24.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

SERIKALI YATAKA MAPINDUZI BIASHARA YA NGOZI

Na Mwandishi wetu


IKISIMAMA kidete kwa azma yake ya  kufanya nchi kuelekea uchumi wa viwanda, Serikali inasisitiza uongezaji wa thamani katika biashara ya ngozi ili kuongeza ajira na ukuaji uchumi wa nchi.

Kupeleka ngozi ghafi nje ni kuhamisha ajira nchini na kufifisha juhudi za kujitoa katika lindi la umasikini ambalo watu wengi wa Tanzania wamo bila sababu ya msingi kuwako huko katika nchi iliyobarikiwa rasilimali nyingi.

Mkakati mkuu wa Serikali katika Awamu ya Tano ni kufanya  nchi kuwa Taifa la viwanda  ambayo ni njia mahsusi ya kupambana na umasikini kwa uhakika.

Kilimo ni sekta  muhimu na sekta ya ngozi  ni mojawapo ya  idara yake na hivyo wadau wametakiwa kuchakata ngozi nchini ili kuongeza kipato badala ya kuzisafirisha nje zikiwa ghafi.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa  Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Mhandisi Christopher Chiza ambaye awali  aliwahi kuwa Waziri wa Kilimo na Ushirika,  alisema  kwa Watanzania huu ndio wakati wa kuchangamkia  fursa zinazojitokeza  katika biashara hiyo.

Akizungumza na wadau wa ngozi, alisema fursa hizo ni pamoja na kutoruhusu   kupeleka ngozi ghafi nje ya nchi, kwani tunapoteza vitu vingi kwa kufanya  hivyo ikiwemo ajira na kipato kitokanacho na bidhaa hii muhimu katika maisha ya binadamu.

Aliainisha kwa takwimu umuhimu wa sekta ya mifugo na uwezekano mkubwa wa nchi ya Tanzania kufanya vizuri katika kukuza uchumi wake.

 “Kwa takwimu za mwaka  2015, Tanzania ilikuwa ya pili kwa idadi ya mifugo barani Afrika baada ya Ethiopia, tulikuwa na ng’ombe milioni 16.7 lakini sekta ya ngozi haijachangia vya kutosha kwenye uchumi wetu sababu kubwa ni kusafirisha ngozi ghafi kwa wingi, kukosa mafunzo ya ufugaji bora, uchunaji na bidhaa zinazokidhi viwango,” alisema Chiza kwa masikitiko makubwa.

Chiza alibainisha vipande vya ngozi vilivyozalishwa nchini kwa mwaka 2015, kuwa ni vipande milioni 3.1 vya ngozi ya ng’ombe, vipande milioni 2.8 vya ngozi ya mbuzi na kondoo vipande 550,000 vyote vikiwa na thamani ya jumla ya Sh bilioni 33.

Alisema kati ya hivyo, vipande vya ngozi yenye thamani ya Sh bilioni 76.3 ilisafirishwa nje katika mataifa ya Uturuki, Italia, Hong Kongo, Pakistan, India, Singapore na China. Hata hivyo, vipande 250,000 tu ndivyo vilivyobaki nchini na kufanywa bidhaa zilizokuwa na thamani ya Sh bilioni 12.5 na kuthibitisha kuwa mali hiyo iliongezeka thamani kubwa ukifananisha na ile iliyouzwa ghafi.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Edwin Rutageruka, alisema sababu ya kuandaa semina hiyo ni kuongeza ujuzi wa wadau wa bidhaa za ngozi nchini ili kuongeza ajira na ufanisi hasa kwa vijana. 

“Mbali ya kujua umuhimu wa ngozi, pia tunataka wafanyabiashara watambue umuhimu wa kurasimisha biashara zao na kulipa kodi.

“Sekta ya ngozi ni ya kipaumbele ikiwemo nyingine kama asali na nta  pamoja na nguo. Vilevile tunataka watambue thamani ya ngozi inaanzia kwenye kuchunga, uchinjaji na uchunaji. Kila siku tunatoa elimu kuwa wachungaji wasiweke majina kwenye miili ya mifugo inapunguza thamani ya ngozi badala yake waweke alama vichwani,” alisema Rutageruka.

Akizungumzia  kuhusu suala la ubora wa ngozi, Mwenyekiti wa Tantrade  alisema ipo haja wadau wa ngozi wakaanza kuangalia namna bora ya kuzuia vurugu zinazotokana na wafugaji na wakulima ili kulinda  rasilimali ya mifugo.

“Hiki kiatu nilichovaa nimepewa zawadi na Jeshi la Magereza, ni kizuri sana na hii inaonyesha namna Taifa letu lilivyo na ngozi bora, lakini tunafanyaje kulinda thamani hii, lazima tuzuie mapigano au vurugu za wafugaji na wakulima, zinasababisha kupoteza mifugo na wakati mwingine mifugo inashambuliwa kwa silaha inapata majeraha,” alisema.

Katibu wa Chama cha Watengenezaji bidhaa za ngozi Tanzania (Talepa), Timothy Futo, alisifia  mafunzo hayo  na kusema: “Hapa tumefika washiriki 25 ambao tunaamini baada ya mafunzo haya tutasambaza elimu kwa wengine nchi nzima.

“Tulikua na tatizo la kujua masoko na elimu juu ya masuala ya kodi pamoja na kusajili kampuni, lakini tunashukuru leo ni siku ya pili ya mafunzo lakini kuna mengi tumepata,” alisema.

“Biashara za ngozi ni mali ulimwengu mzima,” alihitimisha Chiza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles