WAKATI mashabiki wa timu ya Simba wakiwa na shauku kubwa kutaka kujua ujio wa kocha mkuu wa timu hiyo, uongozi wa klabu hiyo umewatuliza presha kwa kuahidi kumtangaza rasmi kocha mpya ndani ya wiki mbili kabla ya kuanza michezo ya kirafiki ya kujiandaa na msimu mpya wa 2016/17.
Simba bado wanaumiza kichwa kufanya uamuzi wa kupata saini ya kocha mmoja kati ya makocha wawili wa kimataifa ambaye ataweza kuiletea mafanikio timu hiyo msimu ujao, akiwamo aliyekuwa kocha wa timu ya taifa ya Kenya Mscotlandm Bobby Williamson na mwingine ambaye jina lake halikutajwa.
Kocha huyo ana kila dalili ya kutua Msimbazi kipindi hiki cha usajili kwa ajili ya msimu ujao, kutokana na hali iliyopo ndani ya benchi la ufundi la Kenya ambapo kwa sasa Shirikisho la soka la nchi hiyo ‘KFF’, limempa madaraka ya kuiongoza timu hiyo ya taifa kocha mzawa, Stanley Okumbi, akisaidiwa na Mussa Otieno.
Taarifa toka ndani ya klabu ya Simba, zinadai kwamba baada ya mipango yake ya kupata saini ya kocha wa Taifa wa Zimbabwe, Kalisto Pasuwa, kuvurugika ipo kwenye mazungumzo ya mwisho na makocha hao akiwamo Bobby.
“Tulikaribia kuipata saini ya Pasuwa ambaye alikuwa chaguo letu la kwanza, lakini kutokana na mkataba wake kuwa wa muda mrefu pia timu yake kufuzu katika fainali za mataifa ya Afrika, Afcon hivyo ikawa kikwazo kwetu, hata hivyo hatujakata tamaa na tunaahidi kupata kocha bora, tunawataka mashabiki watulie, safari hii hatutafanya makosa kama yaliyopita, tutafanya uamuzi sahihi kwa ajili ya mafanikio ya Simba.
“Ndani ya wiki mbili kila kitu kitakuwa wazi pamoja na majina ya wachezaji wapya ambao tayari tumeshawasajili kwa ajili ya msimu ujao.
“Tutasajili wachezaji kulingana na uhitaji wa klabu kwa kuangalia eneo lenye mapungufu ndani ya kikosi cha Simba,” kilisema chanzo hicho.
Chanzo hicho kilisema kwamba, hadi sasa klabu hiyo imewasajili wachezaji watano ambao ni beki wa kati, Emmanuel Semwanza, Hamad Juma, Ramadhani ‘Chiza’ Kichuya, Muzamil Yassin na Jamal Mnyate kutoka Mwadui FC inayonolewa na Jamhuri Kihwelu ‘Julio’.
“Tunafanya mambo yetu kwa utulivu wa hali ya juu, ndio maana tunasajili wachezaji wapya kwa uangalifu mkubwa ili kuepusha hujuma msimu ujao,” kilisema chanzo hicho