28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yatoa mwongozo Uchaguzi Serikali za Mitaa

  • Jafo asema mbwembwe ruksa wakati wa kuchukua fomu

Waandishi wetu –Dodoma/Dar es salaam

SERIKALI imetoa mwongozo wa uchukuaji fomu za kuwania nafasi mbalimbali katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa zinazoanza kutolewa leo.

Katika mwongozo huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, amesema ni marufuku kufanya kampeni katika kipindi hicho.

Pia amevitaka vyama vya siasa kutumia demokrasia vizuri kwa kuchagua na kuwapeleka wale waliowakusudia ikiwa ni pamoja na kuwadhamini.

Nafasi zinazogombewa katika uchaguzi huo, ni  mwenyekiti wa kitongoji katika mamlaka za miji  midogo, mwenyekiti wa mtaa na wajumbe wa kamati ya mtaa (kundi mchanganyiko la wanawake na wanaume) na wajumbe wa kamati ya mtaa (kundi la  wanawake) katika mamlaka za miji.

Nafasi nyingine ni mwenyekiti wa kijiji, wajumbe wa halmashauri kuu ya kijiji (kundi mchanganyiko wanaume na wanawake), wajumbe wa halmashauri kuu ya kijiji (kundi la wanawake) na wenyeviti wa vitongoji katika mamlaka za wilaya.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Jafo alisema uchukuaji fomu za kugombea nafasi mbalimbali utaanza leo kwa fomu kutolewa katika ofisi ya mitaa na vijiji.

Jafo alisema uchukuaji huo utadumu kwa siku 7 hadi Novemba 4 na uchaguzi unatarajiwa kufanyika Novemba 24.

Akizungumza jana, Jafo aliruhusu kuwapo na mbwembwe za kila aina katika uchukuaji fomu, lakini akatahadharisha zisiwe zenye viashiria vya kufanya kampeni.

“Utaratibu tumesema fomu zitatolewa katika ofisi za mitaa na kijiji, umezungumza suala la mbwembwe, naomba niwaambie kampeni kabla ya uchaguzi hairuhusiwi, kwa hiyo naamini hata watu wakileta mbwembwe za aina yoyote, lakini mbwembwe zile zisiwe katika ‘style’ ya kampeni, maanake mtu huwezi kumzuia kuchukua fomu kwa ‘style’ ambayo anaitaka.

“Lakini isije ikawa katika ‘style’ ya kampeni, mtu kusindikizwa na rafiki zake haina shida,” alisema.

KUCHUKUA NA KUREJESHA FOMU

Jafo alisema kumekuwa na mkanganyiko katika vyama vya siasa, kuhusu muda wa kuchukua na kurejesha fomu.

Kuhusu hilo alisema mgombea anaweza kuchukua na kurejesha fomu muda huo huo ama kurejesha muda atakao yeye ndani ya siku saba tangu leo hadi Novemba 4. 

“Mwanzo kulikuwa na mkanganyiko katika vyama vya siasa wakisema kwamba kuchukua fomu ni siku ya tarehe 29 peke yake halafu kurudisha kuanzia tarehe 29 mpaka tarehe 4.

“Kuchukua na kurudisha mtu anaweza kuchukua fomu kesho na akarejesha kesho hiyo hiyo, anaweza kuchukua  na akataka kurudisha keshokutwa, lakini kipindi hiki cha siku saba ndio cha kuchukua na kurejesha fomu katika nafasi mbalimbali,” alifafanua.

WATANZANIA WENYE SIFA

Jafo aliwataka Watanzania wenye sifa kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali kwa kutumia vyama ambavyo vina usajili wa kudumu.

“Imani yangu kubwa wale Watanzania wenye nia ya kushika nafasi mbalimbali katika mamlaka za Serikali za Mitaa, sasa huu ndio muda mwafaka wa kufanya hivyo kupitia vyama vyao vyenye usajili wa kudumu,” alisema.

WAGOMBEA NA WASIMAMIZI

Jafo aliwataka wagombea na wasimamizi wa uchaguzi kufuata kanuni taratibu na sheria katika kipindi cha uchukuaji wa fomu.

“Na tulisema kipindi hiki ni kigumu na watu wazingatie kanuni. Imani yangu watu watafuata misingi yote ya kanuni. Wasimamzi wa uchaguzi watasimamia jambo hili, lengo ni kila mtu apate haki yake ya kikatiba.

“Imani yangu wasimamizi wa uchaguzi wakati huu hakutaingia na changamoto zozote, tunataka kila mtu apate haki yake,” alisema.

WAKUU WA MIKOA NA WILAYA

Jafo aliwataka wakuu wa mikoa na wilaya kusimamia amani katika maeneo yote ambayo utafanyika  uchaguzi.

“Niwaombe wakuu wa mikoa na wilaya ambao ni wasimamizi wa amani, kusimamia jambo hili kwa kuhakikisha kunakuwa na utulivu na watu watimize matakwa yao,” alisema Jafo.

ANGALIZO VYAMA VYA SIASA

Kwa upande wa vyama vya siasa, Jafo alivitaka kutumia demokrasia vizuri kwa kuchagua na kuwapeleka wagombea waliowakusudia ikiwa ni pamoja na kuwadhamini.

“Tumieni vizuri demokrasia kwa kuhakikisha mnawapeleka wale watu ambao mnawakusudia pamoja na kuwadhamini kama sheria inavyoelekeza.

“Hatutarajii kutokee changamoto yoyote kwani watu ambao hawakuelewa waliomba ufafanuzi na hivi karibuni niliweza kutoa ufafanuzi kwa vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu jinsi ya kuchukua fomu na kurejesha.

“Imani yangu kwa sababu wao walitaka ufafanuzi wa aina mbalimbali, utakuwa umetusaidia kwa kiasi kikubwa na zoezi hili litaenda vizuri,” alisema Jafo.

MAJUKUMU KIPINDI CHA MPITO

Katika hatua nyingine Jafo alisema baada ya nafasi za uenyekiti wa vijiji au mtaa muda wao kuisha, wametoa maelekezo.

Alisema maelekezo hayo ni kwamba majukumu ambayo yanapaswa kuamuliwa na kijiji ama mtaa, mtendaji wa kijiji anapaswa kupeleka kwa mtendaji wa kata na mtendaji wa kata atapeleka kwa mkurugenzi na atatafakari namna bora ya nini kifanyike.

NAFASI ZILIZOKUWA WAZI

Kuhusu nafasi za maofisa tarafa, watendaji wa mitaa na vijiji kukosa watu, Jafo alisema zimeishazibwa na sehemu ambako wanakosekana kuna utaratibu wa watu kukaimu.

“Nafasi nyingi ambazo zilikuwa wazi zimeweza kuzibwa za watendaji, maofisa tarafa zote zimezibwa, nafasi za watendaji wa kata zote zimezibwa, nafasi za wenyeviti za vijiji nyingi zimezibwa na hata pale tunapochelewa na haijazibwa nafasi hiyo tumeiziba kwa mtu kukaimu,” alisema Jafo.

ELIMU YA URAIA NA UANGALIZI

katika hatua nyingine, mashirika yasiyo ya kiserikali ya Action for Change (ACHA) na The Right Way (TRW),  yamepanga kutoa elimu ya uraia na uangalizi wa  uchaguzi huo.

Lengo la mpango huo,  utakaozinduliwa Ijumaa ijayo, ni kufanya uchaguzi kuwa huru, haki na wenye kuaminika kwa Watanzania.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa TRW, Sebastian Masaki, alisema asasi hizo zimeungana baada ya kupata kibali cha kuendesha shughuli hizo kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

“Asasi hizi zina mwelekeo wa kufanya shughuli zinazofanana, hususan za uchaguzi kikatiba kwa kuhakikisha uendeshaji bora na michakato ya uchaguzi na uungaji mkono wa mabadiliko ya kiutawala kupitia elimu ya uraia.

“Muungano huu utakuwa chombo ambacho kitapunguza gharama na kuchangia thamani ya pesa na kuongeza mbinu za kiufundi na mtaji wa watu kuelekea shughuli hii.

“Tunatamani kuona mchakato wa uchaguzi ambao unaongozwa na wananchi, kwa maana ya ushirikishaji, yenye uwazi, huru na haki na unaoaminika juu ya misingi ya haki na uwajibikiji,” alisema Masaki.

Alisema elimu hiyo itatolewa kupitia vyombo vya habari na mawasiliano ya aina nyingine.

“Uangalizi au uchambuzi wa mifumo ya uchaguzi vitakwenda sanjari ili kuziwezesha ACHA na TRW kubaini ukiukwaji wa kanuni za mchakato wa uchaguzi,” alisema Masaki.

Kwa upande mwingine, alisema ushirikiano wa ACHA na TRW unalenga kuona mchakato wa uchaguzi unafuata viwango vya kimataifa, kama ambavyo Tanzania imeridhia na zile zilizopo kwenye sheria za manispaa, kanuni na miongozo kutoka vyombo mbalimbali vya kusimamia uchaguzi, yaani Tume ya Uchaguzi na vyombo vya kisheria vya kimataifa.

“Pia, kutakuwa na uwazi utakaoshirikisha makundi maalumu; wenye ulemavu, wanawake, vijana na wazee.

“Ni dhahiri kuwa uangalizi wa uchaguzi huo utafanyika kwa kutumia vifaa vya teknolojia ya kisasa na mafunzo bora yatakayotolewa katika nyadhifa zote wakati na baada ya uchaguzi.

 “Waangalizi wa muda mrefu 215 watakaopewa jukumu hili ngazi ya majimbo na waangalizi wa muda mfupi 3,600 watapelekwa kwenye vituo mbalimbali vya uchaguzi nchi nzima,” alisema Masaki.

Habari hii imeandaliwa na RAMADHAN HASSAN (DODOMA), FERDNANDA MBAMILA Na BRIGHITER MASAKI (DAR ES SALAAM)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles