SERIKALI YATAKA WANANCHI WASILAZIMISHWE NJIA YA KULIPWA FIDIA YA ARDHI

0
961

Mwandishi Wetu, Dodoma


Serikali imezielekeza Mamlaka za Upangaji kutowalazimisha wananchi kutumia njia moja ya kulipa fidia badala yake wananchi washirikishwe kuchagua njia wanayoona inafaa kati ya kuingia ubia au kulipwa fidia wakati wa kuuziana ardhi kwa manispaa.

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula, amesema hayo bungeni jijini Dodoma leo Ijumaa Septemba 7, wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Fakharia Khamis, aliyetaka kujua ni kwanini wananchi wanalazimishwa kuuza maeneo yao kwa manispaa na kulipwa bei ndogo badala ya kufanya zoezi hilo kwa ubia.

“Kwa sasa kumekuwa na wimbi kubwa la upimaji viwanja kwenye manispaa mbalimbali nchini, kwa sababu maeneo mengi ni mashamba, je, serikali haioni kufanya hivyo kunasababisha Watanzania kukosa kazi maana asilimia 75 ni wakulima,” amehoji mbunge huyo.

Akijibu swali hilo, Mabula amesema Sheria ya Mipango Miji Na.8 ya Mwaka 2007 inaelekeza kuwa eneo lolote likishatangazwa kuwa eneo la upangaji (planning area) linapaswa kupangwa kwa kuzingatia sheria ya upangaji mijini.

“Wananchi wanaokutwa kwenye maeneo hayo wanatakiwa kutambuliwa, kuelimishwa na kushirikishwa katika hatua zote za upangaji hadi umilikishaji.

“Aidha, Sheria ya Utwaaji Ardhi ya Na.47 ya mwaka 1967 pamoja na mambo mengine inazipa Mamlaka za Upangaji uhalali wa kutwaa ardhi iliyopangwa au inayohitaji kupangwa kutoka kwa wamiliki na kuwalipa fidia kwa kufuata miongozo ya ulipaji fidia,” amesema Mabula.

Amesema Sera na Sheria ya Ardhi zinaelekeza umuhimu wa kutathmini ardhi na maendelezo ya wananchi waliokutwa nayo na kulipa fidia sambamba na kupima na kumilikisha kwa makubaliano yatakayoridhiwa na pande zote mbili bila kuathiri sheria.

“Hata hivyo, uzoefu unaonyesha kuwa mamlaka za upangaji hupenda kutumia njia ya kulipa fidia ya ardhi na maendelezo hali ambayo imeleta malalamiko mengi kutoka kwa wananchi, hivyo serikali inazielekeza mamlaka za upangaji kuwashirikisha wananchi wachague njia wanayoona inafaa,”amesema Mabula.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here