27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Shule ya kimataifa yachunguzwa kwa ushoga

Na WAANDISHI WETU – DAR ES SALAAM

SERIKALI inachunguza Shule ya Msingi ya Heaven of Peace Academy (HOPAC) iliyopo Salasala, Barabara ya Bagamoyo, Dar es Salaam kwa kashfa ya kuhamasisha wanafunzi kufanya vitendo vya ushoga.

Kwa mujibu wa taarifa zilizosambaa katika mitandao ya jamii hivi karibuni, siku ijulikanayo kama ‘International Day’ (Siku ya Kimataifa) ambayo wazazi nao hufika shuleni hapo, wanafunzi walifanya onesho la ushoga na kuutetea kuwa ni haki ya kila mtu.

Katika onesho hilo, pamoja na mambo mengine, inadaiwa wanafunzi walinyanyua bendera yenye alama ambazo zinadaiwa hutumiwa na watu wanaojihusisha na ushoga.

“Shule ya Heaven watoto wame-‘perform theme’ ya ushoga, ni haki ya kila mtu kuchagua akipendacho na kwamba watoto wajijue mapema ‘their sexual preference’ (mapendeleo yao ya ngono) waongee na wazazi wao,” ilisema sehemu ya taarifa iliyosambaa katika mitandao ya kijamii.

Akizungumza na MTANZANIA kuhusu taarifa hizo jana, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Leornad Akwilapo, alisema wameona tukio hilo katika mitandao na baadhi ya vyombo vya habari na haraka wametuma timu kufuatilia.

“Ni kweli tumeona kwenye mitandao watoto hao wakiwa wameshikilia bendera zikiwa na rangi nyingi nyingi mpaka hata mimi sijajua nini maana yake.

“Lakini baada ya kuona hilo, tayari tumetuma timu ya uchunguzi inayoongozwa na Mdhibiti Ubora wa Kanda ya Dar es Salaam, kwa ajili ya uchunguzi zaidi, kisha tutatoa majibu ya nini kilikuwa kinaendelea,” alisema Dk. Akwilapo.

Mtumishi wa shule hiyo ambaye yuko kitengo cha utawala, Marietha Tarimo aliliambia MTANZANIA kuwa hata yeye aliwaona wanafunzi wakiwa wameshika bendera hizo na kwamba hakuelewa maana yake.

“Mimi si msemaji, lakini niko upande wa utawala na nimeona baada ya kushika hizo bendera zimetafsiriwa tofauti maana ya ushoga, hata sifahamu pia kama zilikuwa zikimaanisha hivyo au laa.

“Na kama unahitaji ufafanuzi zaidi fika shuleni kesho asubuhi (leo) kwa sababu muda huu walimu na viongozi wote wameshatawanyika… lakini pia ukienda kwenye ukurasa wetu wa Facebook utakuta maelezo kuhusu hilo jambo,” alisema mtumishi huyo.

Katika ukurasa wa Facebook wa shule hiyo uliandikwa ujumbe ukisema; “Leo hii tulitembelewa na mwakilishi kutoka Wizara ya Elimu kwa minajili ya kuchunguza shule yetu.

“Katika ujio huo wameuliza maswali kadhaa, maswali yao yalihusu mitaala na vipindi kwa nia ya kuona kama vinaendana na namna tunavyofundisha, waliuliza maswali kwa watawala, walimu na wanafunzi.

“Haven of Peace Academy (HOPAC) inaomba msamaha kutokana na kile kilichotokea wakati tunaadhimisha tamasha la Siku ya Kimataifa Ijumaa 9, Novemba mwaka huu.

“Tunasisitiza HOPAC hatukuruhusu na hatukubali vitu vinavyounga mkono ushoga na usagaji.

“Picha na maelezo yanayosambaa kwenye mitandao ya kijamii ni ya upotoshaji. Haina uhusiano na kile ambacho HOPAC inasimamia na pia haielezi maudhui ya kusherehekea wanafunzi wetu wanaotoka mataifa mbalimbali.

“Tumegundua kinachofikiriwa na umma kwa ujumla kwa sasa ni kwamba HOPAC kama taasisi inahalalisha vitendo vya ushoga na ndiyo kwa maana tunaomba radhi. Sio sehemu sahihi kama shule kutoa matamko ya kisiasa.

“Wanafunzi wahusika ambao walitoa tamko hilo hawawakilishi shule. Hawa wanafunzi wameshapewa adhabu ya ndani kwa ndani kwa mujibu wa sera ya nidhamu ya shule.

“Tutashukuru kwa kutusaidia kuacha kueneza tuhuma za uongo kuhusu shule yetu na kila mwanafunzi ambaye alisoma hapa wamekuwa mfano mzuri kwa sababu shule yetu inadumisha imani ya Wakristo Tanzania.”

Oktoba 31, mwaka huu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alitangaza kampeni ya kupambana na ushoga na kuunda kamati ya watu 15 kuongoza mapambano hayo.

Kwa mujibu wa sheria za Tanzania, kufanya mapenzi ‘kinyume na maumbile’ ni kosa la jinai ambalo mtu akikutwa na hatia adhabu yake ni kifungo cha miaka 30 au maisha jela.

Baada ya tangazo la Makonda, Novemba 4, mwaka huu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ilitoa taarifa ikisema kampeni hiyo ni mawazo binafsi ya Makonda na si msimamo rasmi wa Serikali.

“Serikali ya Tanzania ingependa kufafanua kwamba hayo ni mawazo yake (Makonda) na si msimamo wa Serikali,” ilisema taarifa hiyo.

Katika taarifa hiyo, Serikali ilisema itaendelea kuheshimu mikataba yote ya kimataifa ambayo imeisaini na kuiridhia.

“Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea na itaendelea kuheshimu na kulinda haki hizo kama zilivyo katika Katiba,” ilisema taarifa hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles