31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Simba kumshtaki Mwakalebela TFF

WINFRIDA MTOI – DAR ES SALAAM

SAKATA la kiungo wa Simba , Clatous Chama, kudaiwa kufanya mazungumzo ya kutaka kusajiliwa na Yanga, limechukua  sura mpya baada ya uongozi wa Wekundu wa Msimbazi kupanga kumshtaki Makamu Mwenyekiti wa Wanajangwani hao, Fredrick Mwakalebela.

Simba inakusudia kuchukua uamuzi huo kwa kile inachodai bado ina mkataba na Chama wa zaidi ya miezi sita.

Kulingana na kanuni za usajili za Shirikisho la Soka la Kimataifa(Fifa) na zile na Shirikisho la Soka Tanzania(TFF), klabu itakuwa imefanya kosa endapo itazungumza na mchezaji wa klabu nyingine mwenye mkataba wa zaidi ya miezi sita.

Lakini klabu au mchezaji atakuwa huru kuzungumza na klabu nyingine kuhusu usajili ikiwa mkataba wake umesalia miezi sita.

 Chama amekuwa gumzo baada ya ya Mwakalebela kusikika kupitia chombo kimoja cha habari akisema kuwa wamefanya mazungumzo na mchezaji huyo ili atue Jangwani, kwakua mkataba wake na Simba ni chini ya miezi sita.

Kitendo hicho kiliwaibua viongozi wa Simba na kuweka wazi kusudio lao la ku
kumfikisha Mwakalebela kwenye vyombo vya sheria vinavyohusika na soka kikiwamo TFF.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara, alisema jana kuwa, mkataba wa nyota wao huyo unaomalizika Julai mwakani, hivyo timu yeyote inayomwitaji inapaswa kuwasilisha maombi rasmi kwa klabu yao na si vinginevyo.

“Chama ana mkataba hilo halina ubishi na TFF na vyombo vingine vinajua, nashangaa kiongozi mkubwa mwenye uzoefu wa soka kama Mwakalebela anazungumza vitu ambavyo hana ukakika navyo.

“Hata mtu akienda TFF leo hii, mkataba wa Chama uko pale ataangalia na kujiridhisha, anamaliza mkataba Julai 2021, iko wazo kabisa,” alisema Manara.

Manara  alisema wanatarajia kuwasilisha barua TFF, ili hatua za kisheria zichukuliwe ili kukomesha vitendo kama hivyo.

Manara alisema kanuni za usajili wa katika mashirikisho yote ya soka, zinazuia kuzungumza na mchezaji akiwa na mkataba wa zaidi ya miezi sita na klabu yake, hivyo wanashangazwa na kitendo cha bosi hiyo wa Yanga.

“Tumemsikia mwenyewe kasema wamezungumza na mchezaji, hiyo pekee inaipa hasara Yanga kwa sababu ni limezungumzwa na kiongozi mkubwa ambaye ni makamu mwenyekiti.

“Angezungumza mtu wa mtaani au mwingine asiye kiongozi tungeichukulia poa, tutakachokifanya ni zaidi ya kile kilichotokea kwa Kessy(Hassan), baada ya kumvalisha jezi na kumpeleka Uturuki wakati alikuwa bado ana mkataba na sisi, ” alisema Manara.

Aliongeza kwa kusema, barua ya malalamiko yao iko tayari hivyo wakati wowote wakaifikisha TFF, lengo likiwa kutoa funzo kwa viongozi  wa soka wasiofuata kanuni.

Lakini ikionekana kama amenusa  hatari ya kukabiliwa na adhabu, saa chache baadaye ya Manara kuweka wazi kusudio lao, Mwakalebela alijitokeza hadharaji na kuwaomba radhi wapenzi wa soka, akisema kauli yake ilikuwa masihara na si  ya kuichukuliwa kwa umakini, akisema alifanya hivyo kama wenzao Simba walivyofanya kwa kiungo wao Papy Tshishimbi.

“Napenda kuchukua nafasi hii kuelezea suala lilijitokeza la kumzungumzia mchezaji wa Simba, Chama, inaonekana Simba  hawajalipokea vizuri, lakini ukweli nilikua nafanya utani kama walivyokuwa wanatufanyia wao kwa Tshishimbi.

“ Naomba msamaha kwa Simba na  wapenzi wa Yanga, nimefanya vile nikijua ni utani wa jadi tuliokuwa nao kwa sababu, hapa katikati tumekuwa tukitaniana kuchukuliana wachezaji, naomba radhi pia kwa TFF, sijazungumza na mchezaji huyo.

“Nina ahidi jambo hili halitajitokeza tena, nadhani utani nilioufanya ulivuka mipaka, naomba jambo hili limalizike na tuendelee na urafiki wetu kama kawaida,” alisema Mwakalebela.

Mwakalebela ambaye aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa TFF, alikiri kuwa kama kiongozi mwenye weledi, akimhitaji mchezaji huyo atalazimika kuzungumza na uongozi wa Simba kwanza.

Katika hatua nyingine, Manara, alitolea ufafanuzi kuhusu suala la bilioni 20 zinazopaswa kuingizwa na mwekezaji wa Simba, Mohamed Dewji ‘Mo’, katika kaunti ya Kampuni ya Simba (Simba Sports Club LTD), ambazo zimekuwa na utata.

“Ni kweli fedha hazijaingizwa kwasababu ya Kampuni ya Simba ambayo asilimia 48 inamilikiwa na Mohamed Dewj na familia yake na asilimia 51 wanachana wa Simba haijaanza shughuli zake kutokana na kutokamilika kwa baadhi ya mambo, lakini niwatoe hofu Wanasimba kila kitu kitakwenda sawa,”alisema

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles