24.4 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

SIMBA KUGOMEA MECHI YA WATANI

simba*Yajipanga kuleta waamuzi kutoka nje

*Wambura asema wanapingana na kanuni

ADAM MKWEPU NA MOHAMED KASSARA DAR ES SALAAM

BAADA ya kuchoshwa na uamuzi mbovu katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara, hasa mchezo wa Watani wa Jadi Simba na Yanga, vinara wa ligi hiyo Simba wameeleza kuwa hawatapeleka timu uwanjani kucheza mchezo wowote dhidi ya Yanga, ikiwa waamuzi watakaochezesha watatoka nchini.

Timu hiyo imeenda mbali zaidi na kueleza kuwa wataanza kugharamia waamuzi kutoka nje ya nchi wanaotambuliwa na Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) kuchezesha mechi hiyo kubwa katika mzunguko wa pili utakaoanza Desemba 17.

Uamuzi huo wa Simba si tu kuonyesha jeuri ya fedha, bali ni kuchoshwa na waamuzi hao ambao wanashindwa kutafsiri sheria 17 za mpira ambazo hutumika ulimwenguni kote na kuonekana kuwabeba wapinzani wao.

Simba na Yanga kwa mara ya mwisho zimekutana Oktoba mosi katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, katika mchezo uliokuwa wa vurugu uliosimamiwa na mwamuzi Martin Saanya, ambaye alishindwa kuumudu mchezo huo na kupelekea mashabiki wa Simba kufanya uharibifu mkubwa wa miundombinu katika Uwanja huo, hali iliyoifanya Serikali kufungia timu zote mbili kuutumia.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Msemaji wa klabu hiyo, Haji Manara, alisema uamuzi wao wa kuleta waamuzi kutoka nje utamaliza migogoro ya kiuamuzi inayotokea ndani ya uwanja pindi timu hizo zinapokutana.

“Hatutacheza mchezo wowote hapa nyumbani dhidi ya Yanga, ikiwa waamuzi watatoka hapa hapa, hii ni kutokana na maamuzi mabovu wanayoyafanya.

“Tupo tayari kugharamia waamuzi wote watakaotakiwa kuchezesha mchezo wetu dhidi ya Yanga, ili kuondoa utata wa kiuamuzi unayojitokeza katika michezo yetu,” alisema Manara.

MTANZANIA halikuishia kwa Manara, lilimtafuta Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Ligi (TPLB) ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, ambaye alieleza kuwa jambo wanalotaka kufanya Simba linapingana na kanuni ya ligi hiyo.

“Kanuni ya ligi inasema, waamuzi wakataochezesha ligi kuu ni wale wenye daraja la kwanza waliofaulu katika semina na majaribio ya vipimo vya afya yanayoendeshwa na Kamati ya Waamuzi ya TFF, hivyo mamlaka ya uteuzi wa waamuzi kuchezesha michezo ya ligi yanatolewa na Kamati hiyo,” alisema Wambura.

Hata hivyo, endapo Simba watafanikiwa zoezi la kuwaleta waamuzi hao watalazimika kulipa Dola 750 (Sawa na Shilingi 1,635,075) kwa kila mmoja kati ya waamuzi wanne wanaotakiwa, tiketi ya ndege ya kwenda na kurudi, maradhi, ulinzi wa uhakika, usafiri wa ndani na eskoti ya polisi baada ya mchezo.

Wakati huo huo, klabu hiyo imejipanga kuomba kukutana na Rais wa TFF, Jamal Malinzi, ili kueleza dukuduku juu ya malalamiko yao kutofanyiwa kazi, likiwamo suala la mchezaji wao wa zamani, Hassan Ramadhani ‘Kessy’.

“Yapo malalamiko mengi ambayo tumeyapeleka TFF, lakini hadi sasa hakuna uamuzi uliochukuliwa jambo ambalo linatukatisha tamaa.

“Mbali na Kessy, hadi sasa TFF wanashindwa kutoa uamuzi juu ya mwamuzi aliyechezesha mchezo wetu na Yanga, Martin Saanya, wakati wanajua bila uamuzi wake mashabiki wetu wasingefanya vurugu zozote na kuharibu miundombinu,” alisema Manara.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles