SIMBA YAJIANDALIA SHEREHE U/TAIFA

0
194

Na MOHAMED KASSARA -DAR ES SALAAM

KOCHA msaidizi wa Simba, Masoud Djuma, ametamba kuwa kikosi chake kitaichapa Ruvu Shooting kesho ili kuzindua kampeni zao za mzunguko wa pili kwa shangwe.

Simba itakuwa mwenyeji wa Ruvu Shooting katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa kesho Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Simba inaongoza msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 35 baada ya kucheza michezo 15, ikishinda michezo 10 na kutoka sare mitano, huku ikiwa haijapoteza mchezo.

Wekundu hao wa Msimbazi wanajivunia kumaliza duru ya kwanza kileleni kwa tofauti ya pointi saba dhidi ya mahasimu wao, Yanga walioko nafasi ya tatu wakiwa na pointi 28 na Azam iliyojikita nafasi ya pili ikiwa na pointi 30.

Wekundu hao walihitimisha mzunguko wa kwanza kwa kishindo baada ya kuizamisha Majimaji FC mabao 4-0, kwenye Uwanja wa Taifa.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Djuma, alisema kikosi hicho kinaendelea kujifua vikali kuhakikisha kinaendelea kupata matokeo mazuri na kujiweka katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa huo msimu huu.

Alisema baada ya kutolewa kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam, timu hiyo inaelekeza nguvu zake katika kuwania ubingwa pamoja na kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa.

“Kikosi chetu kinaendelea kujifua vikali kuhakikisha lengo letu la kutwaa ubingwa msimu huu linatimia.

“Tumepata muda mzuri wa kujiandaa na michezo yetu ya Ligi Kuu na michuano ya kimataifa, tumepanga kuutumia vema muda huu kuweka mikakati ya kupata ushindi dhidi ya Ruvu Shooting ili kuanza mzunguko wa pili kwa kishindo,” alisema Djuma.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here