30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Shaka: CCM tunashiriki uchaguzi na tutashinda

ASHURA KAZINJA-MOROGORO

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Morogoro kimetamba kujiandaa vyema na kusema kipo tayari kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji  unaotarajiwa kufanyika Novemba 24.

Kimesema kuwa uchaguzi huo ndio kitovu cha kushika hatamu za utawala wa dola, hivyo kitaheshimu sheria na matakwa ya demokrasia na ni kipimo cha kuaminiwa kwa vyama vya siasa kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka 2020.

Hayo yalisemwa jana mjini hapa na Katibu wa CCM Mkoa wa Morogoro, Shaka Hamdu Shaka, wakati akitoa tathmini ya uchukuaji fomu za kuomba kuteuliwa na chama kugombea nafasi ya vitongoji, alipokuwa akizungumza na viongozi wa kata, matawi na mashina mjini hapa.

Shaka aliwataka viongozi hao waendelee kujipanga kwa kufuata kanuni, taratibu za kisheria na kikatiba zilizowekwa na Serikali.

Alisema kila kiongozi wa CCM ana wajibu wa msingi kuhakikisha chama kinapitisha wagombea wenye weledi na sifa, wanaokubalika kwa jamii na watakaokuwa tayari kuwatumikia wananchi.

Shaka alisema wakati uchaguzi huo ukifanyika Novemba, Serikali za CCM zimejitahidi vya kutosha kuimarisha huduma za kiwajibu kwa jamii, kuinua uchumi na kushughulikia kero sugu na kuzitatua.

“Nawapongeza sana makatibu wa wilaya, kata na matawi. Hamasa na mwitikio kwa wana-CCM umekuwa mkubwa katika kuchukua fomu za vitongoji ndani ya chama, tunaendelea kusisitizana kuwa uchaguzi huu ni muhimu kwa mustakabali wa chama.

“Mtendaji yeyote wa chama atakayezembea atahesabiwa ni msaliti na amekihujumu chama, usaliti na hujuma si sifa njema, bali ni dhambi isiyosameheka,” alisema Shaka.

Aidha aliwakumbusha watendaji hao wa chama muda wote kuzingatia maelekezo ya kikanuni na kisheria kuhusu usimamizi na kufuata taratibu, miongozo na kanuni za chama na Serikali ili kutimiza dhana ya demokrasia kivitendo.

“Viongozi wa kata, matawi chama na jumuiya sambamba na viongozi wa chama ngazi za vijiji, mitaa na vitongoji lazima msimame pamoja na mfanye kazi usiku na mchana bila kuchoka, wote kwa umoja wenu na mshikamano mjitume kama wafanyavyo siafu ili tushinde vizuri ili kulinda heshima ya Rais Magufuli mbele ya macho ya dunia,” alisema.

Alisema CCM inajua ina sifa za kushinda kwakuwa siku zote imekuwa mstari wa mbele kuheshimu na kufuata taratibu, lakini mahasimu wao kisiasa alidai wanajiandaa kwa ulalamishi na uzushi wa kutengeneza baada ya kupotezea mwelekeo na kupoteza dira kisiasa.

Aliwaeleza watendaji wake kazi na dhamana ya kuwatumikia wananachi imepewa CCM, hivyo kuwaachia wengine hatua hiyo itahesabika ni makosa kisiasa, kiufundi na kihistoria

“Tunashiriki uchaguzi kwa kujiamini tutashinda kwa haki usawa na amani. CCM Mkoa wa Morogoro tunaahidi kufuata taratibu zote za kikanuni na kikatiba, tutakaposhindwa tutaheshimu matokeo na wenzetu pia wawe waungwana wa kutii matakwa na uamuzi wa wananchi,” alisema Shaka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles