23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Simbachawene amrithi Lugola, Zungu ndani

Mwandishi wetu – Dar es Salaam

RAIS Dk. John Magufuli amefanya mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri kwa kumteua Mbunge wa Ilala, Mussa Azan Zungu kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira na George Simbachawene kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, alisema Simbachawene anaziba nafasi ya Lugola ambaye uteuzi wake umetenguliwa, huku Zungu akiziba nafasi ya Simbachawene ambaye amehamishwa Wizara ya Mambo ya Ndani.

Uteuzi wa Zungu ulitangazwa ikiwa ni saa chache tangu ashiriki hafla ya uzinduzi wa nyumba za askari magereza Ukonga akiwa kama Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, ambapo kwenye hotuba yake alisema huu ni mwaka wa uchaguzi na hana wasiwasi kuwa Rais Magufuli atapita tena.

UTEUZI WA MABALOZI

Balozi Kijazi alisema Rais pia ameteua mabalozi watatu ambao wataiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali, baada ya mabalozi katika vituo hivyo aidha kumaliza muda wao au kufikisha umri wa kustaafu.

Alisema walioteuliwa ni aliyekuwa Katibu Mkuu wa Mambo ya Ndani, Meja Jenerali Jacob Kingu ambaye alijiuzulu juzi, na John Simbachawene aliyekuwa Ofisi ya Rais, Ikulu.

Balozi Kijazi alisema Rais pia amemteua aliyekuwa Kamishna Jenerali wa Magereza, Faustine Kasike kuwa balozi ambaye sasa nafasi yake itajazwa baadaye na kwamba vituo vyao vitatangazwa badaye.

“Rais pia amewaongezea muda wa miaka miwili mabalozi saba ambao wanaiwakilisha nchi katika nchi mbalimbali, ambao muda wao wa uwakilishi umekwisha,” alisema Balozi Kijazi.

Alisema mabalozi walioongezewa muda ni Balozi George Madafa (Italia), Luteni Jenerali Paul Mwela (DRC), Job Masima (Israel), Emmanuel Nchimbi (Brazil), Asharose Migiro (Uingereza), Bebedict Mashiba (Malawi) na Sylvester Mabumba (Comoro).

Balozi Kijazi alisema Rais pia ametengua uteuzi wa Kamishna Jenerali wa Zimamoto na Uokoaji, Thobias Andengenye na nafasi yake itajazwa baadaye.

Alisema pamoja na kutengua uteuzi huo, Rais Magufuli pia ameagiza Takukuru wafanye uchunguzi wa haraka kuhusiana na mkataba uliosainiwa kati ya kampuni kutoka nje ya nchi na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ambao hauna masilahi kwa nchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles