30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

SETH WA ESCROW AELEZA ALIVYOKAMATWA ‘KIMAFIA’ NA WATU WASIOJULIKANA

*Adai walimfunika uso na kumpeleka asipopajua

NA KULWA MZEE -DAR ES SALAAM

MWENYEKITI Mtendaji wa PAP, Harbinder Singh Sethi, amedai kwa mara ya kwanza alivyokamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, alifunikwa uso na kitambaa na kupelekwa mahali kusikojulikana, huku waliomkamata wakiwa na silaha.

Amedai hayo katika maombi yake aliyowasilisha Mahakama Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.

Sethi kupitia wakili wake, Joseph Makandege, aliwasilisha maombi hayo jana mbele ya Jaji Winifrida Koroso, akiwa ameambatanisha na hati ya kiapo.

Katika maombi hayo, ameiomba mahakama hiyo kumpa dhamana kwa sababu ni mgonjwa, anahitaji kuwa chini ya uangalizi wa wataalamu vinginevyo, kuna uwezekano mkubwa wa kupoteza maisha yake.

Alivyokamatwa

Katika hati ya kiapo, anadai Juni 17 akiwa Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere ili kusafiri kwenda Afrika Kusini kwa matibabu, alikamatwa na kufunikwa uso kisha kushambuliwa na baadaye alipelekwa mahali kusikojulikana na watu wenye silaha.

Sethi anadai Juni 19 alipelekwa Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam (Central), kisha mahakamani kushtakiwa pamoja na Mkurugenzi wa VIP Engineering, James Rugemarila kwa uhujumu uchumi na Julai 17 walibadilishiwa mashtaka na kuwekewa mashtaka sita ya kutakatisha fedha.

“Kutokana na shauri hili naamini makosa hayana dhamana, lakini katika mazingira kadhaa mahakama inaweza kuchepuka katika msimamo huo wa kisheria na kutoa dhamana.

“Sababu ya kuomba dhamana ni ugonjwa, mteja wangu anatakiwa kuwa chini ya uangalizi wa wataalamu, bila kufanya hivyo kuna uwezekano mkubwa wa kupoteza maisha na hivyo kushindwa kuendelea na kesi,”alidai Makandege.

Sababu ya kuwekewa maputo

Makandege alidai mshtakiwa huyo alifanyiwa upasuaji mara mbili ambapo mara ya kwanza ni mwaka 2016 na mara ya pili mwaka huu Afrika Kusini na kuwekewa puto.

Alielezea sababu ya kukabiliwa na matatizo hayo kuwa ni ajali aliyopata kati ya mwaka 1994-1995 nchini Namibia , mapafu yake yaliathirika ambapo madaktari walichukua saa kadhaa kunusuru maisha yake.

Anadai mwaka 2015 mapafu yake yalishindwa kufanya kazi, akapatiwa matibabu na matatizo hayo anatakiwa kila mwezi kwenda Afrika Kusini kuangalia afya yake.

“Kuna kifaa maalum ambacho mshtakiwa anatakiwa kutumia kwa ajili ya kumsaidia kupumua usiku, kashindwa kukipata kwa sababu magereza wanazuia mahabusu ama wafungwa kuwa na kifaa hicho na yenyewe (Magereza)  haina uwezo wa kumpatia kifaa hicho,”anadai Makandege.

Makandege aliomba mahakama ikubali kumpa dhamana mteja wake kwa sababu za ugonjwa na kwamba anao wadhamini wa kuaminika na yuko tayari kutimiza masharti ya dhamana.

Serikali yapinga

Wakili wa Serikali Mkuu, Dk. Zainabu Mango, aliwasilisha pingamizi la awali akidai hati ya kiapo ina upungufu hivyo aliomba maombi itupe maombi yaliyowasilishwa mbele yake.

Jaji Koroso, aliahirisha maombi hayo namba 29/2017 hadi Septemba 29 kwa ajili ya kutoa uamuzi.

Makosa ya Sethi na Rugemarila

Sethi na Rugemarila wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi, kutakatisha fedha na kuisababishia Serikali  hasara ya Dola za Marekani milioni 22 na Sh bilioni 309.

Washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka  12 ya  uhujumu uchumi  kwa kula njama, kujihusisha mtandao wa uhalifu , kughushi,  kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu,  kutakatisha fedha  na kuisababisha Serikali hasara ya Dola za Marekani 22, 198,544.60 na Sh 309,461,300,158.27.

Katika shtaka la kwanza inadaiwa, Rugemarila   na Sethi kati ya Oktoba 18 ,2011 na Machi 19 , 2014 jijini Dar es Salaam walikula njama katika nchi za Afrika Kusini, Kenya na India ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Shtaka la pili wanadaiwa kujihusisha na mtandao, washtakiwa wote kati ya Oktoba 18,2011na Machi 19,2014 jijini Dar es Salaam wakiwa siyo watumishi wa umma na watumishi wa umma  walitekeleza mtandao huo wa uhalifu kwa lengo la kujipatia faida.

Kwa upande wa shtaka la tatu, Sethi  anadaiwa  kuwa   Oktoba 10, 2011 katika mtaa wa Ohio Ilala DSm akiwa na nia ya ulaghai alighushi fomu namba 14 a ya usajili wa makampuni  na kuonesha yeye ni mtanzania anayeishi Kitalu namba 887 Mtaa wa Mrikau Masaki wakati akijua ni uongo.

Seth katika shtaka la nne anadaiwa kutoa nyaraka ya kughushi ambayo ni fomu namba 14 ya usajili wa kampuni kwa Ofisa Msajili wa Kampuni, Seka Kasera kwa njia ya kuonesha kwamba yeye ni Mtanzania na Mkazi wa Mtaa wa Mrikau.

Katika shtaka la tano, washtakiwa wote, wanadaiwa kati ya  Novemba 28/29, 2011 na Januari 23,2014 Makao Makuu Benki ya Stanbic Kinondoni  na Benki ya Mkombozi tawi St. Joseph  kwa ulaghai walijipatia kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh 309, 461,300,158.27.

Katika shtaka sita la kusababisha hasara, washtakiwa wanadaiwa kuwa   Novemba 29, 2013 katika Benki ya Stanbic tawi la  kati Kinondoni kwa vitendo vyao waliisababishia Serikali hasara ya Dola za Marekani 22, 198, 544.60 na Sh 309,461,300,158.27.

Katika shtaka la saba, inadaiwa kati ya Novemba 29, 2013 na Januari 23, 2014 maeneo tofauti Dar es Salaam kwa pamoja walitenda kosa la kutakatisha fedha kwa kuchukua fedha kutoka BoT Dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh 309,461,300.27 wakati wakijua fedha hizo zao la kujihusisha na genge la uhalifu.

Shtaka la nane, wanadaiwa Novemba 29,2013 katika tawi la kati la Benki ya Stanbic Tanzania Wilaya ya Kinondoni, Sethi alitakatisha fedha kwa kuchukua BoT Dola za Marekani 22,198,544.60 wakati akijua fedha hizo zimetokana na zao la kujihusisha na genge la uhalifu.

Kwa upande wa shtaka la tisa, Sethi anadaiwa kuwa kati ya Novemba 29, 2013 na Machi 14,2014 katika tawi la kati la Benki ya Stanbic Kinondoni Dar es Salaam alitakatisha fedha, Sh 309,461,300,158.27 kutoka BOT wakati akijua fedha hizo zimetokana na zao la kujihusisha na genge la uhalifu.

Shtaka la kumi,  inadaiwa Januari 23, 2014 katika Benki ya Mkombozi tawi la St Joseph Cathedral, Rugemarila alitakatisha fedha, Sh 73,573, 500,000 kutoka kwa Sethi wakati akijua fedha hizo zimetokana na zao la kujihusisha na genge la uhalifu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles