27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Simba, JKT Ruvu kazi ipo Taifa

NA ABDUCADO EMMANUEL, DAR ES SALAAM

TIMU ya Simba leo itakuwa na shughuli pevu ya kusaka ushindi itakapovaana na JKT Ruvu katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), utakaofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 jioni.

Simba itaingia dimbani ikiwa na kumbukumbu ya kufungwa mabao 2-1 na Mbeya City kwenye mchezo uliopita uliofanyika Jumatano iliyopita, JKT Ruvu wao waliambulia sare ya bao 1-1 walipovaana na Mtibwa Sugar.

Kipigo dhidi ya Mbeya City kilipelekea mashabiki wa Simba kuwajia juu wachezaji wao mara baada ya mechi hiyo, iliyopelekea Jeshi la Polisi kuwatawanya kwa mabomu ya machozi na hali kuwa shwari.

Mshambuliaji wa wekundu hao, Mganda Emmanuel Okwi, aliyezimia uwanjani na kukimbizwa hospitali kwenye mchezo dhidi ya Azam baada ya kugongana na beki wa timu hiyo, Aggrey Morris, leo atarejea uwanjani kuwavaa maafande hao.

Lakini Simba itaendelea kumkosa kiungo wake, Said Ndemla, aliyepumzishwa kwa muda wa takribani wiki mbili kuuguza majeraha ya nyama za paja aliyopata kwenye mchezo dhidi ya Azam, ulioisha kwa sare ya bao 1-1.

Kama Simba itapoteza mchezo huo basi itazidi kujiweka pabaya kwenye msimamo wa ligi kwani inaweza kuteremka kwa nafasi moja na kushika nafasi ya 12, iwapo Stand United itashinda katika mechi yake ya leo dhidi ya Ruvu Shooting itakayofanyika Uwanja wa Mabatini, Pwani.
Ushindi wowote wa wekundu hao utaifanya kusogea katika msimamo wa ligi endapo timu za juu yake zitaangukia pua kwenye mechi zao, JKT Ruvu yenyewe itaweza kulingana pointi na vinara Azam wenye pointi 21 kama itafanikiwa kuifunga Simba leo.

Matola ajiuzulu, Ndemla awaniwa Ulaya

Rais wa timu ya Simba, Evans Aveva, ameeleza jijini Dar es Salaam jana kuwa kocha msaidizi wa timu hiyo, Seleman Matola, amejiuzulu kwenye nafasi yake hiyo kutokana na matatizo ya kifamilia huku akiomba kupumzika.

Aveva alisema alipata barua hiyo juzi jioni, ambapo wataijadili na baadaye watatoa uamuzi kwa kuwa Matola ni kati ya wachezaji wa zamani wa Simba ambao walikuwa na utii na nidhamu ya hali ya juu.

Matola aliiongoza Simba kama nahodha miaka ya nyuma na kuipatia mataji mengi ikiwemo kuifikisha timu hiyo katika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuiondosha Zamalek ya Misri mwaka 2003.

Sababu kubwa nyingine inayoelezwa ambayo imechangia Matola kubwaga manyanga,ni matokeo mabovu ya timu hiyo kwenye mechi za Ligi Kuu.

Akizungumzia mwenendo huo, Aveva alisema timu hiyo inafanya vibaya katika mechi za Ligi Kuu kwa sababu ya wachezaji kuchoka baada ya kucheza mechi 10 za mashindano ndani ya siku 30.

Aveva pia alitangaza Mkutano Mkuu wa dharura wa Simba utakaofanyika Machi mosi mwaka huu, huku akidai mkutano huo ni wa kikatiba na wanachama watapata fursa ya kujadili masuala mbalimbali ya klabu hiyo.

Wakati huo huo, kiungo wa Simba, Said Ndemla, anawaniwa na mawakala watano wa Ulaya kutoka nchi za Ujerumani, Hispania na Ulaya Mashariki kwenda kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa.

Aveva alisema mawakala hao, wamepitia kwa kocha mkuu wa timu hiyo, Mserbia Goran Kopunovic, ambapo Ndemla ataondoka nchini muda wowote kuanzia sasa kujaribu bahati katika nchi hizo.

Coastal, Mtibwa kuonyeshana ubabe

Mechi nyingine ya nguvu itafanyika kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga kwa wenyeji Coastal Union kuwakaribisha Mtibwa Sugar, inayoshika nafasi ya nne katika msimamo wa ligi.

Mtibwa Sugar itaingia dimbani ikiwa na kumbukumbu ya kufungwa na Ruvu Shooting mabao 2-1 na kupoteza rekodi yake ya kutofungwa kwenye michezo tisa ya awali ya ligi, Coastal Union nayo ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Stand United, ukiwa ni ushindi wa kwanza chini ya kocha, James Nandwa, aliyerithi mikoba ya mwenzake, Yusuph Chipo.

Kagera Sugar iliyofungwa mabao 2-1 na Ndanda FC wiki iliyopita, itakuwa kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya kuivaa timu inayoburuza mkia katika msimamo wa ligi hiyo, Tanzania Prisons.

Nyasi za Uwanja wa Jamhuri, mjini Morogoro nazo zitawaka moto kwa wenyeji Polisi Morogoro kupambana na wababe wa Simba, Mbeya City.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles