24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

SHERIA MPYA YA TAKWIMU MUHIMU YAJA

Na Shermarx Ngahemera


SERIKALI inatambua matatizo wanayopata watu binafsi, taasisi na serikali yenyewe kuhusu uhaba na ubora wa takwimu na hali ya usajili wa matukio  muhimu kwa maisha ya binadamu na kiraia (Civil Registration Vital Statistics , CRVS) ya vizazi, vifo na sababu zake, vilevile ndoa na  talaka hapa nchini, kwani si nzuri.

Hivyo serikali imejipanga kufanya maboresho katika kuwezesha kupatikana kwa mfumo bora wa usajili.

Waziri wa Sheria na Katiba, Palamagamba Kabudi, anasema idadi kubwa ya wananchi wamekuwa hawasajili matukio haya yanapotokea, japokuwa wengi wamekuwa na nia ya kufanya hivyo, lakini wameshindwa kutokana na sababu mbalimbali.

“Kutokana na ukosefu huo wa kumbukumbu muhimu imekuwa kawaida kinadharia kwa marehemu kutojulikana nafasi zao na kuleta  vurugu katika maisha ya wale wanaoishi kwa kukosekana vielelezo sahihi juu yao na hivyo kuendelea ‘kuishi’ na kuleta mikaganyiko maishani,” alisema Kabudi.

Alibainisha kuwa, wananchi wengi wamezaliwa na kufariki bila kuwapo kumbukumbu zao za matukio muhimu katika mfumo wa usajili wa kiserikali na kusababisha kuwapo kwa kile kinachoitwa kashfa ya kutoonekana (scandal of invisibility).

“Wananchi hawa wanaishi lakini hawaonekani katika picha kubwa ya taifa inayochorwa kwa kutumia takwimu na sababu kuu ya kwa nini hawaonekani ni kwamba hawakusajiliwa wakati walipozaliwa,” alifafanua.

Waziri Kabudi alitanabahisha kuwa, Sheria ya Usajili wa Vizazi na Vifo ina umri wa karne moja, kwani ilitungwa kuanzia ukoloni mwaka 1917 na Wajerumani na kutimia miaka mia moja mwaka huu na hivyo lazima ifanyiwe marekebisho, kwani ufanisi wake ni  mdogo mno kwa asilimia 13 tu.

Kabudi alisema pale ambapo kumbukumbu muhimu zimetamalaki kama Ujerumani na Marekani, Idara ya Takwimu ndio wanaendesha na kusimamia uchaguzi.

Sababu mbalimbali zimeelezwa kuchangia kuwapo kwa hali ya uhaba wa takwimu za kumbukumbu muhimu za maisha nchini, ikiwamo sheria, ughali wa usajili, kukosa uelewa na umbali wa utoaji huduma kutoka kwa wananchi. Alifafanua kuwa, usajili wa vizazi hufanyika mtoto anapozaliwa katika vituo vya tiba na baadaye mzazi kutakiwa kuwasilisha maombi ya kumpatia mtoto cheti cha kuzaliwa katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya.

“Wengi tunajua umbali uliopo na gharama zinazotumika kufika Makao Makuu ya Wilaya ili kuweza kupata cheti cha kuzaliwa. Kutokana na changamoto hizo, wananchi wengi wamelazimika kutowasajili watoto wao, hivyo kuongeza mrundikano wa wananchi wasio na vyeti vya kuzaliwa nchini,” alieleza Kabudi.

 

Alisema kuwa, Takwimu za Sensa za Watu na Makazi za mwaka 2012, zinaonyesha kuwa asilimia 13.4 ya wananchi ndio wamesajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa.

“Hii ni idadi ndogo na ni kiashiria kuwa serikali haina taarifa za idadi kubwa ya wananchi na hivyo kukosa vitendea kazi muhimu vya mipango na kuishi kwa makisio,” alibainisha.

Pamoja na takwimu hizo, wapo wananchi ambao huzaliwa na kufa bila hata taarifa zao kuonekana katika kumbukumbu zozote za serikali na hivyo kutishia hali ya usalama wa nchi katika ulimwengu huo uliojaa  matukio ya ugaidi.

Alieleza kuwa, hali ya usajili wa matukio ya vifo, ndoa na talaka nayo hairidhishi, pamoja na ukweli kwamba takwimu zake ni za muhimu kwa Serikali kwa kujua mwenendo wa maisha wa raia zake.

Serikali inafanya Maboresho ya CVRS katika  Mkakati wa Kitaifa wa Usajili wa Matukio Muhimu ya Binadamu na Takwimu (National Civil Registration and Vital Statistics – CRVS- Strategy), unaolenga kumuona kila mwananchi katika picha ya taifa.

Waziri Kabudi alisisitiza umuhimu wa usajili wa matukio muhimu, kwani ndio mfumo mama katika nchi yoyote, kwani husajili taarifa za mtu anapoingia duniani kwa kuzaliwa, unaweka kumbukumbu kadiri anavyokua na kupita katika hatua mbalimbali hadi kuoa na mpaka anapotoka duniani kwa kufariki.

 

“Taarifa kutoka kwenye mfumo huu hupaswa kutumika na mifumo mingine ya Serikali kama kianzio (input) kwa mifumo mingine ya Serikali kama ya uraia, utaifa na daftari la wapiga kura,” alieleza.

Umuhimu wa CVRS

CRVS inakwenda kupanua wigo wa taarifa zinazochukuliwa kuhusu matukio muhimu, kwa mfano katika kifo mfumo utapenda kujua sababu za vifo vinavyotokea.

Waziri alisema kuwa, taarifa hizi zitaisaidia serikali na wadau wengine, hasa wa sekta ya afya, kupanga mipango ya afya ya jamii kulinda rasilimali muhimu ya taifa hili.

Kuhusu uchumi, serikali imedhamiria kuukuza kupitia viwanda na hivyo kuwa na takwimu sahihi za makundi yote ya wananchi zitachochea kukua kwa sekta hii, kutokana na ukweli kwamba zitawawezesha wawekezaji kujua uhakika wa masoko ya bidhaa zao.

Alisema umuhimu wa takwimu zinazopatikana katika usajili wa matukio muhimu ya binadamu ni mkubwa sana na kama nchi, ni dhahiri kwamba tumechelewa kuanza mchakato huu.

“Usajili wa Matukio Muhimu ya Binadamu ni suala mtambuka, hivyo ni muhimu kila mdau ashirikishwe ili kuepuka kukwama katika hatua zinazofuata. Nimeongea na viongozi wa RITA na wameniambia kwamba wamekuwa wakimshirikisha kila mdau pale inapostahili, kuanzia katika hatua za awali mpaka hivi sasa na kikao cha leo ni uthibitisho tosha kwamba hili linatekelezwa.

Kupatikana mfumo thabiti wa usajili ni muhimu, kwani mfumo huu ukisimama kila mdau ataanza kunufaika, kwani kila mtu hutumia takwimu katika utekelezaji wa majukumu yake.

Alisema mchakato wa kurekebisha Mfumo wa Sheria zinazosimamia masuala ya usajili wa matukio muhimu ya binadamu umeshaanza na unaendelea vizuri.

 

Kabudi alitoa rai kwa wote wanaohusika na mchakato huo kutimiza wajibu wao ili kazi iende kwa kasi kubwa zaidi, kwani bila kubadili sheria utekelezaji wa hatua nyingine za maboresho utakwama.

Waziri aliwapongeza RITA kwa kuweza kutekeleza maboresho ya Mfumo kama jinsi Mkakati wa CRVS unavyoelekeza kupitia Mpango wa Usajili wa Watoto walio na Umri wa Miaka Mitano na kutoa mafanikio makubwa hadi mikoa mingine kwa asilimia 100.

“Kwamba mpango huu wa kudumu umeanza kutekelezwa katika mikoa saba na kuonesha mafanikio makubwa kwa kuweza kusajili watoto kwa wastani wa asilimia 77 kwa idadi ya watoto wote wa kundi hilo kwa mikoa husika, ambapo  mikoa minne kati ya hiyo imesajili watoto wa kundi hilo kwa asilimia mia moja na kazi inaendelea,” alieleza.

Alisema hayo ni mafanikio makubwa na yatatumika matokeo ya mpango huu kujifunza changamoto zilizopo katika kusogeza huduma karibu na wananchi.

“Hii ni kwenda na kauli mbiu ya CRVS, inayosema kila mtu awemo katika picha na asiachwe nyuma (Get everyone in the picture and leave no one behind) na hii inawezekana kwa kusajili kila tukio mara tu na mahali linapotokea.

Mwenyekiti wa Bodi na Mshauri wa RITA, Profesa Hamisi Dihenga, anasema Umoja wa Mataifa umeagiza kuwa ni wajibu kwa Serikali kufanya usajili wa Matukio Muhimu ya Binadamu na hivyo kiwango kidogo cha usajili ni kukosa haki za msingi za kijamii na kuzikosa ni kuharibu maendeleo na ustawi wake.

Katika usajili wa nchi za SADC hutoka Tanzania kwa asilimia 16 watoto chini ya miaka mitano  na asilimia 8.3 kwa bara la Afrika Kusini ya Jangwa la Sahara.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles