24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Simu za mkononi janga jipya ajali za barabarani

Na VERONICA ROMWALD

 – ALIYEKUWA DODOMA

NDANI ya kila sekunde 24 duniani mtu mmoja hupoteza maisha kwa ajali ya barabarani. Vifo vitokanavyo na ajali za barabarani katika nchi zilizopo Bara la Afrika ni mara tatu zaidi ya vile vinavyotokea Bara la Ulaya. 

Shirika la Afya Duniani (WHO) linakadiria idadi ya vifo vitokanavyo na ajali kila mwaka vimeongezeka kutoka watu milioni 1.24 ilivyokuwa mwaka 2016 na kufikia watu milioni 1.35 mwaka 2018.

Hiyo ni kulingana na ripoti ya Hali ya Usalama Barabarani Duniani, iliyotolewa hivi karibuni na shirika hilo ambayo inasisitiza kuna vifo 27 kwa kila watu 1000.

VYANZO VYA AJALI

Ripoti za nchi mbalimbali na WHO za hali ya usalama barabara, zinataja moja kwa moja visababishi vikuu vitano vya ajali duniani ni pamoja na makosa ya kibinadamu, sababu za kimazingira, ubovu wa miundombinu na vyombo vya moto.

Hata hivyo katika miaka ya hivi karibuni matumizi ya simu za mkononi, nayo yanatajwa kuwa kisababishi kipya cha ajali za barabarani.

“Nakubaliana na jambo hilo, kwani nimeshuhudia mara kadhaa ajali za barabarani ambazo naweza kusema chanzo chake ni simu za mkononi.

“Kwa mfano hapa katika eneo la Kisasa (Dodoma), jinsi barabara ilivyo finyu, eneo la kivuko cha waenda kwa miguu kimeweka sehemu ambayo kwa namna moja au nyingine ni hatari.

“Lakini pamoja na hayo, niliwahi kushuhudia kijana mmoja akivuka huku akiwa anatumia simu yake ya kiganjani, aligongwa na gari na kufariki wakati akikimbizwa hospitalini kwa matibabu.

“Alikuwa anavuka huku akiendelea ‘ku-chart’ kwa kutumia simu yake ya smart (mfuto), tukio lile lilinisikitisha mno,” anasema Dickson Malema mkazi wa Dodoma.

RIPOTI YA TCRA

Matumizi ya simu za mkononi yanazidi kuongezeka si tu hapa nchini bali duniani kote, changamoto iliyopo sasa ni kwamba zinatajwa kuwa miongoni mwa visababishi vya ajali za barabarani.

Ripoti ya robo ya nne ya mwaka inayoishia Desemba 2017 ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), inaelezwa idadi ya wamiliki wa simu za mkononi nchini imeongezeka maradufu.

Kulingana na ripoti hiyo idadi ya watumiaji wa simu za mkononi imeongezeka kutoka milioni 27.62 mwaka 2012 kufikia milioni 40 kutoka milioni, mwaka huo.

Ripoti hiyo inaeleza pia kuna ongezeko kubwa la watumiaji wa huduma ya intaneti kufikia asilimia 45 ya watanzania ambayo ni sawa na watu milioni 23 ukilinganisha na watanzania milioni 7.52 ambao ni sawa na asilimia 12 tu ya watanzania mwaka 2012.

Aidha, kuna ongezeko kubwa la watumiaji wa intaneti mwaka hadi mwaka, mwaka 2012 ya watumiaji wa intaneti ilikuwa ni milioni 7.52 sawa na asilimia 17 wakati mwaka 2013 waliongezeka kufikia milioni 9.31 sawa na asilimia 21.

Mwaka  2014 watumiaji walifikia milioni 12.17 sawa na asilimia 29, mwaka 2015 watumiaji waliongezeka kufikia milioni 17.62 sawa na asilimia 34 na mwaka 2016 idadi ilifika milioni 19.86 sawa na asilimia 40.

TAFITI ZA KIDUNIA

Nchini Marekani hivi sasa kuna ongezeko kubwa la vifo vya watembea kwa miguu kutokana na ajali za barabarani, simu za mkononi zikitajwa kuwa chanzo.

Inaelezwa watu hupata ajali kutokana na kutumia simu zao wakati wakitembea pembezoni au wakivuka barabara na huku madereva nao husababisha ajali kutokana na matumizi ya simu zao wakiwa wanaendesha.

Baraza linalohusika na masuala ya usalama barabarani nchini humo inakadiria mwaka 2016, wasafiri 6,000 wanaotembea kwa miguu walifariki dunia ikiwa ndiyo idadi kubwa zaidi katika kipindi cha miaka 20.

Mtandao wa BBC Swahili unaripoti kwamba katika kipindi cha miaka sita iliyopita vifo vimeongezeka nchini humo mara nne zaidi.

Ripoti ya Baraza hilo, inaeleza vifo kadhaa vimechangiwa na matumizi ya simu za mkononi aina ya ‘smart’.

Sababu zingine zinazotajwa ni pamoja na ongezeko la wamiliki wa magari kufuatia kuboreka kwa uchumi, kushuka kwa bei ya petroli na watu wengi kutembea kama njia ya kufanya mazoezi.

Pombe nayo imelaumiwa kwa kuchangia asilimia 34 ya watembea kwa miguu na asilimia 15 ya madereva walihusika kwenye ajali wakiwa wamelewa.

Ripoti hiyo imetokana na takwimu kutoka majibu yote nchini humo, zilizokusanywa kwa kipindi cha miezi sita ya kwanza 2016.

Mtandao wa Edgarsnyder.com unanukuu ripoti ya Baraza la Usalama la Taifa nchini Marekani kwamba matumizi ya simu ya mkononi barabarani husababisha ajali zipatazo milioni 1.6 kila mwaka, watu 390,000 hujeruhiwa.

Ajali moja kati ya nne nchini humo husababishwa na madereva wanao-chart wakiwa wanaendesha magari yao, inaelezwa matumizi ya simu barabarani huongeza uwezekano wa dereva kusababisha ajali mara sita zaidi, kwani ku-chart huhamisha mawazo ya mhusika.

Mtandao huo unaeleza madereva wapatao 660,000 hutumia simu za mkononi wakiwa wanaendesha barabarani, kusoma ujumbe mfupi wa maandishi, barua pepe, simu au maombi mengine ya simu, hivyo kuongeza hatari ya uwezekano wa kusababisha ajali.

Mtandao wa The Times nchini India unaeleza kuwa mwaka 2016 ajali za barabarani zilisababisha vifo vya zaidi ya watu 2,138, kulingana na ripoti ya huduma ya usafiri nchini humo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watu 17 walikufa kila saa katika ajali za barabara.

Kulingana na mtandao huo wapo madereva ambao hujipiga ‘selfies’ wakati wakiwa mbele ya usukuni wakiendesha magari yao.

HALI ILIVYO NCHINI  

Hivi karibuni MTANZANIA likiwa jijini Dodoma lilifanya mahojiano na Kamanda wa Jeshi la Polisi Dodoma, Gilles Muroto, ambaye anakiri suala hilo sasa ni changamoto na anabainisha jinsi walivyojipanga kuikabili.

“Matumizi ya simu za mkononi barabarani hasa kwa watembea kwa miguu na madereva wanapokuwa barabarani kweli kabisa kwamba sasa ni miongoni mwa visababishi vya ajali.

“Ku-chart’ kunawaponza wengi, unakuta mtu anatembea barabarani, anavuka huku akiwa anaendelea ku-chart’ au unakuta ni dereva anaendesha na wakati huo huo ana-chart, matokeo yake ni ajali,”anasema Kamanda wa Jeshi la Polisi Dodoma, Gilles Muroto.

Kamanda Muroto anasema bado jamii inahitaji kupatiwa elimu na kwamba Jeshi hilo kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani, linaendelea kuhakikisha linasimamia sheria ipasavyo dhidi ya wanaozivunja.

“Lazima wazitii bila shuruti, Dodoma ni mji Mkuu na Makao Makuu ya Nchi, viongozi wengi wa serikali wapo hapa akiwamo Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Waziri wa Mambo ya Ndani, wakuu mbalimbali wa nchi.

“Shughuli mbalimbali ya kitaifa zinafanyika hapa, tunahakikisha tunaimarisha usalama hadi barabarani, wanakuja salama na kuondoka salama, hakuna ajali, tunajiimarisha katika kila eneo kulingana na maelekezo tunayopewa na Mkuu wa Jeshi (IGP), Simon Sirro,”anasisitiza.

RIPOTI YA WHO

Ripoti ya Masuala ya Usalama Barabarani iliyotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) 2018, inaeleza Tanzania haijaweka sheria madhubuti kudhibiti matumizi ya simu za mkononi barabarani.

Tofauti na nchi zingine za Afrika Mashariki hususan Kenya na Uganda ambazo zenyewe tayari zimetunga sheria ili kudhibiti ajali za barabarani.

MAREKEBISHO MUHIMU

“Kuna haja ya kufanya marekebisho (mabadiliko) ya Sheria ya Usalama Barabarani inayotumika hivi sasa nchini ambayo ilitungwa tangu mwaka 1973.

“Kimsingi wakati huo hata matumizi ya simu za mkononi hayakuwapo kwa kiwango kikubwa kama tunavyoshuhudia hivi sasa,” anasema Mjumbe wa Kamati Maalum ya Kitaifa ya Mabadiliko ya Sheria ya Usalama Barabarani, Alferia Nchimbi.

Nchimbi anasema ni wazi ripoti hiyo ya WHO inayoeleza pia idadi ya vifo vitokanavyo na ajali duniani imezidi kuongezeka.

 “Ripoti hiyo ilihusisha nchi zote ambazo zipo ndani ya Jumuiya ya Umoja wa Mataifa (UN), Tanzania ikiwamo, dunia iliweka malengo maalumu kwamba hadi kufikia mwaka 2020 angalau vifo na majeruhi wa ajali vipungue kwa kufikia milioni 50.

“Kwa hiyo ripoti ililenga kuangazia katika kipindi cha muongo mmoja (2011-2020), je dunia inaweza kufikia malengo hayo iliyojiwekea, kulingana na maeneo yaliyoangaziwa, ripoti inabainisha kwamba itakuwa vigumu malengo yale kufikiwa.

“Kwa sababu lengo ni kupunguza idadi lakini utaona vifo vitokanavyo na ajali vimeongezeka kutoka milioni 1.2 hadi milioni 1.5.

“Hivyo tunaangazia sasa…tunapojiandaa kwenda kwenye mkutano wa mwaka 2020 ili kutathimini malengo tuliyojiwekea ndani ya muongo huo mmoja, ni mikakati gani tuweke kukabili hali hiyo au pengine iende sambamba na ule Mpango wa Maendeleo Endelevu ya Dunia (SDGs).

“Lakini kwa upande wa Tanzania, ripoti inaonesha hatujafanya vibaya sana, tupo kwenye mwelekeo mzuri kwa maana kwamba kuna mambo yalipendekezwa kuundwa, yameundwa.

“Kwa mfano, Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, ambalo kazi yake ni kuratibu masuala ya usalama barabarani, ndani ya ripoti imeelezwa tayari limeundwa, lakini kuna maeneo mengine ambayo bado tunahitaji kufanya mabadiliko ya sheria.

“Kwa mfano ajali zinazotokana na ulevi, ripoti inaeleza bado ni tatizo, hivyo japo inatuonesha tuna mwelekeo mzuri lakini hatupaswi kulala kwani kuna mambo makubwa mbele yetu ambayo lazima tuyafanyie kazi.

“Lazima tukaze ‘buti’ kwa mfano juu ya suala la marekebisho ya sheria hii ya mwaka 1973 ambayo tunatarajia itawasilishwa bungeni, Februari, mwaka huu.

“Mambo mengi yatarekebishika kwa mfano ufungaji wa mikanda, uvaaji wa kofia ngumu, vizuizi vya watoto wadogo, uendeshaji hatari wa vyombo vya usalama, unywaji wa pombe na kuendesha.

“Mambo haya yametamkwa kwenye sheria lakini hayajatiliwa mkazo, kwa mfano suala la kufunga mkanda limetajwa lakini imeelezwa ni kwa wanaokaa siti za mbele pekee, kofia ngumu kwa dereva wa bodaboda pekee haijatamka upande wa abiria.

“Lazima tuendelee kupaza sauti ili marekebisho ya sheria yafanyike haraka, watu wanakufa, tumetoa mapendekezo lakini lazima taratibu zifuatwe hasa za kibunge, ni kweli awali wabunge wetu walikuwa hawajalipa msukumo sasa ‘wameamka’.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles