25.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yataifisha mali za Wakili Mwale

Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Biswalo Mganga (kulia) akikagua magari yaliyokuwa yanamilikiwa na wakili Median Mwale mkoani Arusha jana, yaliyotaifishwa na Serikali.

* Zote zina thamani zaidi ya Sh bilioni 1

Janeth Mushi -Arusha

MALI za Wakili Median Mwale aliyekuwa akikabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi zimetaifishwa na Serikali na kukabidhiwa kwa Ofisi ya Hazina.

Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Biswalo Mganga, aliyeongozana na baadhi ya maofisa wa Hazina akiwamo Benezeth Ruta ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Mali za Serikali, walizikagua mali hizo yakiwamo magari sita ya kifahari nyumba mbili na shamba vyote vyenye thamani zaidi ya Sh bilioni 1.197 na zitapangiwa matumizi baadaye.

DPP alisema katika kesi ya maombi ya jinai namba 100 ya mwaka jana iliyokuwa kati ya DPP dhidi ya Mwale, Aprili 14, mwaka huu Mahakama Kuu ilitoa amri ya kutaifishwa kwa mali hizo.

Mwale ambaye ni wakili maarufu jijini Arusha, alitiwa hatiani baada ya kukiri makosa 30 yakiwamo ya kutakatisha fedha haramu na kughushi.

Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ilimtia hatiani Novemba 27, mwaka jana baada ya kukiri kutenda makosa hayo mbele ya Jaji Issa Maige.

Baada ya kukiri kutenda makosa hayo, Jaji Maige alimtia hatiani na aliachiwa huru baada ya kulipa faini ya Sh milioni 200.

Mwale aliachiwa huru baada ya kukidhi masharti yaliyotolewa na Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha iliyomtaka kulipa faini ya kiasi hicho cha fedha baada ya kukiri makosa mawili ya utakatishaji fedha haramu.

Pia alihukumiwa kifungo cha miaka saba gerezani kutokana na makosa 28. Hata hivyo, mahakama hiyo ilimpunguzia adhabu hiyo baada ya kuzingatia muda aliokaa mahabusu wa zaidi ya miaka saba baada ya kukamatwa mwaka 2011.

Mbele ya Jaji Maige, mshtakiwa huyo ambaye ni kati ya watuhumiwa wanne waliokabiliwa na mashtaka hayo alikiri makosa 30 yaliyokuwa yakimkabili ikiwamo utakatishaji fedha haramu, kosa moja la kula njama, makosa matano ya kughushi nyaraka kinyume na kifungu cha 337 cha mwenendo wa kanuni ya adhabu, makosa 17 ya kughushi nyaraka kinyume na kifungu cha 338 cha mwenendo wa kanuni ya adhabu, makosa matano ya kuandaa nyaraka za uongo na kosa moja la kukutwa na mali iliyopatikana kwa njia batili.

Mwale alikuwa ni mshtakiwa wa pili kuachiwa katika kesi hiyo baada ya mshtakiwa wa pili, Don Gichana ambaye ni Raia wa Kenya kuachiwa huru Oktoba Mosi, mwaka jana baada ya kulipa faini ya Sh milioni 300.

Gichana aliachiwa baada ya kukidhi masharti yaliyotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha iliyomtaka kulipa faini ya kiasi hicho cha fedha baada ya kukiri makosa mawili yaliyokuwa yakimkabili, ikiwamo kula njama ya kutenda kosa pamoja na kutakatisha fedha haramu zaidi ya Dola za Marekani milioni 5.2.

Pia mahakama hiyo ilimuhukumu adhabu ya kwenda jela miaka mitano baada ya kukiri kula njama ya kutakatisha fedha hizo na kuhusu adhabu ya kifungo cha jela, iliamuriwa adhabu hiyo ianze kutekelezwa tangu alipokamatwa Aprili 13, 2013 hivyo aliondokana na adhabu hiyo baada ya kukaa miaka mitano mahabusu.

Akisoma hukumu hiyo ya Mwale, Jaji Maige alisema alitoa adhabu hiyo baada ya kuzingatia hoja saba zilizowasilishwa na mawakili wa utetezi walioomba mteja wao kupunguziwa adhabu katika mashtaka yaliyokuwa yakimkabili.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Boniface Mwimbwa na Elias Ndejembi waliokuwa ni wafanyakazi wa Benki ya CRDB tawi la Clock Tower jijini Arusha na wote kwa pamoja walikuwa wakikabiliwa na mashtaka 59 na kesi yao inaendelea kusikilizwa.

Novemba Mosi, mwaka jana, Mwale na wenzake walisomewa mashtaka hayo baada ya kuachiwa huru na kukamatwa tena Oktoba 31, mwaka jana na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.

Awali katika kesi hiyo ya jinai namba 61 ya mwaka 2015, washtakiwa hao walikuwa wakikabiliwa na mashtaka 44 yakiwamo ya utakatishaji fedha haramu, kughushi nyaraka na kukutwa na mali zilizopatikana kwa njia za uhalifu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles