23.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

SERIKALI YATOA MASHARTI MAZITO

JOHANES RESPICHIUS -DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema serikali itanunua dawa zinazotengenezwa na wawekezaji wa hapa nchini kwa kuzingatia ubora, usalama na ufanisi.

Waziri Mwalimu alitoa masharti hayo jana kwenye hafla ya uzinduzi wa Maabara zinazohamishika uliofanyika kwenye ofisi za Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), Dar es Salaam.

Alisema baada ya  Serikali kuhimiza ujenzi wa viwanda nchini itaanza kununua dawa zinazotengenezwa na viwanda vya ndani lakini kwa wekezaji waliotimiza vigezo.

Waziri Mwalimu alisema uzinduzi wa maabara hizo ni moja ya jitihada zinazofanywa na serikali kuondoa bidhaa na dawa bandia ili kuokoa maisha ya raia wake

“TFDA imeendeleza mpango mahsusi wa uchunguzi wa awali wa dawa ulionza 2002 katika baadhi ya hospitali za mikoa na vituo vya forodha kwa dawa muhimu za kifua kikuu, dawa za kufubaza virusi vya ukimwi (ARVs) na viua sumu (antibiocs).

“Hatua hii ya kununua maabara zinazohamishika 10 na kufikia 25 kote nchini inalenga kuimarisha nguvu katika kudhibiti ubora na usalama wa dawa zinazoingia na zilizoko sokoni.

“Na niweke wazi kwamba Serikali haitanunua dawa za ndani ambazo hazikidhi vigezo,” alisema Mwalimu.

Aidha Waziri Mwalimu aliitaka TFDA kutowaone aibu na kuwaogopa wawekezaji ambao wataleta dawa bandia bali iwachukulie hatua stahiki bila kujali gharama za mzigo wenyewe.

“Wawekezaji walete dawa zenye ubora unaotakiwa hivyo TFDA hata mtu akileta mzigo wa bei ya juu kiasi gani kama hauna ubora msimwonee aibu.

“Lakini pia TFDA msikwamishe wawekezaji bali muwe sehemu ya kuwezesha ufikiaji wa uchumi wa viwanda nchini,” alisema Mwalimu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TFDA, alisema maabara hizo 10 zimegharimu Sh milioni 100 na kwamba hivi sasa maabara hizo zimefikia 25 kutoka 15 mwaka 2012/13.

 

Alisema maabara hizo zitapelekwa katika ofisi za kanda tatu za Tabora (Magharibi), Mbeya (Nyanda za juu Kusini) na Mtwara (Kusini) na vituo vya forodha Namanga, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa (KIA), Sirari na Mutukula na katika Bandari ya Dar es Salaam na kwamba maabara nyingine mbili zitapelekwa katika mikoa ya Geita na Katavi.

“Kutokana na kuongezeka kwa idadi ya maabara hizo, uwezo wa kubaini dawa duni na bandia umeongezeka na imewezesha idadi ya dawa duni kushuka kutoka asilimia 3.7 2005 hadi chini ya asilimia 1 mwaka 2017,” alisema.

Alisema TFDA ilimebaini dawa bandia zilizodaiwa kuwa na viambata vya Ampicillin, Erythromycin, Quinine Sulphate, Metronidazole na dawa ya mseto ya Metakelfin.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles