31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Simba haichagui wakupiga

JACKLINE LAIZER, ARUSHA

SIMBA imeendeleza hasira zake baada ya jana kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Singida United,  katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini hapa.

Katika mchezo huo, uliochezeshwa na mwamuzi Ahmad Simba kutoka mkoani Kagere, bao pekee la Simba lilifungwa na Miraji Athumani.

Matokeo hayo, yameiwezesha Simba kufikisha pointi 18 baada ya kucheza mchezo sita huku ikiendelea kufukuzia rekodi ya msimu wa 2009, ambao walichukua ubingwa bila kufungwa.

Simba  walipata ushindi wa tatu wakiwa ugenini baada ya kuifunga Kagera Sugar mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba, kabla ya kupata ushindi wa  mabao 2-0 dhidi ya Biashara United katika mchezo uliochezwa  Uwanja wa Karume mjini Musoma .

Katika mchezo wa jana, ukuanza kwa kasi huku kila timu ikisaka bao la mapema, lakini milango ilionekana ni migumu.

Hata hivyo, mchezaji wa Singida United,  Gilbert Mbweni alionyeshwa kadi ya njano kwa kosa la kumchezea madhambi beki wa Simba Haruna Shamte.

Simba  walifanikiwa kupata bao dakika ya 42 kupitia kwa Athuman, baada ya beki wa timu hiyo, Pascal Wawa kumtangulizia pasi ndefu na kupiga shuti lililokwenda moja kwa moja wavuni.

Mshambuliaji wa Simba, Meddie Kagere alikosa bao la wazi dakika ya 49, baada ya kupenyezewa  pasi safi na Deo Kanda, lakini alipaisha shuti lake.

Wawa aliyepanda mbele kusaidia mashambilizi alikosa bao dakika ya 54, baada ya kupokea pasi kutoka kwa kiungo Mzamiru Yassin, lakini alipaisha shuti lake.

Dakika ya 60 Said Ndemla  wa Simba alishindwa kufunga baada ya kufumbua shuti kali ambalo lililishia mkononi mwa kipa wa Singida United, Mkumbo  Mfasiri.

Singida United  walifanikiwa kufanya shambulizi nzuri dakika ya 68 , lakini  walikosa umakini wa kufunga.

Mwamuzi Simba, alimwonesha kadi ya njano beki wa timu ya Simba, Gadiel Michael  dakika ya 73 kutokana na kuchelewesha kurusha mpira.

Rashid Juma aliyetokea benchi kuchukua nafasi ya Kanda alijaribu kupiga shuti la kichwa,  baada ya Ndemla  kuingiza krosi kati, lakini kipa wa Singida alituliza na kuokoa hatari hiyo.

Singida United; Mkumbo Msafiri, George Wawa Gilbert Mbweni, Daud Mbweni, Meshaki Kibona/Himid Suleiman (dk.89), David Nartey, Elinyesi Sumbi, Jonathan Daka/Emmanuel Manya (dk. 46), Pascal Ndaga, Stephano Opoku na Ismail Ally.

Simba; Aishi Manula, Haruna Shamte, Gadiel Michael, Erasto Nyoni, Paschal Wawa, Said Ndemla, Deo Kanda/Rashid Juma (dk. 71), Mzamiru Yassin, Meddie Kagere, Ibrahim Ajib/Hassan Dilunga (dk. 50) na Miraj Athuman/ Gerson Fraga (dk. 80).

Mchezo mwingine uliochezwa Uwanja wa Mabatini, mkoani Pwani, Ruvu Shooting  iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya  Azam, wakati timu ya Biashara United ikiifunga Namungo bao 1-0 kwenye Uwanja wa Karume, Musoma.

Timu ya Mwadui ilitoka sare ya mabao 2-2 na JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Kambarage, mjini Shinyanga na Coastal Union iliondoka na ushindi wa bao 1-0 dhidi Lipuli  kwenye Uwanja wa Samora, mkoani Iringa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles