30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Shahidi kesi ya akina Mbowe adai kuporwa na polisi

Kulwa Mzee – Dar es Salaam

MWANAFUNZI wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Lumola Kahumbi (30), amedai askari wa Kituo cha Polisi Oysterbay alichukua hela zake Sh 12,500, mwingine akamwambia ajiongeze naye akatoweka akiwa njiani kuelekea chooni alikokuwa anapelekwa.

Shahidi huyo wa utetezi amedai alikuwa chini ya ulinzi kituoni hapo, akaomba kwenda chooni, akiwa huko askari mmoja akamwambia jiongeze huku mwingine akizamisha mkono mfukoni kwake na kutoka na kiasi hicho cha fedha akabakiwa na Sh 200.

Shahidi huyo wa 13 wa upande wa utetezi alidai hao jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba

Alidai alikamatwa na askari eneo la Kinondoni Studio na kupelekwa Kituo cha Polisi Oysterbay Februari 16 mwaka 2018, mfukoni alikuwa na Sh 12,700.

“Tuliambiwa kama kuna mtu anataka kujisaidia aseme, mimi nikataka kwenda, nilisindikizwa na polisi wawili,  kabla hatujafika chooni chini ya mwembe askari mmoja akaniambia  jiongeze, mwingine akanisachi na kuchukula Sh 12,500 kisha akaniambia niondoke na nisigeuke nyuma. 

“Februari 16,2018 nilitoka chuo na kupanda daladala la Kariakoo/ Makumbusho kwenda Kinondoni Studio kumuona shangazi yangu saa moja na nusu usiku, niliposhuka studio nilielekea nyumba ya nne kwa shangazi,”alidai.

Alidai akiwa kwenye daladala aliona magari ya polisi na yalipofika usawa wa kituo cha daladala cha studio, waliruka kutoka kwenye gari zao wakati huo katika barabara hiyo ya Kawawa wananchi walikuwa wakiendelea na shughuli zao na kwamba ule msafara wa gari za polisi ulileta taharuki.

Shahidi huyo wa utetezi alibainisha kuwa katika kituo cha daladala cha studio wakati wa tukio hilo kulikuwepo na gari za daladala tatu zikipakia abiria na kondakta wa gari moja wapo alikamatwa.

Alidai askari walipoanza kukimbiza watu na kuwakamata alikimbia kuelekea Magomeni lakini alipofika eneo la wauza vitanda askari walimkamata.

Wengine walikamatwa wauza viwanda na wateja wao na walikimbia baada ya polisi kuonesha kama kuna kitu wanafanya wananchi wakataharuki na kuanza kukimbia.

Alidai kwamba walikamatwa watu wengi na gari nyingi za polisi zilijaza watu ambapo walipofika katika Kituo cha Polisi Osterbay wote waliwekwa eneo la nje ya geti chini ya mwembe na wengine waliwekwa ndani ya geti.

Alidai geti lilipofunguliwa walipata wasaa wa kuonana kwa muda wa nusu saa na wakiwa hapo askari waliwapiga kwa kutumia mikanda.

Shahidi alidai mmoja kati ya askari hao alitoka ndani ya kituo hicho cha polisi akiwa na ngoma akampa mmoja wao aipige na kuwalazimisha waimbe wimbo wenye maneno ‘dola si lelemama’.

Kahumbi alidai ndani ya dakika 20 kuna askari aliwaambia wanaotaka kakwenda chooni wajitokeze na yeye alikuwa miongoni kwa waliojitokeza kutaka kwenda chooni.

Wakati akielekea chooni walipofika eneo la chini ya mwembe askari ndipo akanyang’anywa hela aliyokuwa nayo akabaki na Sh 200.

Alidai kwa kuwa Sh 200 nilikuwa haitoshi nauli, aliondoka kwa miguu kutoka kituo cha polisi Osterbay hadi DIT.

Baada ya ushahidi huyo kueleza hayo, Wakili wa Serikali Salim Msemo, alimuuliza awali kuwa ni kweli mwanachama wa chama cha siasa na asiye mwanachama wanatofautishwa kwa kadi na hizo kadi zina namba na akajibu ni sahihi.

Alidai  hakuna uthibitisho wowote ambao ameutoa mahakamani kuthibitisha ni mwanachama wa CCM kama anavyodai katika ushahidi wake.

Shahidi wa 14 Shabani Othman anaendelea kutoa ushahidi ambapo alidai alikuwa wakala wa Chadema katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kinondoni na baada ya kuapa hakupewa kiapo  hadi Februari 17 asubuhi siku ya uchaguzi.

Mbowe na wenzake nane wanashtakiwa kwa mashtaka 13 yakiwemo ya uchochezi na kufanya maandamano haramu Februari 16 mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles