya timu ya Jeshi la Polisi kukagua tukio na kuwahoji majeruhi na  mashuhuda, inaonyesha wazi  chanzo chake ni mwendokasi, huku dereva wa gari hilo akikiri kosa lake, licha ya kuwapo alama ya tahadhari ya kupunguza  mwendo eneo hilo.

Alisema sababu ya pili, ni  uchovu wa dereva kutokana na safari ndefu kwa kuendesha gari usiku na mchana.

“Dereva hakupata muda wa kupumzika, kabla ya kuanza safari yao alikuwa  akishughulikia matengenezo ya gari,”alisema Kamanda.

Alisema katika tukio hilo, Mchungaji Mtikila alikuwa hakufunga mikanda .

Kutokana na  uchunguzi huo, aliwataka madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani na wale watakaokaidi hatua kali zitaendelea kuchukuliwa.

Waliojeruhiwa katika ajali hiyo ni Patrick Mgaya (57) ambaye alipata michubuko kidogo usoni na kuumia kichwani na Geoge Ponera aliyepata michubuko eneo la mabegani.

 

KUAGWA

 

Katika hatua nyingine, mwili Mchungaji Mtikila unatarajiwa kuagwa kesho nyumbani kwake Mikocheni na kusafirishwa kwenda Ludewa kwa mazishi.

Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwa marehemu Mikocheni, Dar  es Salaam jana, Msemaji wa Familia, Stanley Mtikila alisema wanategemea kuaga mwili huo, kisha kusafirisha hadi kijijini kwao Milo alikozaliwa kwa mazishi.

“Tutaanza safari ya kwenda Ludewa keshokutwa muda mfupi baada ya kuaga hapa Dar es Salaam, tunatarajia kuzika siku hiyo, itategemea na muda tutakaofika,” alisema Stanley.

Alisema kwa kuwa yeye(marehemu), ndiye alikuwa kiongozi wa kanisa, hafahamu ni kiongozi gani wa dini atakayeongoza mazishi hayo.

“Hakuna kiongozi wa Serikali wala wa dini aliyethibitisha kuongoza mazishi hayo mpaka sasa, bado tunaendelea na mawasiliano nao tutawapa taarifa kama kutakuwa na mabadiliko yoyote,” alisema Stanley.

Aliyesoma naye

Naye Anyambilile Mwakatobe alimwelezea marehemu Mchungaji Mtikila kama mtu aliyekuwa na kipawa cha pekee katika kujieleza na kujenga hoja bila kuogopa mtu yeyote.

Alisema Taifa limepoteza mtu muhimu aliyekuwa msaada wa kimwili na kiroho.

“Tumeachana na Mchungaji Mtikila Alhamisi iliyopita, baada ya kufanya ibada katika kanisa lake saa 2 usiku na yeye kuondoka Ijumaa jioni kwenda Njombe kumnadi mgombea ubunge jimboni humo,” alisema Mwakatobe.

Alisema walikutana na marehemu mwaka 1966 katika Shule ya Sekondari ya Malangali iliyopo Iringa na kuwa marafiki.

“Tulikutana na Mchungaji tukiwa na umri wa miaka 16, tukiwa na Profesa Mark Mwandosya, nakumbuka aliwahi kutengeneza kundi la kuzuia wizi shuleni hapo,” alisema Mwakatobe.

Mchungaji Mtikila alifariki dunia juzi katika eneo la Msolwa wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani,baada ya gari waliokua wakisafiria lenye namba za usajili T 189 AGM aina ya Toyota Corola kuacha njia na kupinduka.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles