SHEARER AONGEZA PRESHA KWA WENGER

0
30

LONDON, England


MCHEZAJI wa zamani wa timu ya Newcastle, Alan Shearer, amesema inahitajika maelezo ya ziada kutoka kwa kocha wa timu ya Arsenal, Arsene Wenger, kwamba kwanini alishindwa kuwaanzisha washambuliaji, Alexis Sanchez  na Alexandre Lacazette, katika mchezo uliochezwa juzi dhidi ya Manchester City.

Katika mchezo huo uliochezwa Etihad, Arsenal ilifungwa mabao 3-1 na kuifanya Manchester City kusalia kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu England kwa kuwa na pointi 31 baada ya kucheza michezo 11 mbele ya wapinzani wao, Manchester United wenye pointi 24.

Lacazette  ambaye ndiye aliyesajiliwa kwa fedha nyingi katika klabu hiyo kwa sasa, anaongoza kwa ufungaji wa mabao akifunga bao sita katika msimu huu.

Katika mchezo huo, Wenger alimchezesha Sanchez  akiwa mshambuliaji pekee dhidi ya Manchester City, lakini alimwingiza Lacazette wakati timu hiyo ilipofungwa mabao 2-0 katika kipindi cha pili hata hivyo haikumchukua muda kupata bao.

Sanchez ambaye  anatarajia kujiunga na kikosi cha  Pep Guardiola baada ya kumaliza mkataba wake wa kuichezea Arsenal, Shearer anaamini Wenger  alituma ujumbe  usiofaa kwa Lacazette pamoja na wachezaji wa timu hiyo  kuhusu Sanchez kupangwa katika kikosi cha kwanza badala yake.

Shearer akihojiwa alisema: “Wenger alimuacha Lacazette wakati walipocheza dhidi ya Liverpool katika Uwanja wa Anfield, hivyo hivyo leo (juzi) wakati walipocheza na Manchester City. Unatumia pauni milioni 50 kwa kumsajili mshambuliaji wa kati ukifikiria kumtumia katika michezo mikubwa ambayo ataleta utofauti. Amefunga mabao sita, mara mbili kwa kila mchezaji wa timu hiyo, si hivyo tu bali anatakiwa kucheza sambamba na Sanchez , ni mchezaji ambaye si mchoyo na  amesajiliwa kwa pauni milioni 50.

“Si hivyo tu vipi kuhusu wachezaji wenzake? Lacazette ana haki ya kumgongea mlango Wenger asubuhi na kumweleza: ‘Hivi unachofanya si kuniwekea kikwazo au kuna jambo la ziada? Hauhitaji mimi nicheze’?”

Akiongezea katika kile alichozungumza Shearer, Ian Wright, anaamini kwamba, Lacazette anaweza kuwa katika msongo wa mawazo katika kipindi hiki akijaribu kutafakari namna atakavyoweza kumshawishi Wenger ili amwamini.

Wright alisema: “Atakuwa anafikiria sana namna ya kufanya ili kumshawishi Wenger baada ya kuona Sanchez akipangwa kikosi cha kwanza huku akiwa kwenye kiwango kibovu.”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here