23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Simba Mabadiliko

SIMBANa ADAM MKWEPU-DAR ES SALAAM

MKUTANO Mkuu wa wanachama wa klabu ya soka ya Simba, umeridhia mabadiliko mapya ya kuboresha mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo kutoka kwenye mfumo wa kadi hadi kwenye hisa, wakati ikisubiri tamko rasmi kutoka kwa Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo.

Katika mabadiliko hayo, wanachama wa Simba wapatao 700 kati ya 860 halali waliotakiwa kuhudhuria mkutano huo, walikubaliana klabu hiyo kuendeshwa kwa umiliki wa hisa na kubadili mfumo mzima wa uongozi wake.

Maamuzi ya wanachama hao yamesafisha njia kwa mfanyabiashara maarufu nchini mwenye mapenzi makubwa na klabu hiyo, Mohamed Dewji ‘Mo’, anayedaiwa  kutaka kumiliki hisa za asilimia 51 za klabu hiyo ili kuwa mmiliki halali kwa kuwekeza Sh Bilioni 20.

Akiwakilisha ripoti ya klabu hiyo ya msimu uliopita katika mkutano huo uliofanyika ukumbi wa Bwalo la Maafisa wa Polisi uliopo Oysterbay, Dar es Salaam, Rais wa klabu hiyo, Evans Aveva, alisema licha ya kuwepo kwa wafadhili mbalimbali kama Azam, Vodacom, TBL na mapato ya viingilio katika mchezo, fedha hizo hazitoshi hivyo kufanya uendeshaji wa klabu hiyo kuwa mgumu na kuhitaji njia mbadala ya kuongeza mapato hayo.

“Katika ripoti yangu nimeeleza kwamba ili kumpata mchezaji mmoja wa kimataifa, mwenye kiwango bora ni lazima atugharimu kuanzia dola 30,000 (Sh milioni 65 za kitanzania) na mshahara wa dola 5000 (Sh milioni 10), ambayo ni gharama sana.

“Tumekuwa na malengo makubwa ndani ya klabu yetu, ili yaweze kufanikiwa lazima tuwe na fedha za kutosha,” alisema Aveva.

Aveva alisema katika kutafuta njia mbadala ya kuendesha klabu hiyo, ilimlazimu kuunda kamati ya kuchukua maoni ya wanachama wake.

“Niliunda kamati ambayo ilifanya kazi ndani ya siku 45 kwa kuwahoji wanachama 23, ambao walipendekeza klabu hiyo kuendeshwa kwa umiliki wa hisa na mabadiliko ya mfumo wa uongozi.

“Hata hivyo, kamati hiyo ilipendekeza wapewe muda, ili kuja na ripoti ambayo itakuja na mabadiliko,” alisema Aveva.

Aveva alikiri kuwa ni muumini wa mabadiliko ya uongozi ndani ya klabu hiyo kutokana na hali ya uchumi ilivyo kwa klabu kushindwa kufanikisha baadhi ya mambo ya maendeleo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya udhamini wa klabu hiyo, Ramesh Patel, alisema hawana tatizo kwa kumpa Mo umiliki wa klabu hiyo, lakini bado mfanyabiashara huyo hajawasilisha barua rasmi ya kuomba kufanya hivyo.

“Mabadiliko lazima yawepo lakini hayawezi kutokea katika magazeti pekee, lazima Mo aje kuonana na uongozi ili kufanya mazungumzo na kufikia mwafaka.

“Katika kufanikisha hilo, kuna mambo mengi ya kuzingatiwa likiwamo la kubadili Katiba, ambapo linahitaji muda wa ziada,” alisema Patel.

Aidha, mkutano huo ulimalizika kwa wanachama na viongozi kukubaliana kauli moja ya mabadiliko ndani ya klabu hiyo.

Aveva alifunga Mkutano huo kwa kusema: “Uongozi umekubali kwa dhati mabadiliko yanayotakiwa na wanachama, hivyo suala hilo tutaliachia Kamati ya Utendaji ya klabu ili kuamua na kuja na  mapendekezo ya nini kifanyike katika mabadiliko hayo”.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles