26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Siku 47 za Maximo Yanga SC usipime

Marcio Maximo
Kocha wa Yanga, Marcio Maximo

NA ABDUCADO EMMANUEL, DAR ES SALAAM

KAMA kuna kitu kikubwa kwa kocha yeyote duniani, ni kufikia malengo aliyojiwekea.

Malengo hayo yana njia zake na hiyo hutokana na falsafa za kocha husika kwa kile anachokiamini.

Juni 29, mwaka huu, Yanga ilimrejesha kocha wa zamani wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Mbrazil Marcio Maximo, kama kocha wao mkuu pamoja na Mbrazil mwingine, Leonardo Neiva, ambaye ni msaidizi wake.

Julai 1 mwaka huu, Maximo alianza kibarua cha kuifundisha Yanga, ambapo aliwafanyisha mazoezi ya ufukweni kwa siku nne na nyota wake ili kuwaongezea stamina.

Maximo atakuwa na mtihani mzito msimu ujao wa timu yake kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.

Hivi sasa Maximo programu yake imetimiza siku takribani 47 hadi kufikia jana, ambayo imeonesha kuwa tofauti sana na makocha wengine wa kigeni wanaokuja nchini.

Ifuatayo ni tathimini fupi kuhusiana na mambo aliyoyaleta Maximo Yanga na yaliyo kwenye mipango yake ya baadaye ili timu hiyo kufikia mafanikio.

Nidhamu

Maximo, kama walivyo makocha wote duniani, huzingatia nidhamu kwenye kikosi chake, ili kudhihirisha hataki masihara alifanya kikao na wachezaji wote siku moja kabla ya kuanza kibarua chake na kusisitiza suala hilo kwa wachezaji wake.

Itakumbukwa alipokuwa Stars miaka minne iliyopita, aliwahi kuwafungia vioo wachezaji mahiri wa Tanzania, Juma Kaseja, Athuman Iddi ‘Chuji’ na Haruna Moshi ‘Boban’ kwa vitendo vya utovu wa nidhamu, lakini baada ya kutua Yanga hivi sasa amewasamehe.

Soka ya kasi, uwajibikaji

Mbrazil huyo ameonekana kufundisha soka la kasi zaidi kwenye mazoezi yake, huku akiwatumia zaidi mabeki wa pembeni kupanda kwa kasi kufanya mashambulizi.

Katika kuonyesha amedhamiria hilo, ndiyo maana amemsajili beki wa kushoto, Edward Charles kutoka JKT Ruvu, ambapo amedai beki huyo ni mzuri kwenye kushambulia na kuzuia.

“Napenda mabeki wanaoshambulia sana na ndiyo maana nimemsajili Charles, ni mzuri kwenye eneo la ulinzi na kushambulia,” alisema Maximo.

Katika hatua nyingine, Maximo ameleta mfumo wa kila mchezaji kuwajibika kwenye timu kwa staili ya kuzibiana nafasi kwa kucheza namba tofauti uwanjani, hataki kabisa mchezaji anayesimama uwanjani kuwategea wenzake.

Awapa ujuzi wachezaji

Maximo si kama makocha wengine ambao huingiza mifumo na falsafa zao kwenye timu moja kwa moja wanapoanza kazi zao.

Mbrazil huyo ameonekana kuwapa ujuzi mbadala wachezaji wake kwa kuwafundisha namna ya kupiga pasi, kumiliki mipira (danadana, vichwa) na kupiga mipira mirefu, yaani vile vitu ambavyo wachezaji hupewa wakiwa na umri mdogo ‘basics’.

Ushindani

Maximo amekubali muziki wa kikosi chake, ambapo amekiri kabisa kuna ushindani mkubwa kwenye kikosi hicho, hasa baada ya kurejea wachezaji waliokuwa kwenye majukumu ya timu zao za Taifa.

Baadhi ya wachezaji waliokuwa timu za Taifa ni Kelvin Yondani, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Deogratius Munishi ‘Dida’, Haruna Niyonzima, Hamis Kiiza, ambapo Maximo amedai atapata kikosi bora kutokana na hilo.

“Nimefurahishwa kwa kweli na hali hii, kuna ushindani mkubwa sana, nidhamu ya hali juu kwa wachezaji na uwajibikaji, hii inanionyesha ishara njema baadaye ya kikosi changu kufanya vizuri,” alisema.

Maximo pia alishangazwa na ushindani huo kiasi kwamba ilifikia wakati mchezaji aliyeumia au kuumwa malaria amekuwa akiomba kufanya mazoezi, jambo ambalo hakukubaliana nalo.

Haamini ‘first eleven’

Maximo ameweka wazi kuwa hana kikosi cha kwanza na atakuwa akiwapanga wachezaji wake kulingana na viwango vyao kwenye mechi na mazoezini.

Mbrazil huyo amesema haamini kikosi cha kwanza kwenye aina yake ya ufundishaji, kwani si wanaobadilisha mchezo.

“Siamini kuhusiana na wachezaji wa kikosi cha kwanza, kwani wachezaji wazuri wapo benchi na hao ndio wanaobadili mchezo siku zote, hivyo nawaamini sana wachezaji hao,” alisema.

Awapa shavu vijana

Katika kuhakikisha anaendeleza falsafa yake ya kutumia wachezaji vijana, Maximo amewapandisha wachezaji sita kutoka timu ya vijana ya Yanga, ambao ni asilimia 20 ya kikosi chake, amedai msimu ujao watafikia asilimia 40.

Wachezaji hao sita ni beki wa kushoto Amos Abel, Issa Ngao, Gerald, Hamis Issa, Ben Michael na Sospeter Maiga.

Miundombinu

Maximo ameangalia kwa makini mafanikio waliyokuwa nayo Azam FC kupitia uwekezaji wao mkubwa kwenye miondombinu, ambapo ameeleza ataifanya Yanga kuifikia timu hiyo miaka michache ijayo.

“Azam nimeiona ni timu nzuri na kwa kiasi kikubwa uwekezaji wao kwenye miundombinu ndio umeifanya kufikia huko, miaka michache ijayo Yanga itakuwa kama wao kupitia uwekezaji tunaotarajia kuufanya,” alisema.

Ujio wa Jaja, Coutinho

Ujio wa wachezaji wa Kibrazil kwenye kikosi hicho, Geilson Santos Santana ‘Jaja’ na Andrey Coutinho, Maximo ameuelezea kuwa ni kufungua milango kwa wachezaji wa Kitanzania kwenda nao kucheza soka la kulipwa nchini Brazil.

“Ujio wa Jaja na Coutinho ni mzuri, kama ilivyo kwa wao kuja hapa basi milango ya Watanzania kucheza Brazil inafunguka zaidi. Baadaye pia tunataka kufanya ushirikiano na timu za Brazil kwa wachezaji wetu vijana kupata mafunzo kule,” alisema.

Ataka ubingwa

Maximo amekiri msimu ujao wa Ligi utakuwa mgumu kwa ushindani mkubwa, baada ya kuwaona mabingwa Azam FC, Simba na Mbeya City, lakini amejinasibu Yanga itatwaa ubingwa huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles