27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

SIMBA YAPIGA MWINGINE TENA

NA ASHA KIGUNDULA-DAR ES SALAAM

SIMBA imeendelea kutakata msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya jana kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya timu ya Manispaa ya Kinondoni ya  jijini Dar es Salaam(KMC), mchezo uliopigwa Uwanja wa Uhuru.

Hata hivyo, Simba ililazimika kusubiri hadi kipindi cha pili ili kuzitikisa nyavu za KMC.

Mshambuliaji, Deo Kanda ndiye aliyeanza kulitia ‘nuksi’ lango la KMC, baada ya kuifungia Simba bao la kuongoza dakika ya 46 kwa mkwaju wa mguu wa kulia, akimalizia krosi  ya upande wa kulia iliyochongwa na Hassan Dilunga.

Beki Gerson Fraga aliifungia Simba bao la pili dakika ya tisini, baada ya kuunganisha kwa mguu wa kushoto pande la Francis Kahata.

Kipindi cha kwanza

Dakika 45 za kipindi cha kwanza, timu hizo zilikuwa zikishambuliana kwa zamu ingawa Simba ilionekana kucheza kwa tahadhari, ambapo idadi kubwa ya wachezaji wake walikuwa wakishuka chini kulinda lango lao pale timu ilipokuwa haina mpira.

Kwa upande wa KMC, ilionekana kumiliki zaidi mpira, lakini udhaifu ulionekana pale ilipoingia robo tatu ya uwanja, kwani washambuliaji wake Boniface Maganga na Salum Kabunda walionekana kukosa maarifa ya kuipangua ngome ya Simba.

Washambuliaji wa Simba, Meddie Kagere na Kanda mara kadhaa nao walipata nafasi nzuri ambazo kama wangekuwa makini wangeuweka mpira wavuni lakini walionekana kukosa utulivu na kufanya timu hizo ziende mapumziko zikiwa nguvu sawa.

Kipindi cha pili

 Simba iliingia uwanjani na mpango kazi mwingine wa kuongeza kasi ya mashambulizi langoni mwa wapinzani wao KMC.

Kasi ya Simba iliwafanya wachezaji wa KMC kukosa hali ya kujiamini na hivyo kupoteza umiliki wa mpira.

Mpango huo ulizaa matunda baada ya mmoja wa mabeki wa KMC kushindwa kuudhibiti mpira wa krosi ya Dilunga na kuumkuta Kanda aliyeukwamisha wavuni. 

Dakika ya 50, mwamuzi wa mchezo huo Mbaraka Rashid alimwonyesha kadi ya njano  Maganga kwa kuonyesha mchezo usio wa kiungwana.

Simba wakati huu iliendelea kuutawala mchezo,  dakika ya 54,  kipa wa KMC  ambaye jana alikuwa kikwazo kwa Simba kupata mabao mengi alipangua mkwaju wa Kanda wakiwa wanaangaliana na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Ili kuongeza ufanisi, KMC ilifanya mabadiliko dakika ya 61, alitoka Maganga na kuingia Serge Allen wakati huo huo Simba alitoka Ibrahim Ajib na kuingia Clatous Chama.

Dakika ya 68, Simba ilifanya mabadiliko mengine, alitoka Dilunga na kuingia Kahata.

Nayo KMC ilifanya mabadiliko dakika ya 81, alitoka Kabunda na kuingia Rehani Kibindu.

Pamoja na mabadiliko hayo ya kila upande hakuna kilichobadilika, badala yake dakika 90 za patashika hiyo zilikamilika kwa Simba kuchomoza na ushindi wa mabao 2-0.

Kwa ushindi huo, Simba ilifikisha pointi 31 na kuendelea kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo, ikishuka dimbani mara 12, ikishinda michezo 10, sare moja na kupoteza mchezo mmoja.

KMC ilisalia nafasi ya 17 miongoni mwa timu 20 zinazoshiriki Ligi Kuu msimu huu, ikikusanya pointi tisa, baada ya kushuka dimbani mara 13, ikishinda michezo miwili, sare tatu na kuchapwa mara nane.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles