24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

SHERIA MPYA KUFUTA WAKALA WA MADINI

NA KULWA MZEE-DODOMA

WAKALA wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) inafutwa kwa mujibu wa sheria mpya ya madini.
Majukumu yake yatawekwa chini ya Kamisheni ya Madini ambayo itaanzishwa.

Hayo yalisemwa jana bungeni na Waziri wa Sheria na Katiba, Profesa Palamagamba Kabudi wakati akiwasilisha Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2017.

“Kamisheni ya Madini ambayo imependekezwa itakuwa na makamishna tisa , watatu kati yao akiwamo mwenyekiti, watakuwa wa kudumu na watashirikiana na Mtendaji Mkuu kutekeleza majukumu ya kila siku.

“Mabadiliko yanayopendekezwa katika muswada huu yanahamisha majukumu yote yaliyokuwa yakitekelezwa na TMAA na kuwekwa chini ya Kamisheni ya Madini ambako kwa msingi huo TMAA itafutwa rasmi,”alisema.

Profesa Kabudi alisema makamishna wa Kamisheni ya Madini watateuliwa kutokana na nafasi zao ambao ni Katibu Mkuu Hazina, Katibu Mkuu-TAMISEMI, Ardhi, Ulinzi na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Alisema kamisheni inayopendekezwa kuundwa itachukua majukumu ya kamishna wa madini yakiwamo kutoa, kuhuisha au itakapolazimika kufuta leseni zote zinazotolewa kwa mujibu wa shughuli za madini, ikiwa ni pamoja na kufanya ukaguzi maeneo ya migodi na kadhalika.

Waziri Kabudi alisema kupitia marekebisho hayo, vyombo mbalimbali vitaanzishwa ambavyo vitahusika katika shughuli za madini kwa niaba ya Serikali, ikiwamo kuanzisha hifadhi ya dhahabu na vito chini ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na maeneo maalum kwa ajili ya dhahabu na vito.

Kwa mujibu wa Waziri, sehemu ya tano ya muswada huo inapendekeza kufanya marekebisho katika sheria ya bima, ambayo inalenga kumpatia nguvu za sheria kamishna wa mamlaka ya udhibiti wa sekta ya bima kuainisha viwango vya chini vya ada ya bima kwa aina mbalimnbali ya bima inayotolewa na kampuni za bima.

Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mohammed Mchengerwa, alisema kamati inaishauri Serikali kuhuisha sheria nyingine kuwawezesha Watanzania kushiriki katika sekta mbalimbali za uzalishaji kuimarisha uchumi.

Alisema kamati inaendelea kuishauri serikali kuendelea kuimarisha mifumo ya ulinzi na usimamizi wa rasilimali za madini, mafuta na gesi asili Watanzania waweze kunufaika.

Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani bungeni ambaye ni Naibu Waziri Kivuli wa Sheria na Katiba, David Silinde, alisema kambi hiyo ina imani kwamba mapendekezo ya marekebisho ya sheria nyingine zilizotajwa kwenye muswada pamoja na nia njema, yamechelewa na yanaweza yasilete tija inayotegemewa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles