25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Shule binafsi zaongoza matokeo darasa la saba

Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani (NECTA), Dk Charles Msonde, akionesha sare za wanafunzi wa darasa la saba wa shule binafsi zikiwa zimejazwa majibu ya mitihani wakati akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam jana.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani (NECTA), Dk Charles Msonde, akionesha sare za wanafunzi wa darasa la saba wa shule binafsi zikiwa zimejazwa majibu ya mitihani wakati akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam jana.

NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

BARAZA la Mitihani la Taifa (NECTA), limetangaza matokeo ya Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi (PSLE) uliofanyika Septemba, mwaka huu, huku shule binafsi zikizipiga teke za Serikali.

Katika matokeo hayo, Mkoa wa Geita umeng’ara kwa kushika nafasi ya kwanza kitaifa.

Matokeo hayo yanaonyesha kuwa ufaulu wa jumla umepanda kwa asilimia 2.52 ikilinganishwa na mwaka jana ambao ulikuwa asilimia 67.84. Mwaka huu ni asilimia 73.50.

Kwa mujibu wa matokeo hayo, wavulana wamefanya vizuri kwa kushika nafasi tisa katika 10 za kwanza (kumi bora), huku msichana akishika nafasi ya nne katika orodha hiyo.

Akitangaza matokeo hayo jana, Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk. Charles Msonde, alisema jumla ya watahiniwa 795,739 walisajiliwa kufanya mtihani huo, wasichana wakiwa 422,864 sawa na asilimia 53.14 na wavulana 372,875 sawa na asilimia 46.86.

Alisema kati ya watahiniwa waliosajiliwa, 811 walikuwa na uono hafifu na 95 walikuwa ni wasioona.

“Watahiniwa 789,479 sawa na asilimia 99.21 ya waliosajiliwa walifanya mtihani, kati yao wasichana walikuwa 419,932 sawa na asilimia 99.31 na wavulana walikuwa 369,547 sawa na asilimia 99.11. Watahiniwa 6,260 sawa na asilimia 0.79 hawakufanya mtihani kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo utoro na ugonjwa, kati yao wasichana ni 2,932 na wavulana ni 3,328,” alisema.

Dk. Msonde alisema matokeo hayo yanaonyesha jumla ya watahiniwa 555,291 kati ya 795,739 waliosajiliwa wamefaulu mtihani huo, na kwamba watahiniwa wamepata alama 100 au zaidi kati ya 250.

“Idadi ya watahiniwa waliofaulu ni sawa na asilimia 70.36, kati yao wasichana ni 283,751 ambao ni sawa na asilimia 67.59 na wavulana ni 271,540 sawa na asilimia 73.50. Mwaka jana watahiniwa waliofaulu walikuwa asilimia 67.84, hivyo kuna ongezeko la asilimia 2.52,” alisema.

UFAULU KIMASOMO

Dk. Msonde alisema takwimu za matokeo hayo zinaonyesha kuwa ufaulu katika masomo ya Sayansi na Maarifa ya Jamii umepanda kwa asilimia kati ya 4.06 hadi 14.76 ikilinganishwa na mwaka jana.

“Kwa masomo ya Kiswahili, Hisabati na Kiingereza, ufaulu umeshuka kwa asilimia 0.39 na 12.51 ikilinganishwa na mwaka jana. Watahiniwa wamefaulu zaidi katika somo la Kiswahili ambalo ufaulu ni asilimia 76.81. Somo walilofaulu kwa kiwango cha chini ni Kiingereza lenye ufaulu wa asilimia 36.05.

10 BORA KITAIFA

Alisema watahiniwa 10 waliofanya vizuri ni Japhet Stephano, Jamal Athuman, Enock Bundala, Jacob Wagine, Isaac Isaac, Daniel Kitundu, Benjamin Shabu wote wa shule ya Kwema iliyoko mkoani Shinyanga, Justina Gerald, Shabani Mavunde wa Tusiime, Dar es Salaam na Azad Ayatullah wa Kaizirege, Kagera.

WASICHANA 10 BORA

Dk. Msonde aliwataja wasichana 10 bora kitaifa kuwa ni Justina Pius Gerald, Danielle Adhiambo Onditi, Asnath Haruni Lemanya (Tusiime), Linda Blasio Mtapima, Ashura Ngwashi Makoba (Kaizirege), Rachel Godwin Ntitu (Fountain of joy), Irene Leonard Mwijage (Atlas), Fatuma Ramadhan Singili, Magdalena Deogratias (Rocken Hill) na Cecilia Gabriel Kenene (Mugini).

WAVULANA 10 BORA

Alisema wavulana waliofaulu vizuri ni Japhet Stephano, Jamal Athuman, Enock Bundala, Jacob Wagine, Isaac Isaac, Daniel Kitundu, Benjamin Benevenuto na Benezeth Hango (Kwema), Shabani Mavunde (Tusiime) na Azad Ayatullah (Kaizirege).

SHULE 10 BORA

Alitaja shule zilizofanya vizuri ni Kwema na Rocken Hill zilizopo Shinyanga, Mugini ya Mwanza, Fountain of Joy, Atlas na Gift Skillfull za Dar es Salaam, Mudio Islamic ya Kilimanjaro, St. Achileus ya Kagera na Carmel ya Morogoro.

SHULE 10 ZILIZOFANYA VIBAYA

Dk. Msonde alizitaja shule kumi zilizofanya vibaya kuwa ni Mgata, Kitengu, Lumba Chini, Magunga na Chohero za Morogoro, Zege na Kilole za Tanga, Nchinila ya Manyara na Ilorienito ya Arusha.

MIKOA ILIYOONGOZA

Aliitaja mikoa kumi iliyofanya vizuri zaidi kuwa ni Geita, Katavi, Iringa, Dar es Salaam, Kagera, Mwanza, Kilimanjaro, Arusha, Njombe na Tabora.

HALMASHAURI 10 BORA

Dk. Msonde alizitaja halmashauri kumi zilizoongoza kuwa ni Mpanda Manispaa iliyoko Mkoa wa Katavi, Geita Mjini, Chato zilizopo Geita, Arusha Mjini ya Arusha, Mafinga Mjini ya Iringa, Mwanza Mjini na Ilemela za Mwanza, Mji Makambako ya Njombe, Moshi Mjini na Hai za Kilimanjaro.

MIKOA ILIYOFANYA VIBAYA

Alisema hawakutaja mikoa yote iliyofanya vibaya katika matokeo hayo, na kwamba taarifa hiyo wataitoa baadae.

“Ipo mikoa mingi hatujaitaja awamu hii, wakati wowote tutatoa taarifa inayoeleza mkoa wa kwanza hadi wa mwisho, halmashauri ya kwanza hadi ya mwisho na shule ya kwanza hadi ya mwisho, kila mmoja ajue yupo nafasi gani,” alisema.

WADANGANYIFU HADHARANI

Kwa mara ya kwanza, Dk. Msonde aliwataja baadhi ya wamiliki wa shule, walimu wakuu na wasimamizi waliohusika na vitendo vya udanganyifu wakati wa mtihani huo.

“Katika Shule ya Tumaini iliyopo Sengerema, Mwanza, mmiliki wa shule hiyo, Jafari Mahunde, kwa kushirikiana na msimamizi, mwalimu Alex Singoye waliiba mtihani, waliandaa majibu ambayo watahiniwa waliyaandika kwenye sare za shule na kuingia nayo ndani ya chumba cha mtihani.

“Katika shule ya Little Flower iliyopo Serengeti, Mara, mwalimu mkuu aliiba mtihani, akaanda majibu na kumpa msimamizi mkuu, mwalimu Haruni Mumwi pamoja na msimamizi mwalimu Genipha Simon ili wawapatie watahiniwa ndani ya chumba cha mtihani,” alisema.

Aliongeza: “Katika Shule ya Mihamakumi iliyoko Sikonge, Tabora, Mwalimu Mkuu Kaombwe Samweli na walimu Leonard Maleta, Andrew Michael, Gilbert Gervas, John Puna na msimamizi Fatuma Selemani walikutwa wakiwafanyia mtihani watahiniwa na kukamatwa na maofisa wa Takukuru na Kamati ya Mtihani ya Mkoa.

Alisema katika Shule ya Qash iliyopo Babati mkoani Manyara, mwalimu alijificha chooni, kupokea maswali kutoka kwa watahiniwa na kuandaa majibu kisha kuwapatia. Waliohusika ni mwalimu Asha Mosha na mtahiniwa Najma Omari.

Alitaja shule nyingine iliyofanya udanganyifu ni Kondi Kasandalala iliyopo Sikonge, Tabora ambako wanafunzi walikutwa wana mfanano wa majibu usio wa kawaida jambo linaloonyesha walitumia chanzo kimoja cha majibu huku wahusika wakiwa ni wasimamizi Christina Chimungu wa Shule ya Msingi Chabutwa na Mosses Kasikiwe wa Matale.

“Katika shule ya St. Getrude ya Madaba, Ruvuma mwalimu mkuu Fridolina Mwalongo na walimu Michael Mwafongo, Leonard Haule, Samson Mwaijibe, January Hongoli, Alkano Kisakali na Theodate Hyera wakishirikiana na askari mgambo Peter Msigwa walibainika kufanya udanganyifu.

“Walimu hao walikuwa wanajificha kwenye mabweni na nyumba ya mwalimu iliyokuwa karibu na chumba cha mtihani, kisha wanafunzi walikuwa wanatoka kwenda kuchukua majibu wakiaga kuwa wanakwenda kujisaidia,” alisema.

HATUA ZITAKAZOCHUKULIWA

Dk. Msonde alisema baraza limeshatoa taarifa za waliohusika na udanganyifu kwa mamlaka zao za utumishi ili wachukuliwe hatua kwa mujibu wa kanuni za utumishi wa umma, huku akisisitiza kwamba halitamvumilia mtumishi yeyote anayevunja kanuni na sheria za nchi kwa kuvuruga usimamizi wa mitihani ya taifa.
“Pamoja na matokeo haya, tutafanya ufuatiliaji wa makusudi kwa wanafunzi waliofaulu ambao watachaguliwa na mamlaka za uchaguzi kujiunga na kidato cha kwanza… tutawafuatilia mwenendo wao, tutajua kama walipenya au walifaulu kwa uwezo wao kweli.
“Tukibaini mwanafunzi alifaulu kwa hujuma, tutafuta matokeo yake, kwa hiyo wakae wakijua kama walipenya huku tutawafuata huko huko juu,” alisema Dk. Msonde.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles