23.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Sintofahamu Z’bar

DSC_7165*CCM yajipanga kurudia uchaguzi

*CUF wagoma, wataka Maalim atangazwe

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

HALI ya sintofahamu sasa imeikumba Zanzibar, baada ya Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi iliyokutana jana mjini Unguja, kuweka mikakati ya kujiandaa na uchaguzi wa marudio visiwani humo.

Wakati CCM ikiendelea na mipango hiyo, wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF), wamekuwa wakisubiri kutangazwa kwa aliyekuwa mgombea urais wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad kama mshindi halali katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu.

Kikao hicho cha CCM kimefanyika miezi miwili tangu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, alipotangaza kufuta matokeo ya uchaguzi huo Oktoba 28, mwaka huu.

Kikao hicho kilichofanyika chini ya Mwenyekiti wake Rais wa Zinzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, ambapo pamoja na mambo mengine wajumbe walitumia siku ya jana kujadili na kutafakari hatima ya visiwa hivyo.

Chanzo cha kuaminika kiliambia MTANZANIA jana kuwa, wajumbe wa kikao hicho walichambua zaidi namna watakavyojipanga katika marudio ya uchaguzi visiwani humo.

“Kwanza tumekaa kwa muda mrefu sana leo (jana), kikao kilianza saa 4 asubuhi hadi saa 12 jioni  na mjadala mkubwa ulikuwa ni maandalizi kwa ajili ya uchaguzi wa marudio.

“Pamoja na kujadili hili bado hatujajua lini uchaguzi huo wa marudio utatangazwa, lakini pia tumejadili kwa kina kuhusu udhaifu wetu katika uchaguzi wa awali hasa wapi tulipokosea na nini cha kufanya,” kilisema chanzo hicho.

Kikao hicho kimefanyika siku moja baada ya Rais Dk. John Magufuli kukutana na Rais wa Zanzibar, Ali Mohamed Shein Ikulu, Dar es Salaam kwa ajili ya mazungumzo ya mwenendo wa kisiasa visiwani humo.

Mazungumzo hayo yalifanyika juzi, ambapo taarifa ya kukutana kwa viongozi hao ilitolewa kwa vyombo vya habari jana jioni na Kaimu Mkurugenzi Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa.

Taarifa hiyo ilieleza baada ya mazungumzo ya viongozi hao, Rais Shein ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, alieleza kuwa lengo la mazungumzo yao ilikuwa ni kumpa taarifa Rais Magufuli kuhusu hali ya mazungumzo ya kutafuta mwafaka wa kisiasa Zanzibar.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa Rais Shein alisema mazungumzo yanaendelea chini ya Kamati Maalumu ya kutafuta suluhu ambayo ipo chini ya uenyekiti wake.

Kamati hiyo inaundwa na Shein, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd na Rais mstaafu wa awamu ya pili Alhaji Ali Hassan Mwinyi.

Wengine ni Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, Rais mstaafu wa awamu ya sita wa Zanzibar Dk. Amani Abeid Karume na Rais mstaafu wa awamu ya tano wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour.

Dk. Shein alisema amemtaarifu Rais Magufuli kuwa kamati yake ilianza mazungumzo Novemba 9, 2015 na hadi sasa bado inaendelea na kazi yake.

“Nimekuja kumpa taarifa Rais Magufuli kuhusu maendeleo ya mazungumzo yetu ili aweze kujua kinachoendelea akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo Zanzibar ni sehemu yake, na sisi ni jukumu letu kumpa taarifa,” alisema Dk. Shein.

Kabla ya kukutana na Rais Shein, tayari Desemba 21, mwaka huu Rais Magufuli alikutana na Maalim Seif, Ikulu Dar es Salaam na kuzungumzia mgogoro huo wa Zanzibar.

Mazungumzo haya yanaendelea huku mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar ukitajwa kuwa na athari mbaya kwa Tanzania kwa kuisababisha kukosa zaidi ya Sh trilioni 1 zilizokuwa zitolewe na Serikali ya Marekani, ikiwa ni sehemu ya fedha za msaada wa Mfuko wa Changamoto za Milenia (MCC).

Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), ilitangaza kufuta matokeo ya uchaguzi mkuu visiwani humo ambapo Serikali ya Uingereza na ile ya Ireland Kaskazini zilipinga uamuzi huo kwa maelezo kuwa hazioni sababu ya kufutwa huko baada ya taarifa ya waangalizi wa kimataifa kueleza kufurahishwa na mwenendo wa uchaguzi.

Hatua za kutatua mgogoro huo zilianza mwezi Novemba, siku chache kabla ya Kikwete kukabidhi madaraka kwa Rais Magufuli.

Kikwete alikutana na Maalim Seif Ikulu Magogoni, Dar es Salaam na kufanya naye mazungumzo kwa takribani saa moja kuhusu mgogoro huo, hususan hali ya usalama visiwani ilivyoonekana kuwa tete.

CUF wapinga

Novemba 4, mwaka huu Maalim Seif alisema CUF inaendelea kutafuta haki ya Wazanzibari ya kutaka Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kuendelea kutangaza matokeo ya uchaguzi ili mshindi ajulikane na hatimaye kuapishwa.

Aliyasema hayo wakati akizungumza na wafuasi wa chama hicho katika makao makuu ya CUF Mtendeni, baada ya kurudi safari yake ya kuonana na rais mstaafu  wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, Ikulu, jijini Dar es Salaam.

Aliwaambia wanachama hao kuwa hakuna kurudi nyuma katika kudai haki yao kwa njia ya amani na utulivu ili matokeo yatangazwe na mshindi wa urais ajulikane.

“Niwahakikishieni vijana na wanachama wa CUF kuwa hakuna kurudi nyuma, tunaendelea kudai haki yetu na tunashukuru dunia nzima inatuunga mkono kwa hili,”alisema Maalim Seif, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK).

Alisema kuwa wapinzani wao, CCM mpango wao ni kutaka kuendelea kuwa katika madaraka wakijua kuwa muda wa Dk.  Ali Mohammed Shein wa kukaa madarakani umekwisha, lakini wanang’ang’ania aendelee kinyume cha Katiba.

Alisema kuwa hakuna dawa yoyote ya kumaliza mgogoro uliopo Zanzibar  isipokuwa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec) kuendelea kutoa matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka huu ili mshindi ajulikane na kuapishwa.

“Wanaosema kuwa uchaguzi urejewe waachieni wenyewe, sisi katika CUF hakuna msamiati huo kwa sasa kurejea uchaguzi, huo ndio msimamo wetu,” alisisitiza Maalim Seif.

Novemba 22, mwaka huu wabunge kutoka Chama cha Wananchi (CUF), waliitaka ZEC, iendelee na mchakato wa kumtangaza mshindi halali wa urais katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles