23.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

SHULE YA PIUS ILIVYOPANIA KUZALISHA WANASAYANSI

NA CHRISTINA GAULUHANGA-DAR ES SALAAM


MWAKA jana serikali iliagiza Halmashauri zote nchini kujenga maabara za kisasa na za kutosha ili kusaidia wanafunzi wa masomo ya sayansi kusoma kwa nadharia na vitendo.

Agizo hilo lilitoka baada ya kubainika juwapo kwa uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi na kuifanya serikali kuongeza idadi ya wanafunzi wa masomo hayo nchini.

Sheria namba 25 ya mwaka 1978 iliruhusu sekta ya elimu nchini, sekta isiyo ya serikali kuanzisha,kusajili na kuendesha shule na vyuo vinavyotoa elimu kwa mtaala unaoandaliwa na Serikali wadau wa sekta binafsi waliungana na serikali ili kutoa elimu bora.

Hata hivyo, mbali ya kutoa elimu yenye ubora wadau hao pia walifanya kila jitihada kuwekeza katika mazingira yenye vivutio ili walimu waweze kufanya kazi ipasavyo.

Zipo jitihada nyingi zinazofanywa na wadau wa elimu ikiwa ni pamoja na kuwekeza madarasa ya kutosha kujifunzia wanafunzi, maabara za kisasa, maktaba zenye vitabu vya kiada na rejea pamoja na mazingira mazuri ya kuishi.

Zipo shule nyingi ambazo zimekuwa kivutio cha wanafunzi kufaulu kwa wingi na ubora wa majengo yake ambapo Shule ya Sekondari ya Pius Iliyopo Kongowe Manispaa ya Temeke nayo ni miongoni mwa shule binafsi zilizopiga hatua katika suala la elimu.

Mkuu wa shule hiyo, Lucas Hassan anasema kwa kutambua upungufu wa wataalamu wa sayansi nchini wamejikita kuzalisha wataalamu hao kwa kutoa elimu bora ambayo inaendana na mtaala ulioandaliwa na serikali.

“Shule yetu tumejipanga kuhakikisha asilimia 80 ya wanafunzi wanaosoma shuleni hapa wanapenda masomo ya sayansi, ili kupata wataalamu wa kutosha na kuiunga mkono serikali.

“Ili kupunguza uhaba wa walimu wa sayansi tumeweka misingi mizuri sambamba na kuwa na walimu bora wa masomo hayo ambao wanawafundisha wanafunzi kwa nadharia na vitendo,” anasema mwalimu huyo.

Anaongeza kuwa shule hiyo wamejenga maabara ya kisasa ili wanafunzi waweza kusoma kwa vitendo kupitia chumba maalumu kilichojengwa cha mafunzo kwa vitendo.

“Ili tutimize malengo yetu walimu wamekuwa wakitumia mbinu mbadala kuhakikisha wanafunzi wanayapenda masomo hayo kwa kuwafundisha kwa nadharia na vitendo,” anasema Hassan.


Anaongeza kuwa uwepo wa maabara za kisasa kumesaidia wanafunzi kupata elimu bora ambayo inaendana na kiwango kilichopo.

Pia anasema kwa kutambua mchango wa walimu shule hiyo imekuwa ikitoa motisha mbalimbali zikiwemo fedha kwa walimu wanaofaulisha jambo ambalo linazidi kuamsha ari kwa  walimu kujituma zaidi katika ufundishaji.

Hassan anawaasa wanafunzi wahitimu na wengineo kutumia muda mwingi kujisomea ili waweze kufanya mtihani wao vizuri na kwa utulivu.

Naye, Askofu Frank Kadodo wa Kanisa Huru la Kipentekoste Tanzania (FPCT), anawataka wazazi na walezi kuwashawishi watoto wao kujiajiri na kujiunga katika vikundi mbalimbali vya ujasiriamali.

Anasema ili taifa liweze kutimiza malengo yake ya kufikia uchumi wa kati ni lazima vijana wajenge tabia ya kupenda kujiajiri.

Kadodo anasema mfumo uliopo nchini hivi sasa haumpi mwanafunzi fursa ya kuweza kujiajiri hivyo wazazi wanatakiwa kuwa  karibu na watoto wao ili kuwapa ushirikiano wa kuweza kujiajiri wenyewe punde wanapomaliza masomo yao.

“Ili kufikia uchumi wa viwanda ni lazima wazazi nao wawape watoto wao ushirikiano katika masomo yao… hili halikwepeki vinginevyo kila kukicha tutakuwa tunakabiliwa na changamoto mbalimbali za kielimu nchini,” anasema Kadodo.
 

Pia anawataka vijana hao kuwa watiifu kwa wazazi wao na kuwa mfano wa kuigwa na jamii kwa kufuata maadili ili wafanikiwe katika maisha yao.

Kadodo anasema hivi sasa maadili yamepungua kwa vijana wa kitanzania ndio maana mambo mengi hayaendi sawa kwa sababu ukosefu wa maadili.

Kwa upande wake, Meneja wa shule hiyo Mbaulidia Bugingo anawataka wanafunzi wanaomaliza kidato cha sita  kuendeleza nidhamu waliyoipata shuleni na kujiepusha na makundi yasiyofaa.

Jumla ya wanafunzi 211 shuleni hapo  wanatarajia kuungana na wengine nchini kufanya mtihani wa taifa wa kidato cha sita mwaka huu ambapo kati yao wanawake ni 76 na wavulana 135.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles