23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Simba abeba mtoto aliyelala na mama yake, amtafuna

Gurian Adolf -Katavi

WATU watatu wamefariki dunia katika matukio tofauti, likiwamo la mtoto Kangwa Manuga (6) aliyeliwa na simba, wakati amelala na mama yake katika Kijiji cha Sitalike wilayani Mpanda.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Benjamin  Kuzaga, alisema tukio la mtoto huyo kuliwa na simba, lilitokea mwishoni mwa wiki saa 4 za usiku akiwa amelala na mama yake nyumbani kwao.

Alisema mtoto huyo akiwa na mama yake wamelala ndani ya nyumba ambayo haikuwa na mlango imara, walivamiwa na simba.

“Walikuwa wanaishi nyumba ambayo haikuwa na mlango imara, huyu mtoto siku zote yuko na wazazi wake, siku ya tukio baba hakuwapo nyumbani. Ule udhaifu wa mlango ulichangia mnyama huyu kuingia ndani kirahisi,” alisema.

Kamanda Kuzaga alisema katika nyumba hiyo ambayo ni kama kibanda, kulikuwa na ng’ombe lakini simba huyo hakuhangaika nao.

Alisema simba aliingia ndani na kumnyakua mtoto huyo, kisha kutoka naye nje na kumwacha mama yake akiangua kilio.

Kamanda Kuzaga alisema mama huyo alianza jitihada za kumwokoa mtoto wake mikononi mwa simba kwa kumrushia kuni zilizokuwa zikiwawaka moto, huku akipiga yowe kuomba msaada kwa majirani.

Alisema pamoja na jitihada za mama huyo, simba alifanikiwa kukimbia na mtoto vichakani.

Kamanda Kuzaga alisema polisi na  wanakijiji walifika eneo la tukio na walikuta mtoto huyo tayari ameliwa na simba ambaye hawakuweza kumwona.

“Baada ya wananchi na askari wetu kufika eneo la tukio, walikuta mabaki ya kichwa na mifupa ya miguuni tu, huku viungo vingine vikiwa vimeliwa,” alisema.

Katika tukio jingine, Mwenyekiti wa Kijiji cha Shanwe, Romward Fungameza, alisema watu wawili wakazi wa kijiji hicho waliuawa na viboko mwishoni mwa wiki, wakati walipokwenda kuvua samaki bwawa la Milala.

Alisema viboko waliweka makazi katika bwawa hilo lililochimbwa kwa mradi wa maji, wakitoka Hifadhi ya Taifa ya Katavi.

Fungameza alisema wakazi wa kijiji hicho walifanikiwa kuopoa mwili wa marehemu Timos Pius ndani ya maji, lakini mtu wa pili hajapatikana na jitihada za kumtafuta zinaendelea.

Alisema muda mrefu wakazi wa kijiji hicho, wamekuwa wakiiomba Serikali kuua viboko hao kwa sababu wamesababisha maafa makubwa kwa wakazi wa kijiji hicho.

Hivi karibuni, uongozi wa mkoa kwa kushirikiana na Idara ya Wanyamapori Tanzania (TAWA), walivuna viboko zaidi ya 60 waliopo katika bwawa hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles